Book of Common Prayer
Kutii Watawala
13 Watiini watawala wa serikali. Hakuna anayeweza kutawala bila mamlaka ya Mungu. Mamlaka ya kutawala hutoka kwa Mungu. 2 Hivyo yeyote anayekuwa kinyume na serikali hakika anakuwa kinyume na kitu ambacho Mungu amekiweka. Wale walio kinyume na serikali wanajiletea adhabu wao wenyewe. 3 Watu wanaotenda mema hawawaogopi watawala. Bali wale wanaotenda mabaya ni lazima wawaogope watawala. Je, mnataka kuwa huru mbali na kuwaogopa hao? Basi mfanye yaliyo sahihi tu, nao watawasifu ninyi.
4 Watawala ni watumishi wa Mungu kwa ajili ya kuwasaidia ninyi. Lakini mkifanya yasiyo sahihi, mnayo sababu ya kuwa na woga. Hao wanayo mamlaka ya kuwaadhibu, na watayatumia mamlaka hayo. Wao ni watumishi wa Mungu ili wawaadhibu wale wanaofanya yale yasiyo sahihi. 5 Kwa hiyo mnapaswa kuitii serikali, siyo tu kwa sababu mtaadhibiwa, bali kwa sababu mnajua kuwa ni jambo lililo sahihi kufanya hivyo.
6 Na hii ndiyo sababu mnalipa kodi. Watawala hawa wanapaswa kulipwa kwa ajili ya kutimiza wajibu wao wote walionao wa kutawala. Hakika wanatumika kwa ajili ya Mungu. 7 Wapeni watu wote vile wanavyowadai. Kama wanawadai aina yoyote ya kodi, basi lipeni. Onesheni heshima kwa wale mnaopaswa kuwaheshimu. Na onesheni uadilifu kwa wale mnaopaswa kuwafanyia hivyo.
Kuwapenda Wengine Ndiyo Sheria Pekee
8 Msidaiwe chochote na mtu, isipokuwa mdaiwe upendo baina yenu. Mtu anayewapenda wengine anakuwa amefanya yote yanayoamriwa na sheria. 9 Sheria inasema, “Usizini, usiue, usiibe, usitamani kitu cha mtu mwingine.”(A) Amri hizo zote na zingine hakika zinajumlishwa na kuwa kanuni moja tu, “Mpende jirani yako[a] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.”(B) 10 Upendo hauwaumizi wengine. Hivyo kupenda ni sawa na kuitii sheria yote.
11 Nalisema hili kwa sababu mnajua kwamba tunaishi katika wakati ulio muhimu. Ndiyo, ni wakati wenu sasa kuamka kutoka usingizini. Wokovu wetu sasa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa tulipoamini kwa mara ya kwanza. 12 Usiku karibu umekwisha. Na mchana karibu unaingia. Hivyo tunapaswa kuacha kufanya chochote kinachohusiana na giza. Tunapaswa kujiandaa kuupiga uovu kwa silaha za nuru. 13 Tunapaswa kuishi katika njia sahihi, kama watu walio wa mchana. Hatupaswi kuwa na tafrija za ovyo ama kulewa. Hatupaswi kujihusisha katika dhambi ya uzinzi au ya aina yoyote ya mwenendo usiofaa. Hatupaswi kusababisha mabishano au kuwa na wivu. 14 Bali, muwe kama Kristo Yesu katika kila jambo mnalolitenda,[b] ili watu watakapowaangalia, waweze kumwona yeye. Msifikirie namna ya kuridhisha matakwa ya udhaifu wa mwanadamu na tamaa zake.
33 Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?”
34 Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. 36 Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli. 37 Najua kuwa ninyi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Lakini mmekusudia kuniua, kwa sababu hamtaki kuyakubali mafundisho yangu. 38 Nawaambia yale ambayo Baba yangu amenionyesha. Lakini ninyi mnayafanya yale mliyoambiwa na baba yenu.”
39 Wakasema, “Baba yetu ni Ibrahimu.”
Yesu akasema, “Kama mngekuwa wazaliwa wa Ibrahimu kweli, mngefanya yale aliyofanya Ibrahimu. 40 Mimi ni mtu niliyewaambia ukweli niliousikia kutoka kwa Mungu. Lakini Ibrahimu hakufanya kama hayo mnayotaka kufanya. 41 Mnafanya yale aliyofanya baba yenu.”
Lakini wakasema, “Sisi sio kama watoto ambao hawajawahi kumjua baba yao ni nani. Mungu ni Baba yetu. Ni baba pekee tuliye naye.”
42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu kweli, mngenipenda. Nilitoka kwa Mungu, na sasa niko hapa. Sikujileta kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mungu alinituma. 43 Hamuyaelewi mambo ninayosema, kwa sababu hamuwezi kuyakubali mafundisho yangu. 44 Baba yenu ni ibilisi. Ninyi ni wa kwake. Nanyi mnataka kufanya anayotaka. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo. Siku zote alikuwa kinyume na ukweli. Hakuna ukweli ndani yake. Yuko kama uongo anaousema. Ndiyo, ibilisi ni mwongo. Na ni baba wa uongo.
45 Nawaambieni ukweli, na ndiyo maana hamniamini. 46 Kuna mtu miongoni mwenu anayeweza kunishuhudia kuwa mimi nina hatia ya dhambi? Kama nawaeleza ukweli, kwa nini hamniamini? 47 Yeyote aliye wa Mungu huyapokea anayosema. Lakini ninyi hamuyapokei anayosema Mungu, kwa sababu ninyi si wa Mungu.”
© 2017 Bible League International