New Testament in a Year
51 Yesu alipokufa, pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili. Mpasuko wake ulianzia juu mpaka chini. Kulitokea pia tetemeko la ardhi na miamba ilipasuka. 52 Makaburi yalifunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa walifufuka kutoka kwa wafu. 53 Walitoka makaburini. Na baada ya Yesu kufufuliwa kutoka kwa wafu, walikwenda kwenye mji mtakatifu wa Yerusalemu, na watu wengi waliwaona.
54 Afisa wa jeshi na askari waliokuwa wanamlinda Yesu walitetemeka sana kwa kuogopa tetemeko la ardhi na kila walichokiona kikitokea. Wakasema, “Hakika alikuwa Mwana wa Mungu!”
55 Wanawake wengi waliomfuata Yesu kutoka Galilaya kumhudumia walikuwepo pale wakiangalia wakiwa wamesimama mbali na msalaba. 56 Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu na pia mama yao Yakobo na Yohana[a] alikuwepo pale.
Yesu Azikwa
(Mk 15:42-47; Lk 23:50-56; Yh 19:38-42)
57 Jioni ile, mtu mmoja tajiri aliyeitwa Yusufu alikuja Yerusalemu. Alikuwa mfuasi wa Yesu kutoka katika mji wa Arimathaya. 58 Alikwenda kwa Pilato na akamwomba mwili wa Yesu. Pilato akawaamuru askari wampe Yusufu wa Arimathaya mwili wa Yesu. 59 Aliuchukua mwili na kuuvingirisha katika kitambaa mororo cha kitani safi. 60 Yusufu akauzika mwili wa Yesu katika kaburi mpya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba mlimani. Kisha akalifunga kaburi kwa kuvingirisha jiwe kubwa kuziba mlango wa kaburi. Baada ya kufanya hivi, akaondoka. 61 Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu walikuwa wamekaa karibu na kaburi.
Kaburi la Yesu Lalindwa
62 Siku ile ilikuwa Siku ya Maandalizi. Siku iliyofuata, viongozi wa makuhani na Mafarisayo walimwendea Pilato. 63 Wakamwambia, “Mkuu, tunakumbuka kuwa yule mwongo alipokuwa hai alisema, ‘Nitafufuka kutoka kwa watu katika siku tatu.’ 64 Hivyo amuru ili kaburi lilindwe kwa siku tatu. Wafuasi wake wanaweza kuja na kujaribu kuiba mwili. Kisha wataweza kumwambia kila mtu kuwa alifufuka kutoka kwa wafu. Uongo huo utakuwa hatari zaidi ya hata waliyosema juu yake alipokuwa hai.”
65 Pilato akasema, “Chukueni baadhi ya askari, na mwende mkalinde kaburi kwa namna mnavyojua.” 66 Kisha walikwenda kaburini na kuliweka salama dhidi ya wezi. Walifanya hivi kwa kuliziba kwa jiwe langoni na kuwaweka askari wa kulinda kaburi.
© 2017 Bible League International