Book of Common Prayer
8 Angalieni msichukuliwe mateka na mafundisho ya uongo kutoka kwa watu wasio na chochote cha maana kusema, bali kuwadanganya tu. Mafundisho yao hayatoki kwa Kristo bali ni desturi za kibinadamu tu na zinatoka katika nguvu za uovu zinazotawala maisha ya watu. 9 Nasema hili kwa sababu Mungu mwenyewe kama alivyo, ukamilifu wa uungu wake unaishi ndani ya Kristo. Hii ni hata wakati wa maisha yake hapa duniani. 10 Na kwa sababu ninyi ni wa Kristo basi mmekamilika, na mna kila kitu mnachohitaji. Kristo ni mtawala juu ya kila nguvu na mamlaka zingine zote.
11 Mlitahiriwa katika Kristo kwa namna tofauti, si kwa mikono ya kibinadamu. Hii ni kusema ya kwamba, mlishiriki katika kifo cha Kristo, ambacho kilikuwa aina ya tohara kwa namna ya kuuvua mwili wake wa kibinadamu.[a] 12 Na mlipobatizwa, mlizikwa na kufufuka pamoja naye kutokana na imani yenu kwa nguvu za Mungu aliyemfufua Kristo kutoka katika kifo.
13 Mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi zenu na kwa sababu hamkuwa sehemu ya watu wa Mungu.[b] Lakini Mungu amewapa ninyi uhai mpya pamoja na Kristo na amewasamehe dhambi zenu zote. 14 Kwa sababu tulizivunja sheria za Mungu, tunalo deni. Kumbukumbu ya deni hilo imeorodhesha amri zote tulizoshindwa kuzifuata. Lakini Mungu ametusamehe deni hilo. Ameiondoa kumbukumbu yake na kuipigilia msalabani. 15 Pale msalabani, aliwanyang'anya watawala wa ulimwengu wa roho nguvu na mamlaka. Aliwashinda pale. Na akawafukuza kama wafungwa ili ulimwengu wote uone.
Msizifuate Sheria Zilizowekwa na Watu
16 Hivyo msimruhusu mtu yeyote awahukumu katika masuala yanayohusu kula au kunywa au kwa kutofuata desturi za Kiyahudi (kusherehekea siku takatifu, sikukuu za Mwandamo wa Mwezi,[c] au siku za Sabato). 17 Zamani mambo hayo yalikuwa kama kivuli cha yale yaliyotarajiwa kuja. Lakini mambo mapya yaliyotarajiwa kuja yanapatikana katika Kristo. 18 Watu wengine hufurahia kutenda mambo yanayowafanya wajisikie kuwa ni wanyenyekevu na kisha kushirikiana na malaika katika ibada.[d] Nao wanazungumza juu ya kuyaona mambo hayo katika maono. Msiwasikilize wanapowaambia kuwa mnakosea kwa sababu hamfanyi mambo haya. Ni ujinga kwao kujisikia fahari kwa kufanya hivyo, kwa sababu mambo hayo yote yanatokana na namna mwanadamu anavyofikiri. 19 Hawajafungamanishwa na kichwa; Kristo ndiye kichwa, na mwili wote humtegemea Yeye. Kwa sababu ya Kristo viungo vyote vya mwili vinatunzana na kusaidiana kila kimoja na kingine. Hivyo mwili hupata nguvu zaidi na kufungamana pamoja kadri Mungu anavyouwezesha kukua.
20 Mlikufa pamoja na Kristo na kuwekwa huru kutoka katika nguvu zinazotawala dunia. Hivyo kwa nini mnaishi kama watu ambao bado mngali wa ulimwengu? Nina maana kuwa, kwa nini mnafuata sheria hizi: 21 “Usile hiki”, “Usionje kile”, “Usiguse kile”? 22 Sheria hizi zinazungumzia vitu vya kidunia, vitu vinavyotokomea baada ya kutumiwa. Ni amri na mafundisho ya kibinadamu tu. 23 Sheria hizi zinaweza kuonekana za busara kama sehemu ya dini zilizoundwa na watu ambamo watu huiadhibu miili yao na kutenda mambo yanayowafanya wajisikie wanyenyekevu. Lakini sheria hizi haziwasaidii watu kuthibiti tamaa zao za udhaifu wa kibinadamu.
Yesu Aanza Kazi yake Galilaya
(Mk 1:14-15; Lk 4:14-15)
12 Yesu aliposikia kuwa Yohana alikuwa amefungwa gerezani, alirudi katika wilaya ya Galilaya. 13 Lakini aliondoka Nazareti. Alikwenda kuishi Kapernaumu, mji ulio kando kando ya Ziwa Galilaya katika eneo la Zabuloni na Naftali. 14 Hili lilitokea ili kutimiza maneno aliyosema nabii Isaya:
15 “Sikilizeni, enyi nchi ya Zabuloni na Naftali,
nchi iliyo kando ya barabara iendayo baharini,
ng'ambo ya Mto Yordani!
Galilaya, wanapokaa Mataifa.
16 Watu wanaoishi katika giza ya kiroho,
nao wameiona nuru iliyo kuu.
Nuru hiyo imeangaza kwa ajili yao wale
wanaoishi katika nchi yenye giza kama kaburi.”(A)
17 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaambia watu ujumbe wake unaosema, “Mbadili mioyo yenu na maisha yenu pia, kwa sababu Ufalme wa Mungu umewafikia.”
© 2017 Bible League International