New Testament in a Year
Chakula cha Bwana
(Mk 14:22-26; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)
26 Walipokuwa wakila, Yesu alichukua baadhi ya mikate na akamshukuru Mungu. Alimega baadhi ya vipande, akawapa wafuasi wake na akasema, “Chukueni mkate huu na mle. Ni mwili wangu.”
27 Kisha akachukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu na akawapa. Akasema, “Kila mmoja wenu anywe divai iliyo katika kikombe hiki. 28 Divai hii ni damu yangu, itakayomwagika ili kusamehe dhambi za watu wengi na kuanza Agano Jipya ambalo Mungu analifanya na watu wake. 29 Ninataka mjue kuwa, hii ni mara ya mwisho nitakunywa divai mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
30 Waliimba wimbo kwa pamoja kisha wakaenda kwenye Mlima wa Mizeituni.
Yesu Asema Wafuasi Wake Watamwacha
(Mk 14:27-31; Lk 22:31-34; Yh 13:36-38)
31 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Usiku wa leo ninyi nyote mtapoteza imani yangu kwangu. Maandiko yanasema,
‘Nitamwua mchungaji,
na kondoo watatawanyika.’(A)
32 Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka Kisha nitakwenda Galilaya. Nitakuwa huko kabla ninyi hamjaenda huko.”
33 Petro akajibu, “Wafuasi wengine wote wanaweza kupoteza imani juu yako. Lakini imani yangu haitatetereka.”
34 Yesu akajibu, “Ukweli ni huu, usiku wa leo utasema haunifahamu. Utanikana mara tatu kabla jogoo hajawika.”
35 Lakini Petro akajibu, “Sitasema kwamba sikufahamu! Mimi hata nitakufa pamoja nawe!” Na wafuasi wengine wote wakasema kitu hicho hicho.
Yesu Aomba Akiwa Peke Yake
(Mk 14:32-42; Lk 22:39-46)
36 Kisha Yesu akaondoka pamoja na wafuasi wake na kwenda mahali panapoitwa Gethsemane. Akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda mahali pale kuomba.” 37 Alimwambia Petro na wana wawili wa Zebedayo waende pamoja naye. Kisha akaanza kuhuzunika na kuhangaika. 38 Yesu akamwambia Petro na wana wa Zebedayo, “Moyo wangu ni mzito na wenye huzuni hata kujisikia kana kwamba huzuni hiyo itaniua. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”
39 Kisha Yesu akaenda mbele kidogo. Akainama hadi chini uso wake ukiigusa nchi akiomba na akasema, “Baba yangu, ikiwezekana, usifanye nikinywee kikombe hiki cha mateso.[a] Lakini fanya lile ulitakalo na si lile ninalolitaka mimi.” 40 Kisha akarudi walipokuwa wafuasi wake na akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Je hamkuwa na uwezo wa kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 Amkeni kesheni na kuomba ili muyashinde majaribu. Roho zenu zinataka kufanya mambo sahihi, lakini miili yenu ni dhaifu.”
42 Kisha Yesu akaenda mara ya pili na akaomba akisema, “Baba yangu, ikiwa ni lazima nikinywee kikombe hiki na haiwezekani nikakwepa, basi mapenzi yako na yatimizwe.”
43 Kisha akarudi na kwenda walipokuwa wafuasi wake, akawakuta wamelala tena. Hawakuweza kukesha. 44 Hivyo akawaacha akaenda tena kuomba. Mara hii ya tatu alipokuwa anaomba akasema kama alivyosema hapo mwanzo.
45 Kisha Yesu akawarudia wafuasi wake na akasema, “Bado mnalala na kupumzika? Wakati wa Mwana wa Adamu kukabidhiwa kwa wenye dhambi umewadia. 46 Simameni! Tuondoke. Tazama yeye atakayenikabidhi anakuja.”
Yesu Akamatwa
(Mk 14:43-50; Lk 22:47-53; Yh 18:3-12)
47 Yesu alipokuwa anazungumza, Yuda mmoja wa wanafunzi wake kumi na mbili alifika akiwa na kundi kubwa la watu, waliokuwa wamebeba majambia na marungu. Walikuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48 Yuda aliyekuwa amkabidhi Yesu kwao, alipanga kufanya kitu cha kuwajulisha yupi kati ya wafuasi alikuwa Yesu. Alisema, “Mtu nitakayembusu ndiye mtakayemkamata.” 49 Hivyo Yuda alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Salamu, Mwalimu!” Kisha akambusu.
50 Yesu akajibu, “Rafiki yangu, fanya ulilokuja kufanya.”
Kisha wale watu wakaja na kumkamata Yesu.
© 2017 Bible League International