Add parallel Print Page Options

Yesu Amponya Mwana wa Afisa

(Mt 8:5-13; Lk 7:1-10)

43 Siku mbili baadaye Yesu akaondoka na kwenda Galilaya. 44 (Yesu alikwishasema mwanzoni kwamba nabii huwa haheshimiwi katika nchi yake.) 45 Alipofika Galilaya, watu wa pale walimkaribisha. Hao walikuwepo kwenye sikukuu ya Pasaka kule Yerusalemu na waliona kila kitu alichofanya huko.

46 Naye Yesu akaenda tena kutembelea Kana huko Galilaya. Kana ni mahali alikoyabadili maji kuwa divai. Mmoja wa maafisa muhimu wa mfalme alikuwa anaishi katika mji wa Kapernaumu. Mwanawe afisa huyu alikuwa mgonjwa. 47 Afisa huyo akasikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Uyahudi na sasa yuko Galilaya. Hivyo akamwendea Yesu na kumsihi aende Kapernaumu kumponya mwanawe, aliyekuwa mahututi sana. 48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu ni lazima muone ishara zenye miujiza na maajabu kabla ya kuniamini.”

49 Afisa wa mfalme akasema, “Bwana, uje kabla mwanangu mdogo hajafa.”

50 Yesu akajibu, “Nenda, mwanao ataishi.”

Mtu huyo akayaamini maneno Yesu aliyomwambia na akaenda nyumbani. 51 Akiwa njiani kwenda nyumbani watumishi wake wakaja na kukutana naye. Wakasema, “Mwanao ni mzima.”

52 Mtu huyo akauliza, “Ni wakati gani mwanangu alipoanza kupata nafuu?”

Wakajibu, “Ilikuwa jana saa saba mchana homa ilipomwacha.”

53 Baba yake akatambua kuwa saa saba kamili ulikuwa ndiyo ule wakati aliposema, “Mwanao ataishi.” Hivyo afisa huyo na kila mmoja katika nyumba yake wakamwamini Yesu.

54 Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu aliufanya baada ya kufika kutoka Uyahudi na Galilaya.

Read full chapter