Book of Common Prayer
1 Tunataka tuwaambie juu ya Neno[a] linalo toa uzima. Yeye aliyekuwepo tangu mwanzo. Huyu ndiye yule tuliyemsikia na kumwona kwa macho yetu. Tuliyaona mambo aliyeyafanya, na mikono yetu ilimgusa. 2 Ndiyo, yeye aliye uzima alidhihirishwa kwetu. Tulimwona, na hivyo tunaweza kuwaeleza wengine juu yake. Sasa tunawaeleza habari kwamba yeye ndiye uzima wa milele aliyekuwa pamoja na Mungu Baba na alidhihirishwa kwetu. 3 Tuna wasimulia mambo tuliyoyaona na kuyasikia kwa sababu tunawataka muwe na ushirika pamoja nasi. Ushirika tulionao ni pamoja na Mungu Baba na mwanaye Yesu Kristo. 4 Tunawaandikia mambo haya ili furaha yetu iwe kamili.
Mungu Anatusamehe Dhambi Zetu
5 Tulisikia mafundisho ya kweli toka kwa Mungu. Na sasa tunayasimulia kwenu. Mungu ni nuru, na ndani yake hamna giza. 6 Kwa hiyo kama tukisema kuwa tunashirikiana na Mungu, lakini tukaendelea kuishi katika giza, tunakuwa ni waongo, tusioifuata kweli. 7 Tunapaswa kuishi katika nuru, ambamo Mungu yupo. Kama tunaishi katika nuru, tunashirikiana sisi kwa sisi, na sadaka ya damu yake Yesu, Mwana wa Mungu, inatutakasa kila dhambi.
Yesu Awafariji Wafuasi Wake
14 Yesu akasema, “Msisumbuke. Mwaminini Mungu, na mniamini na mimi. 2 Kuna vyumba vya kutosha katika nyumba ya Baba yangu. Nisingewaambia hivi ikiwa isingelikuwa kweli. Ninaenda huko kuandaa mahali kwa ajili yenu. 3 Nitakapomaliza kuandaa, nitarudi. Kisha nitawachukua ili muwe pamoja nami mahali niliko. 4 Mnaijua njia iendayo kule ninakokwenda.”
5 Thomaso akasema, “Bwana, hatujui unakokwenda, sasa tutaijuaje njia?”
6 Yesu akajibu, “Mimi ndiye njia, kweli, na uzima. Njia pekee ya kwenda kwa Baba ni kupitia kwangu. 7 Kwa kuwa sasa ninyi nyote mmenijua, mtamjua Baba yangu pia. Kwa kweli, sasa mnamjua Baba na mmekwisha kumwona.”
© 2017 Bible League International