Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Marko 6:1-29

Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao

(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)

Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.

Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.

Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake

(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)

Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”

12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[a] wagonjwa wengi na kuwaponya.

Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji

(Mt 14:1-12; Lk 9:7-9)

14 Mfalme Herode alisikia habari hii kwani umaarufu wa Yesu ulikuwa umeenea mahali pote. Watu wengine walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana ana uwezo wa kufanya miujiza.”

15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”

Wengine walisema, “Yeye ni nabii kama mmoja wa manabii wa zamani.”

16 Lakini Herode aliyasikia haya na kusema, “Yohana, yule mtu niliyemkata kichwa, amefufuka kutoka kifo.”

Yohana Mbatizaji Alivyouawa

17 Kwa kuwa Herode mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kumkamata Yohana na kumweka gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mkewe Filipo kaka yake ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Kwani Yohana alizidi kumwambia Herode, “Si halali kwako kisheria kumwoa mke wa kaka yako.” 19 Herodia alikuwa na kisa na Yohana. Hivyo alitaka auwawe, lakini hakuweza kumshawishi Herode kumuua Yohana. 20 Hii ni kwa sababu Herode alimhofu Yohana. Herode pia alifahamu ya kuwa Yohana alikuwa ni mtu mtakatifu na mwenye haki, hivyo akamlinda. Herode alimpomsikia Yohana, alisumbuka sana; lakini alifurahia kumsikiliza.

21 Lakini muda maalumu ukafika; katika siku ya kuzaliwa kwake. Herode aliandaa sherehe ya chakula cha jioni kwa maafisa mashuhuri wa baraza lake, maafisa wake wa kijeshi, na watu maarufu wa Galilaya. 22 Binti ya Herodia alipowasili ndani ya ukumbi alicheza na kumpendeza Herode na wageni aliowaalika katika sherehe hiyo.

Mfalme Herode akamwambia yule msichana, “Uniombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” 23 Akamuahidi: “Nitakupa chochote utakachoniomba, hata nusu ya ufalme wangu!”

24 Naye akatoka na kumwambia mama yake, “Niombe kitu gani?”

Mama yake akasema, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”

25 Yule msichana mara moja aliharakisha kuingia ndani kwa mfalme na kuomba: “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji katika sinia.”

26 Mfalme alisikitika sana. Lakini kwa sababu ya viapo vyake alivyovifanya mbele ya wageni wake chakulani hakutaka kumkatalia ombi lake. 27 Kwa hiyo mfalme mara moja akamtuma mwenye kutekeleza hukumu za kifo akiwa na amri ya kukileta kichwa cha Yohana. Kisha akaenda kukikata kichwa cha Yohana, 28 na kukileta katika sinia na kumpa yule msichana, na msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yohana waliposikia haya walikuja na kuchukua mwili na kuuweka ndani ya kaburi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International