Book of Common Prayer
20 Je, hii inasema nini kuhusu mwenye hekima, mtaalamu wa sheria au yeyote katika ulimwengu huu mwenye ujuzi wa kutengeneza hoja zenye nguvu? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upuuzi. 21 Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu katika hekima yake aliamua kuwa hawezi kupatikana kwa kutumia hekima ya ulimwengu. Hivyo Mungu aliutumia ujumbe unaoonekana kuwa upuuzi kuwaokoa wale wanaouamini.
22 Na hii ndiyo sababu Wayahudi wanataka ishara za miujiza na Wayunani wanataka hekima. 23 Lakini ujumbe tunaomwambia kila mtu unahusu Masihi aliyekufa msalabani. Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi na kwa Wayunani ni upuuzi. 24 Lakini kwa Wayahudi na Wayunani walioteuliwa na Mungu, Masihi huyu aliyesulibiwa ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. 25 Maana upumbavu wa Mungu ni hekima zaidi ya hekima ya kibinadamu, na udhaifu wa Mungu ni nguvu zaidi ya nguvu ya kibinadamu.
26 Kaka na dada zangu, fikirini kuhusu hili kwamba Mungu aliwachagua ili muwe milki yake. Wachache wenu mlikuwa na hekima kwa namna dunia inavyoichukulia hekima. Wachache wenu mlikuwa mashuhuri na wachache wenu mnatoka katika familia maarufu. 27 Lakini Mungu aliyachagua mambo ambayo wanadamu huyachukulia kuwa ya kipumbavu ili ayaaibishe yenye hekima. Aliyachagua mambo yanayoonekana kuwa manyonge ili ayaaibishe yenye nguvu. 28 Aliwachagua wasio kitu ili ayaangamize yale ambayo ulimwengu unadhani ni muhimu. 29 Mungu alifanya hivi ili mtu yeyote asisimame mbele zake na akajisifu kuwa yeye ni bora kuliko mwingine. 30 Lakini Mungu ameyafungamanisha maisha yenu na Kristo Yesu. Yeye alifanywa kuwa hekima yetu kutoka kwa Mungu. Na kupitia kwake tumehesabiwa haki na Mungu na tumefanywa kuwa watakatifu. Kristo ndiye aliyetuokoa, akatufanya watakatifu na akatuweka huru mbali na dhambi. 31 Hivyo, kama Maandiko yanavyosema, “Kila anayejisifu, ajisifu juu ya Bwana tu.”(A)
Yesu Aanza Kazi yake Galilaya
(Mt 4:12-17; Lk 4:14-15)
14 Baada ya Yohana kuwekwa gerezani, Yesu akaja katika wilaya karibu na Ziwa Galilaya, huko aliwatangazia watu Habari Njema kutoka kwa Mungu. 15 Akasema, “Wakati umefika. Ufalme wa Mungu umewafikia.[a] Mbadili mioyo yenu na maisha yenu, na kuiamini habari njema!”
Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi
(Mt 4:18-22; Lk 5:1-11)
16 Alipokuwa akitembea kando kando ya Ziwa Galilaya, Yesu alimwona Simoni[b] na Andrea ndugu yake. Hao walikuwa wavuvi na walikuwa wakizitupa nyavu zao ziwani kukamata samaki. 17 Yesu akawaambia, “njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine, nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” 18 Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata.
19 Kisha Yesu akaendelea mbele kidogo na akawaona ndugu wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na kaka yake Yohana. Yesu aliwaona wakiwa kwenye mashua wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. 20 Naye akawaita mara moja. Hivyo wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua na watu waliowaajiri na kumfuata Yesu.
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu
(Lk 4:31-37)
21 Kisha Yesu na wafuasi wake waliingia Kapernaumu. Siku ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na akaanza kuwafundisha watu. 22 Walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[c] 23 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Naye mara alipiga kelele na kusema, 24 “Unataka nini kwetu, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.”
25 Lakini Yesu akamkemea na kumwambia, “Nyamaza kimya, na kisha umtoke ndani yake.” 26 Ndipo roho yule mchafu akamfanya mtu yule atetemeke. Kisha akatoa sauti kubwa na kisha akamtoka.
27 Kila mmoja akashangazwa sana kiasi cha kuwafanya waulizane, “Hii ni nini? Ni mafundisho ya aina mpya, na mtu yule anafundisha kwa mamlaka! Yeye huwapa amri pepo wachafu nao wanamtii!” 28 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea haraka katika eneo lote la Galilaya.
© 2017 Bible League International