New Testament in a Year
Askari wa Pilato Wamdhihaki Yesu
(Mk 15:16-20; Yh 19:2-3)
27 Kisha askari wa Pilato wakamchukua Yesu mpaka kwenye nyumba ya gavana, kikosi kizima cha wale askari kikakusanyika pamoja kumzunguka Yesu. 28 Wakamvua nguo zake na kumvalisha kivazi chekundu.[a] 29 Kisha wakatengeneza taji kutokana na matawi ya miiba na kuiweka kwenye kichwa chake na wakaweka fimbo kwenye mkono wake wa kulia. Kisha kwa kumdhihaki, wakainama mbele zake. Wakasema, “Tunakusalimu, mfalme wa Wayahudi!” 30 Walimtemea mate. Kisha wakachukua fimbo yake na kuanza kumpiga nayo kichwani. 31 Baada ya kumaliza kumdhihaki, askari walimvua kivazi chekundu na kumvalisha nguo zake. Kisha wakamwongoza kwenda kuuawa msalabani.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mk 15:21-32; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)
32 Askari walipokuwa wanatoka mjini wakiwa na Yesu, walimwona mtu mmoja kutoka Kirene aliyeitwa Simoni, na wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 33 Walifika mahali palipoitwa Golgotha. (Yaani “Eneo la Fuvu la Kichwa”.) 34 Askari walimpa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo.[b] Lakini alipoionja, alikataa kuinywa.
35 Askari walimgongomea Yesu msalabani, kisha wakacheza kamari ili wagawane nguo za Yesu. 36 Askari walikaa pale ili kumlinda. 37 Wakaweka alama juu ya kichwa chake kuonesha mashtaka dhidi yake yaliyosema: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.
38 Wahalifu wawili waligongomewa kwenye misalaba pamoja na Yesu, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto wa Yesu. 39 Watu waliokuwa wakipita pale walitikisa vichwa vyao na kumtukana Yesu matusi 40 kwa kusema, “Ulisema ungeweza kubomoa Hekalu na kulijenga tena katika siku tatu. Jiokoe mwenyewe! Teremka chini kutoka kwenye huo msalaba ikiwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu!”
41 Viongozi wa Makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwepo pale pia. Nao pia walimdhihaki Yesu kama watu wengine walivyofanya. 42 Walisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa yeye mwenyewe! Watu husema kuwa yeye ni mfalme wa Israeli. Ikiwa yeye ni mfalme, ashuke kutoka msalabani. Ndipo tutamwamini. 43 Alimtumaini Mungu. Hivyo Mungu amwokoe sasa, ikiwa hakika Mungu anamtaka. Yeye mwenyewe alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44 Hata wale wahalifu wawili waliokuwa misalabani upande wa kulia na wa kushoto wa Yesu walimtukana.
Yesu Afariki
(Mk 15:33-41; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)
45 Ilipofika adhuhuri, giza liliifunika Israeli yote kwa muda wa masaa matatu. 46 Yapata saa tisa alasiri Yesu alilia kwa sauti kuu akisema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha peke yangu?”(A)
47 Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hili wakasema, “Anamwita Eliya.”[c]
48 Mtu mmoja alikimbia haraka akaenda kuchukua sponji, akaijaza siki, akaifunga kwenye fimbo na akanyoosha fimbo ili kumpa Yesu sponji ili anywe siki. 49 Lakini wengine walisema, “Usimjali. Tunataka tuone ikiwa Eliya atakuja kumsaidia.”
50 Yesu akalia kwa sauti kuu tena, kisha akafa.[d]
© 2017 Bible League International