Book of Common Prayer
Yesu Alituagiza Kuwapenda Wengine
7 Wapendwa rafiki zangu, siwaandiki ninyi amri mpya. Ni amri ile ile ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ni fundisho lile lile ambalo mmekwishalisikia. 8 Lakini kile ninachokiandika pia ni amri mpya. Ni kweli; Mnaweza kuiona kweli ndani ya Yesu na ndani yenu ninyi wenyewe. Giza linatoweka, na nuru ya kweli tayari inang'aa.
9 Mtu anaweza kusema, “Niko nuruni,” lakini ikiwa anamchukia ndugu yeyote katika familia ya Mungu, basi angali bado katika giza. 10 Wao wanaowapenda ndugu wanaishi katika nuru, na hakuna kitu ndani yao cha kuwafanya watende mabaya. 11 Lakini yeyote anayemchukia nduguye wa kike au wa kiume yuko gizani. Anaishi katika giza. Hajui anakoenda, kwa sababu giza limemfanya asiweze kuona.
12 Ninawaandikia, ninyi watoto wapendwa,
kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa njia ya Kristo.
13 Ninawaandikia, ninyi akina baba,
kwa sababu mnamjua yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia, ninyi vijana,
kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
14 Ninawaandikia ninyi watoto,
kwa sababu mnamjua Baba.
Ninawaandikia ninyi, akina baba,
kwa sababu mnamfahamu yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia ninyi, vijana,
kwa sababu mna nguvu.
Mafundisho ya Neno la Mungu yimo ndani yenu,
na mmemshinda yule mwovu.
15 Msiipende dunia hii ya uovu wala mambo yaliyomo ndani yake. Kama mkiipenda dunia, upendo wa baba haumo ndani yenu. 16 Yote yaliyomo katika dunia: yaani, tamaa halisi za kibinadamu, tamaa kwa yale mabaya tunayoyaona, na kiburi cha vitu tulivyonavyo. Lakini hakuna hata mojawapo ya haya litokalo kwa Baba. Yote yanatoka katika dunia. 17 Dunia inapita, na mambo yote ambayo watu wanayataka kutoka katika dunia nayo yanapita. Lakini yeyote atendaye mambo ambayo Mungu anayataka ataishi milele.
Baadhi ya Wafuasi Wamwona Yesu
(Mt 28:9-10; Yh 20:11-18; Lk 24:13-35)
9 Baada ya Yesu kufufuka alfajiri na mapema siku ya Jumapili, alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye awali alifukuza mashetani saba kutoka kwake. 10 Baada ya Mariamu kumwona Yesu, alienda na kuwaeleza wanafunzi wake. Walikuwa wamehuzunishwa sana na walikuwa wakilia. 11 Lakini Mariamu aliwaambia kwamba Yesu yu hai. Aliwaambia ya kwamba yeye amemwona, lakini wao hawakumwamini.
12 Baada ya hayo, Yesu kwa namna tofauti akawatokea wanafunzi wake wawili walipokuwa wakitembea kuelekea mashambani. 13 Hawa kisha walirudi na wakawasimulia wengine wote, lakini nao hawakuwaamini.
Yesu Awatokea Wafuasi Wake
(Mt 28:16-20; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)
14 Baadaye, Yesu aliwatokea wale mitume kumi na mmoja walipokuwa wakila. Naye akawakaripia kwa kutokuwa na imani. Walikuwa wakaidi na walikataa kuwaamini wale waliomwona Yesu baada ya kufufuka kwake.
15 Naye akawaambia, “Nendeni ulimwenguni pote, na mkahubiri Habari Njema kwa uumbaji wote. 16 Yeyote atakayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Na wale waaminio wataweza kufanya ishara hizi kama uthibitisho: watafukuza mashetani kwa jina langu; watasema kwa lugha mpya wasizojifunza bado; 18 watakamata nyoka kwa mikono yao; na ikiwa watakunywa sumu yoyote, haitawadhuru; wataweka mikono yao kwa wagonjwa, nao watapona.”
Yesu Arudi Mbinguni
(Lk 24:50-53; Mdo 1:9-11)
19 Hivyo baada ya Bwana Yesu kuzungumza nao, alichukuliwa mbinguni, kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu. 20 Na mitume wakatoka na kwenda kuhubiri kila mahali, na Bwana alifanya kazi pamoja nao akithibitisha kuwa ujumbe wao ni wa kweli kwa ishara zilizofuatana na mahubiri yao.
© 2017 Bible League International