Book of Common Prayer
Habari Njema Kuhusu Yesu Kristo
15 Sasa ndugu zangu, ninataka mkumbuke Habari Njema niliyowahubiri. Mliupokea ujumbe huo na endeleeni kuishi kwa kuufuata. 2 Habari Njema hiyo, ujumbe mliousikia kutoka kwangu, ni njia ya Mungu kuwaokoa. Ni lazima mwendelee kuuamini. Ikiwa mtaacha, kuamini kwenu ni bure.
3 Niliwapa ujumbe nilioupokea. Niliwaambia ukweli muhimu zaidi ya kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema; 4 kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema 5 na kwamba alimtokea Petro kisha mitume kumi na wawili. 6 Baada ya hilo, aliwatokea waamini wengine zaidi ya mia tano kwa wakati mmoja. Wengi wao bado wanaishi sasa, lakini wengine wamekwisha kufa. 7 Kisha alimtokea Yakobo na baadaye aliwatokea mitume wote. 8 Mwisho wa yote kabisa alinitokea mimi. Nilikuwa tofauti, kama mtoto anayezaliwa wakati usiostahili.
9 Mitume wengine wote ni wakuu kuliko mimi. Ninasema hivi kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. Ndiyo sababu sistahili hata kuitwa mtume. 10 Lakini, kwa sababu ya neema ya Mungu, ndivyo hivi nilivyo. Na neema aliyonipa haikupotea bure bila manufaa. Nilifanya kazi kwa bidii kuliko mitume wengine wote. (Lakini, kwa hakika si mimi niliyekuwa nafanya kazi. Ni neema ya Mungu iliyo ndani yangu.) 11 Hivyo basi, si muhimu ikiwa ni mimi au mitume wengine ndiyo waliowahubiri, sisi sote tunawahubiri watu ujumbe huo huo, na hiki ndicho mlichoamini.
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mt 28:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)
16 Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalena, Maria mama yake Yakobo, na Salome wakanunua manukato yenye harufu nzuri ili kuyapaka kwenye mwili wa Yesu. 2 Alfajiri na mapema Jumapili, mara tu baada ya jua kuchomoza, walienda kwenye kaburi la Yesu. 3 Nao walikuwa wakiambiana wao kwa wao, ni nani atakayelivingirisha jiwe litoke katika mlango wa kaburi kwa ajili yetu?
4 Kisha wakatazama juu na wakaona kuwa jiwe lile kubwa lilikuwa limevingirishwa tayari litoke mlangoni mwa kaburi la Yesu. 5 Walipoingia kaburini, wakamwona kijana mmoja ameketi upande wa kulia naye alikuwa amevaa vazi jeupe, nao wakastaajabu.
6 Naye akamwambia, “Usistaajabu. Unamtafuta Yesu wa Nazareti, aliyesulubiwa? Tazama amefufuka! Hayupo hapa. Angalieni mahali walipokuwa wameweka mwili wake. 7 Hata hivyo nendeni na kuwaeleza wafuasi wake pamoja na Petro kwamba: ‘Ametangulia mbele yenu kuelekea Galilaya. Mtamkuta kule, kama alivyowaambia.’”
8 Kwa hiyo wale wanawake walitoka na kukimbia kutoka kaburini, kwa sababu hofu na mshangao ulikuwa umewajia. Nao hawakusema chochote kwa mtu yeyote kwani waliogopa.[a]
© 2017 Bible League International