New Testament in a Year
Wanawali Kumi
25 Nyakati hizo, ufalme wa Mungu utafanana na wanawali kumi waliokwenda kusubiri kuwasili kwa bwana arusi wakiwa na taa zao. 2 Watano kati yao walikuwa na hekima, na watano walikuwa wajinga. 3 Wanawali wajinga walichukua taa zao bila ya kubeba mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao. 4 Wanawali wenye hekima walichukua taa zao pamoja na mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao katika chupa. 5 Bwana arusi alipochelewa sana, walichoka na wote wakasinzia.
6 Usiku wa manane ulipofika, ikatangazwa, ‘Bwana arusi anakuja! Njooni mumlaki!’
7 Wasichana wote waliamka. Wakatayarisha taa zao. 8 Lakini wanawali wajinga wakawaambia wanawali wenye hekima, ‘Tupeni mafuta kiasi kwa sababu mafuta katika taa zetu yamekwisha.’
9 Wanawali wenye hekima wakajibu, ‘Hapana! Mafuta tuliyonayo hayatatutosha sisi sote. Lakini nendeni kwa wauza mafuta mkanunue.’
10 Hivyo wanawali wajinga wakaenda kununua mafuta. Walipoondoka, bwana arusi akafika. Wanawali waliokuwa tayari wakaingia kwenye sherehe ya arusi pamoja na bwana arusi. Kisha mlango ukafungwa.
11 Baadaye wanawali waliokwenda kununua mafuta wakarudi. Wakasema, ‘bwana, bwana! Fungua mlango tuingie.’
12 Lakini bwana arusi akajibu, ‘Kwa hakika hapana! Wala siwajui ninyi.’
13 Hivyo iweni tayari kila wakati. Hamjui siku wala muda ambao Mwana wa Adamu atakuja.
Simulizi Kuhusu Watumishi Watatu
(Lk 19:11-27)
14 Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyekuwa akiondoka nyumbani kwake kusafiri safari ndefu. Aliwaita watumishi wake na kuwaweka kuwa wasimamizi wa mali zake. 15 Alimgawia kila mtumishi kiasi cha mali atakachosimamia. Alimpa mmoja talanta[a] tano. Alimpa mtumishi mwingine talanta mbili na akampa mtumishi wa tatu talanta moja. Kisha akaondoka. 16 Mtumishi aliyepewa talanta tano alikwenda akazifanyia biashara na talanta zile tano zikazaa talanta tano zingine. 17 Mtumishi aliyepewa talanta mbili alifanya vivyo hivyo. Mtumishi huyo alizifanyia biashara talanta mbili alizopewa na zikazaa talanta mbili zingine. 18 Lakini mtumishi aliyekabidhiwa talanta moja, alikwenda akachimba shimo kisha akaifukia talanta moja aliyopewa na bwana wake.
19 Baada ya muda mrefu kupita bwana wao alirudi. Aliwauliza watumishi wake walizifanyia nini talanta alizowaachia. 20 Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano alimletea bwana wake talanta tano alizomwachia na talanta zingine tano zaidi. Mtumishi akamwambia bwana wake, ‘Bwana, uliniamini ukaniachia talanta tano kuzitunza, hivyo nilizifanyia biashara na kupata talanta tano zaidi.’
21 Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’
22 Kisha mtumishi aliyepewa talanta mbili akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana ulinipa talanta mbili ili nizitunze. Nilizifanyia biashara talanta hizi mbili na nimepata zingine mbili zaidi.’
23 Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’
24 Ndipo mtumishi aliyeachiwa talanta moja akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana, nilijua wewe ni mkorofi sana. Unavuna usichopanda. Unakusanya mazao mahali ambapo hukupanda mbegu yoyote. 25 Hivyo niliogopa. Nilienda nikaificha talanta yako ardhini. Hii hapa ni ile talanta moja ya fedha uliyonipa.’
26 Bwana wao akamjibu, ‘Wewe ni mtumishi mbaya na mvivu! Unasema kwamba ulijua ninavuna nisichopanda na ninakusanya mazao ambayo sikupanda mbegu yo yote. 27 Hivyo ungeweka pesa yangu benki. Kisha, wakati nitakaporudi ningepata talanta yangu pamoja na faida ambayo ingezalishwa na talanta yangu.’
28 Hivyo bwana wao akawaambia watumishi wake wengine, ‘Mnyang'anyeni talanta moja mtumishi huyo na kumpa mtumishi mwenye talanta kumi. 29 Kila aliyezalisha faida atapata zaidi. Atakuwa na vingi kuzidi mahitaji yake. Lakini wale wasiotumia walivyonavyo kuleta faida watanyang'anywa kila kitu.’ 30 Kisha bwana wao akasema, ‘Mtupeni nje, gizani mtumishi huyo asiyefaa, ambako watu watalia na kusaga meno kwa maumivu.’
© 2017 Bible League International