Book of Common Prayer
Yesu Azungumzia Uhuru kutokana na Dhambi
31 Hivyo Yesu akawaambia Wayahudi waliomwamini, “Kama mtaendelea kuyakubali na kuyatii mafundisho yangu, mtakuwa wafuasi wangu wa kweli. 32 Mtaijua kweli, na kweli hiyo itawafanya muwe huru.”
33 Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?”
34 Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. 36 Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli.
Tu Watoto wa Mungu
3 Baba ametupenda sisi sana! Hili linaonesha jinsi anavyotupenda: Tunaitwa watoto wa Mungu. Ni kweli kuwa tu watoto wa Mungu. Lakini watu waliomo duniani hawaelewi ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu, kwa sababu hawamjui yeye. 2 Wapendwa, sasa tu watoto wa Mungu. Mungu hajatuonyesha bado namna tutakavyokuwa wakati unaoukuja. Lakini tunajua ya kwamba Kristo atakapokuja tena, tutafanana naye. Tutamwona kama alivyo. 3 Ni mtakatifu, na kila aliye na matumaini haya katika yeye huendelea kuwa mtakatifu.
4 Kila atendaye dhambi huivunja sheria ya Mungu. Ndiyo, kutenda dhambi ni sawa na kuishi kinyume na sheria ya Mungu. 5 Mwajua ya kuwa Kristo alikuja kuziondoa dhambi za watu. Haimo dhambi ndani ya Kristo. 6 Hivyo kila anayeishi katika Kristo haendelei kutenda dhambi. Kama wakiendelea kutenda dhambi, kwa hakika hawajamwelewa Kristo na hawajamjua kamwe.
7 Watoto wapendwa, msimruhusu mtu yeyote kuwadanganya. Kristo daima alitenda yaliyo haki. Hivyo kuwa mwema kama Kristo, ni lazima utende yaliyo haki. 8 Mwovu amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kila anayeendelea kutenda dhambi ni mali ya Mwovu. Mwana wa Mungu alikuja kwa ajili ya hili: Kuziharibu kazi za Mwovu.
© 2017 Bible League International