Book of Common Prayer
Yesu Kristo ni wa Muhimu Zaidi
3 Kwa hiyo sasa, kaka na dada zangu, furahini kwa kuwa ninyi ni wa Bwana. Sisiti kuwaandikia mambo haya haya, kwa sababu yatawasaidia ninyi kuwa imara na salama.
2 Mjihadhari na mbwa, mjihadhari na wafanyakazi waovu, mjihadhari na watu wanaotaka kumkata kila mtu ambaye hajatahiriwa.[a] 3 Lakini sisi ndiyo wenye tohara[b] ya kweli, tunaomwabudu Mungu kupitia Roho wake. Hatutumaini katika namna tulivyo kwa kuzaliwa au kwa yale tuliyoyakamilisha. Tunajivuna kuwa sisi ni milki ya Kristo Yesu. 4 Hata kama ninaweza kujitumainisha mimi mwenyewe, bado sifanyi hivyo. Ikiwa kuna watu wanadhani wana sababu za kutumaini sifa za kibinadamu, wanapaswa kujua kuwa nina sababu zaidi za kufanya hivyo. 5 Nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Mimi ni Myahudi wa kabila la Benjamini. Mimi ni Mwebrania halisi, hata wazazi wangu pia. Nikawa Farisayo na nilitii torati kwa uangalifu sana. 6 Nilikuwa na hamu sana ya kumridhisha Mungu[c] hata nikalitesa kanisa. Kwa usahihi niliitii sheria ya Musa.
7 Wakati fulani mambo haya yote yalikuwa muhimu kwangu. Lakini kwa sababu ya Kristo, sasa ninayachukulia mambo haya yote kuwa yasiyo na thamani. 8 Na si haya tu, lakini sasa ninaelewa kuwa kila kitu ni hasara tu ukilinganisha na thamani kuu zaidi ya kumjua Kristo Yesu, ambaye sasa ni Bwana wangu. Kwa ajili yake nilipoteza kila kitu. Na ninayachukulia yote kama kinyesi, ili nimpate Kristo. 9 Ninataka niwe wake. Katika Kristo ninayo haki mbele za Mungu, lakini kuwa na haki mbele za Mungu hakuji kwa kuitii sheria, Bali inakuja toka kwa Mungu kupitia imani kwa[d] Kristo. Mungu anatumia imani yangu kwa Kristo kunihesabia haki. 10 Ninachotaka ni kumjua Kristo na nguvu iliyomfufua kutoka kwa wafu. Ninataka kushiriki katika mateso yake na kuwa kama yeye hata katika kifo chake. 11 Kisha mimi mwenyewe naweza kuwa na matumaini kwamba nitafufuliwa kutoka kwa wafu.
Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato
(Mt 27:1-2,11-31; Mk 15:1-20; Lk 23:1-25)
28 Kisha walinzi wakamchukua Yesu kutoka katika nyumba ya Kayafa kwenda kwenye jumba la mtawala wa Kirumi. Nayo ilikuwa ni mapema asubuhi. Wayahudi waliokuwa pale wasingeweza kuingia ndani ya jumba hilo. Wao hawakutaka kujinajisi wenyewe kwa sababu walitaka kuila karamu ya Pasaka. 29 Kwa hiyo Pilato akatoka nje kuwafuata na akawauliza, “Mnasema mtu huyu amefanya makosa gani?”
30 Wakajibu, “Yeye ni mtu mbaya. Ndiyo maana tumemleta kwako.”
31 Pilato akawaambia, “Mchukueni wenyewe na kumhukumu kufuatana na sheria yenu.” Viongozi wa Wayahudi wakamwambia, “Lakini sheria yako haituruhusu sisi kumwadhibu mtu yeyote kwa kumwua.” 32 (Hii ilikuwa ni kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu juu ya jinsi ambavyo angekufa.)
33 Kisha Pilato alirudi ndani ya jumba lile. Aliagiza Yesu aje na akamuuliza, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”
34 Yesu akajibu, “Je, hilo ni swali lako mwenyewe au watu wengine wamekuambia juu yangu?”
35 Pilato akajibu, “Mimi sio Myahudi! Ni watu wako mwenyewe na viongozi wa makuhani waliokuleta kwangu. Je, umefanya kosa gani?”
36 Yesu akajibu, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ungekuwa hivyo, watumishi wangu wangenipigania ili nisikabidhiwe kwa viongozi wa Wayahudi. Hapana, ufalme wangu sio wa kidunia.”
37 Pilato akasema, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?”
Yesu akamjibu, “Uko sahihi unaposema kuwa mimi ni mfalme. Nami nilizaliwa kwa ajili ya hili: kuwaeleza watu juu ya kweli. Ni kwa sababu hii nalikuja ulimwenguni. Kila mmoja aliye wa upande wa kweli hunisikiliza.”
38 Pilato akasema, “Kweli ndiyo nini?” Kisha alitoka nje tena kwenda kwa viongozi wa Wayahudi na kuwaimbia, “Mimi sipati kitu chochote kibaya cha kumpinga mtu huyu.
© 2017 Bible League International