Book of Common Prayer
Iweni katika Umoja na Msaidiane
2 Fikirini kuhusu kile ambacho tulichonacho kwa sababu tunamilikiwa na Kristo: hamasa aliyotuletea, faraja ya upendo wake, ushirika katika Roho wake, huruma na wema aliotuonyesha. Ikiwa mnazifurahia baraka hizi, 2 basi fanyeni yale yatakayoikamilisha furaha yangu: iweni na nia moja na mpendane ninyi kwa ninyi. Iweni na umoja katika malengo yenu na katika kufikiri kwenu. 3 Msiruhusu ubinafsi au kiburi viwe dira yenu. Badala yake muwe wanyenyekevu mkiwathamini wengine kuliko ninyi wenyewe. 4 Kila mmoja wenu asijishugulishe kwa mema yake yeye mwenyewe bali kwa mema ya wengine.
5 Hivi ndivyo mnapaswa kufikiri, kuhisi na kutenda katika maisha yenu kwa pamoja, kama vile Kristo Yesu alivyofikiri:
6 Alikuwa sawa na Mungu katika namna zote,
lakini hakufikiri kwamba kuwa sawa na Mungu
kilikuwa kitu cha manufaa kwake.
7 Badala yake, aliacha kila kitu,
hata sehemu yake pamoja na Mungu.
Akakubali kuwa kama mtumwa,
akiwa katika umbo la binadamu.
Wakati wa maisha yake kama mtu,
8 Alijinyenyekeza na akawa mtiifu kabisa kwa Mungu,
hata jambo hilo liliposababisha kifo chake msalabani.
9 Hivyo ndiyo sababu Mungu alimpa mahali pa heshima sana,
na akampa jina lililo kuu kuliko majina yote.
10 Hivyo kila mtu atasujudu kumheshimu Yesu.
Kila mmoja aliye mbinguni, duniani na wale walio chini ya dunia.
11 Wote watakiri kwamba, “Yesu Kristo ni Bwana,”
na hili litamtukuza Mungu Baba.
Iweni Kama Mungu Anavyotaka
12 Rafiki zangu wapendwa, daima mnatii yale mliyofundishwa. Kama mlivyotii nilipokuwa pamoja nanyi, ni muhimu zaidi na zaidi kwamba mtii wakati huu ambapo sipo pamoja nanyi. Hivyo ni lazima mwendelee kuishi katika namna inayoleta maana kwa wokovu wenu. Fanyeni hivi kwa wingi wa heshima na utii kwa Mungu. 13 Ndiyo, Mungu ndiye anayetenda kazi ndani na miongoni mwenu. Anawasaidia ninyi kutaka kutenda yanayomfurahisha, naye anawapa nguvu ya kuyatenda.
Petro Amkana Yesu
(Mt 26:69-70; Mk 14:66-68; Lk 22:55-57)
15 Simoni Petro na mmoja wa wafuasi wengine wa Yesu walienda pamoja na Yesu. Mfuasi huyu alimfahamu kuhani mkuu. Hivyo akaingia pamoja na Yesu ndani ya uwanja wa nyumba ya kuhani mkuu. 16 Lakini Petro alisubiri nje karibu na mlango. Yule mfuasi aliyemjua kuhani mkuu alirudi nje na kuongea na mlinda mlango. Kisha alimleta Petro ndani. 17 Msichana aliyekuwepo langoni alimwambia Petro, “Je! Wewe pia ni mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro akajibu, “Hapana, mimi siye!”
18 Ilikuwa baridi, hivyo watumishi na walinzi waliwasha moto wa kuni. Walikuwa wameuzunguka, wakipasha joto miili yao naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao.
Petro Amkana Yesu tena
(Mt 26:71-75; Mk 14:69-72; Lk 22:58-62)
25 Simoni Petro alikuwa amesimama karibu na moto, akijipasha joto. Watu wengine wakamwambia Petro, “Je, wewe si mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro alikataa hilo. Akasema, “Hapana, mimi siye.”
26 Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu alikuwapo pale. Naye alikuwa ni jamaa wa mtu yule aliyekatwa sikio na Petro. Mtumishi akamwambia Petro, “Nadhani nilikuona pamoja naye pale kwenye bustani!”
27 Lakini kwa mara nyingine Petro akasema, “Hapana, sikuwa pamoja naye!” Mara tu alipomaliza kusema hayo, jogoo akawika.
© 2017 Bible League International