Book of Common Prayer
Kuja Kwa Bwana
13 Kaka na dada, tunawataka mfahamu habari za wale waliokufa. Hatupendi muwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14 Tunaamini kuwa Yesu alikufa, ila tunaamini pia kuwa alifufuka. Hivyo tunaamini kuwa Mungu atawaleta katika uzima kupitia Yesu kila aliyekufa na kukusanywa pamoja naye.
15 Tunalowaambia sasa ni ujumbe wake Bwana. Sisi ambao bado tu hai Bwana ajapo tena tutaungana nae, lakini hatutawatangulia wale waliokwisha kufa. 16 Bwana mwenyewe atakuja kutoka mbinguni pamoja na sauti kuu yenye agizo, na sauti kubwa kutoka kwa malaika mkuu, na ishara ya Mungu ya mlio wa tarumbeta. Na watu waliokufa walio wake Kristo watafufuliwa kwanza. 17 Baada ya hayo, sisi ambao bado tungali hai mpaka wakati huo tutakusanywa pamoja na wale waliokwisha kufa. Tutachukuliwa juu mawinguni na kukutana na Bwana angani. Na tutakuwa na Bwana milele. 18 Hivyo tianeni moyo ninyi kwa ninyi kwa maneno haya.
Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa
6 Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.
2 Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.[a] Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. 3 Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.[b] 4 Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Lk 11:2-4)
5 Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. 6 Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga
16 Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. 17 Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, 18 ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
© 2017 Bible League International