Book of Common Prayer
Ujumbe Wangu: Yesu Kristo Msalabani
2 Wapendwa kaka na dada zangu katika Kristo, nilipokuja kwenu, niliwaambia siri ya kweli iliyofunuliwa na Mungu. Lakini sikuja kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongea au mwenye hekima ya juu. 2 Nilipokuwa pamoja nanyi, niliamua kusahau kila kitu isipokuwa Yesu Kristo na kifo chake msalabani. 3 Nilipokuja kwenu nilikuwa mdhaifu na mwenye hofu. 4 Mafundisho na kuzungumza kwangu hakukuwa kwa maneno yenye hila. Lakini uthibitisho wa mafundisho yangu ilikuwa nguvu inayotolewa na Roho. 5 Nilifanya hivi ili imani yenu iwe katika nguvu ya Mungu siyo katika hekima ya kibinadamu.
Hekima ya Mungu
6 Tunafundisha hekima kwa watu ambao macho yao yamefunguliwa ili waione hekima ya siri ya Mungu. Si hekima ya watawala wa ulimwengu huu wanaobatilika. 7 Tunaisema hekima ya Mungu katika namna ambayo baadhi wanaweza kuiona na wengine hawawezi. Ni hekima iliyofichwa mpaka wakati huu na Mungu aliipanga hekima hii kabla ya kuumba ulimwengu, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hakuna mtawala yeyote wa ulimwengu huu aliyeielewa hekima hii. Ikiwa wangeielewa, wasingemwua Bwana wetu mkuu na mwenye utukufu mwingi msalabani. 9 Lakini kama Maandiko yanavyosema,
“Hakuna aliyewahi kuona,
hakuna aliyewahi kusikia,
hakuna aliyewahi kufikiri
kuhusu kile ambacho Mungu amewaandalia wanaompenda.”(A)
10 Lakini Mungu ametuonesha mambo haya kupitia Roho.
Roho anaweza kuchunguza mambo yote. Anajua hata siri za ndani kabisa za Mungu. 11 Hakuna mtu anayejua mawazo ya mtu mwingine. Ni roho inayoishi ndani ya mtu huyo ndiyo inajua mawazo ya mtu huyo. Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, ni Roho wa Mungu peke yake ndiye anayeyajua mawazo ya Mungu. 12 Tulipokea Roho wa Mungu, si roho wa ulimwengu. Tulimpokea Roho wa Mungu ili tuweze kujua yote aliyotupa Mungu.
13 Tunapozungumza, hatutumii hoja tulizofundishwa na wenye hekima. Bali hoja tulizofundishwa na Roho. Tunatumia hoja za Roho kuelezea kweli za Roho.
Yesu Awaponya Watu Wengi
(Mt 8:14-17; Lk 4:38-41)
29 Wakaondoka kutoka katika sinagogi na mara hiyo hiyo wakaenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mara Yesu alipoingia ndani ya nyumba watu wakamweleza kuwa mama mkwe wake Simoni alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amepumzika kitandani kwa sababu alikuwa na homa. 31 Yesu akasogea karibu na kitanda, akamshika mkono na kumsaidia kusimama juu. Ile homa ikamwacha, na yeye akaanza kuwahudumia.
32 Ilipofika jioni, baada ya jua kuzama waliwaleta kwake watu wote waliokuwa wagonjwa na waliokaliwa na mashetani. 33 Mji mzima ulikusanyika mlangoni pale. 34 Naye akawaponya watu waliokuwa na magonjwa ya kila aina, na kufukuza mashetani wengi. Lakini yeye hakuyaruhusu mashetani kusema, kwa sababu yalimjua.[a]
Yesu Aenda Katika Miji Mingine
(Lk 4:42-44)
35 Asubuhi na mapema, ilipokuwa giza na bado hakujapambazuka, Yesu aliamka na kutoka kwenye nyumba ile na kwenda mahali ili awe peke yake na kuomba. 36 Lakini Simoni na wale wote waliokuwa pamoja naye waliondoka kwenda kumtafuta Yesu 37 na walipompata, wakamwambia, “kila mmoja anakutafuta.”
38 Lakini Yesu akawaambia, “Lazima twende kwenye miji mingine iliyo karibu na hapa, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hilo ndilo nililokuja kulifanya.” 39 Hivyo Yesu alienda katika wilaya yote iliyoko mashariki mwa ziwa la Galilaya akihubiri Habari Njema katika masinagogi na kuwafungua watu kutoka katika nguvu za mashetani.
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mt 8:1-4; Lk 5:12-16)
40 Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.”
41 Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika.[b] Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” 42 Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi.
43 Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. 44 Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze,[c] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru[d] watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” 45 Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko.
© 2017 Bible League International