Book of Common Prayer
Mnavyopaswa Kuishi
17 Nina kitu cha kuwaambia kutoka kwa Bwana. Ninawaonya: Msiendelee kuishi kama wale wasiomwamini Mungu wetu. Mawazo yao hayafai kitu. 18 Hawana ufahamu, na hawajui lolote kwa sababu wamekataa kusikiliza. Hivyo hawawezi kupata maisha mapya Mungu anayowapa watu. 19 Wamepoteza hisia zao za aibu na wanayatumia maisha yao kutenda yale yaliyo mabaya kimaadili. Zaidi ya hapo wanataka kutenda kila aina ya uovu. 20 Lakini aina hiyo ya maisha haiko kama ile mliyojifunza mlipomjua Kristo. 21 Najua kwamba mlisikia juu yake, na ndani yake mlifundishwa ukweli. Ndiyo, ukweli umo ndani ya Yesu. 22 Mlifundishwa kuacha utu wenu wa kale. Hii inamaanisha kwamba mnapaswa kuacha kuishi katika njia za uovu mlivyoishi zamani. Utu wenu wa kale huharibika zaidi na zaidi, kwa sababu watu hudanganywa na uovu wanaotaka kuutenda. 23 Mnapaswa kufanywa upya katika mioyo yenu na katika fikra zenu. 24 Kila mmoja wenu auvae utu ule mpya ulioumbwa kwa kufananishwa na Mungu, ambao kwa hakika una wema na ni wenye kumpendeza Mungu.
25 Hivyo mnapaswa kuacha kusema uongo, “Nyakati zote mseme ukweli tu,”(A) kwa sababu wote sisi tunahusiana na ni wa mwili mmoja. 26 “Unapokasirika, usiruhusu hasira hiyo ikusababishe wewe kutenda dhambi,”(B) na usiendelee na hasira kwa siku nzima. 27 Usimwachie Ibilisi nafasi ya kukushinda. 28 Yeyote ambaye amekuwa akiiba anapaswa kuacha kuiba na afanye kazi. Unapaswa kutumia mikono yako kufanya kitu chenye kufaa. Hapo utakuwa na kitu cha kuwashirikisha walio maskini.
29 Unapozungumza, usiseme chochote kilicho kibaya. Bali useme mambo mazuri ambayo watu wanayahitaji ili waimarike. Ndipo kile unachosema kitakuwa ni baraka kwa wale wanaokusikia. 30 Tena usimhuzunishe Roho Mtakatifu. Mungu alikupa Roho Mtakatifu kama uthibitisho kwamba wewe ni wake na kwamba atakulinda hadi siku atakapokufanya uwe huru kabisa. 31 Usiwe na uchungu, wala kukasirika. Kamwe usiongee kwa hasira au kusema chochote ili uwaumize wengine. Usifanye chochote kilicho kiovu. 32 Mwe mwema na mpendane ninyi kwa ninyi. Msameheane ninyi kwa ninyi kama Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo.
Yesu Amponya Aliyepooza
(Mk 2:1-12; Lk 5:17-26)
9 Yesu akapanda katika mashua na akasafiri kwa kukatisha ziwa kurudi kwenye mji wake. 2 Baadhi ya watu wakamletea mtu aliyepooza akiwa amelala kwenye machela. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Changamka mtoto wangu! Dhambi zako zimesamehewa.”
3 Baadhi ya walimu wa sheria walisikia alichosema Yesu. Wakaambizana wao kwa wao, “Si anamtukana Mungu mtu huyu akasema hivyo!”
4 Yesu alipotambua walichokuwa wanafikiri, akasema, “Kwa nini mna mawazo maovu kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? 5 Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kitanda chako na utembee’? 6 Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kitanda chako uende nyumbani!’”
7 Mtu yule akasimama na kwenda nyumbani. 8 Watu walipoliona tukio hili wakashangaa. Wakamsifu Mungu kwa kuwapa watu mamlaka hii.
© 2017 Bible League International