Book of Common Prayer
8 Ndugu zangu, tunapenda mfahamu juu ya mateso tuliyoyapata hapa Asia. Tulikuwa na mzigo sana huko, ulikuwa mzito kuliko hata nguvu zetu. Hata tulipoteza tumaini la kuishi. 9 Ukweli ni kuwa, ilionekana kana kwamba Mungu alikuwa anatuambia kuwa tunakwenda kufa. Lakini haya yalitokea ili tusizitumainie nguvu zetu bali tumtumainie Mungu, ambaye huwainua watu toka mautini. 10 Yeye alituokoa toka katika hatari hizi kubwa za mauti, na ataendelea kutuokoa. Twajisikia kuwa na hakika kuwa ataendelea kutuokoa. 11 Nanyi mnaweza kutusaidia kwa njia ya maombi. Ndipo watu wengi wataweza kumshukuru Mungu kwa ajili yetu; kwamba Mungu alitubariki kutokana na maombi yao mengi.
Mabadiliko katika Mipango ya Paulo
12 Hili ndilo tunalojivunia, na naweza kusema kwa dhamiri safi kwamba ni kweli: Katika kila kitu tulichofanya duniani, Mungu ametuwezesha kukifanya kwa moyo safi. Na hili ni kweli zaidi katika yale tuliyowatendea ninyi. Tulifanya hivyo kwa neema ya Mungu, si kwa hekima ambayo ulimwengu unayo. 13 Tunawaandikia mambo mnayoweza kusoma na kuyaelewa. Na nina matumaini kuwa mtayaelewa inavyopasa 14 kama ambavyo tayari mmekwisha kuyafahamu mambo mengi kuhusu sisi. Natumaini mtaelewa kuwa mnaweza kuona fahari juu yetu, kama nasi tutakavyoona fahari juu yenu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja.
15 Nilikuwa na uhakika sana juu ya haya yote. Ndiyo maana niliweka mpango wa kuwatembelea kwanza. Kisha mngebarakikwa mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nilipokuwa nikienda Makedonia na nilipokuwa ninarudi. Na nilipanga kuwaomba mniletee kutoka huko hadi Yudea chochote ambacho nilihitaji kwa ajili ya safari yangu. 17 Je! Mnadhani nilipanga mipango hii bila kufikiri? Au mnadhani ninafanya mipango kama vile dunia inavyofanya, lugha yetu kwenu si ndiyo na hapana kwa wakati mmoja.
18 Kama ambavyo kwa hakika mnaweza kumwamini Mungu, basi mnaweza kuamini kuwa lile tunalowaambia kamwe haliwezi kuwa ndiyo na hapana kwa pamoja. 19 Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, Yeye ambaye Sila, Timotheo, na mimi tuliwaeleza habari zake, hakutokea kuwa ni ndiyo na hapana kwa ahadi za Mungu. Kinyume chake ndiyo ya Mungu imethibitika daima katika Kristo kuwa ni ndiyo. 20 Ndiyo kwa ahadi zote za Mungu katika Kristo. Na hii ndiyo maana twasema “Amina” Katika Kristo kwa utukufu wa Mungu. 21 Na Mungu ndiye anayewafanya ninyi na sisi kuwa imara katika Kristo. Mungu pia ndiye aliyetuchagua kwa ajili ya kazi yake.[a] 22 Aliweka alama yake juu yetu ili kuonesha kuwa tu mali yake. Ndiyo, amemweka roho wake ndani ya mioyo yetu kama malipo ya awali yanayotuhakikishia mambo yote atakayotupa.
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mt 21:23-27; Lk 20:1-8)
27 Yesu na wanafunzi wake walirudi Yerusalemu. Na walipokuwa wakitembea ndani ya viwanja vya Hekalu, viongozi wa makuhani, walimu wa Sheria na wazee walimjia Yesu 28 na kumwuliza, “Kwa mamlaka gani unafanya vitu hivi? Nani alikupa mamlaka ya kuvifanya?”
29 Yesu akawaambia, “Nitawauliza swali, na mkinijibu, ndipo nitawaeleza kwa mamlaka gani ninafanya vitu hivi. 30 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni ama ulitoka kwa watu? Sasa mnijibu basi.”
31 Walijadiliana wao kwa wao wakisema, “Tukisema ‘ulitoka mbinguni’, atasema, ‘Kwa nini basi hamumuamini?’ 32 Lakini kama tukisema kuwa ubatizo wa Yohana ulitoka kwa wanadamu, watu watatukasirikia.” Viongozi waliwaogopa watu, kwani watu wote waliamini kuwa Yohana kweli alikuwa nabii.
33 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.”
Hivyo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”
© 2017 Bible League International