New Testament in a Year
Simulizi Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Sherehe
(Lk 14:15-24)
22 Yesu aliendelea kuwajibu viongozi wa Kiyahudi kwa mifano zaidi. Akasema, 2 “Ufalme wa Mungu unafanana na jambo lililotokea mfalme alipoandaa sherehe ya harusi kwa ajili ya mwanaye. 3 Aliwaalika baadhi ya watu. Wakati ulipofika mfalme aliwatuma watumwa wake kuwaambia watu waende kwenye sherehe. Lakini walikataa kwenda kwenye sherehe ya mfalme.
4 Ndipo mfalme aliwaita baadhi ya watumishi wengine zaidi na akawaambia namna ya kuwaambia wale aliowaalika: ‘Njooni sasa! Sherehe imeandaliwa. Nimechinja ng'ombe wangu madume na ndama wanono waliolishwa nafaka, na kila kitu kiko tayari kuliwa. Njooni kwenye sherehe ya harusi.’
5 Lakini watu walioalikwa hawakujali yale waliyoambiwa na watumwa wa mfalme. Wengine waliondoka wakaenda kufanya mambo mengine. Mmoja alikwenda shambani na mwingine alikwenda kwenye shughuli zake. 6 Wengine waliwakamata watumwa wa mfalme, wakawapiga na kuwaua. 7 Mfalme alikasirika sana na akatuma jeshi lake kuwaua wale waliowaua watumwa wake. Na jeshi likauchoma moto mji wao.
8 Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Sherehe ya harusi iko tayari. Niliwaalika wale watu lakini hawakustahili. 9 Hivyo nendeni kwenye pembe za mitaa na mwalikeni kila mtu mtakayemwona, waambieni waje kwenye sherehe yangu.’ 10 Hivyo watumwa wake waliingia mitaani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wabaya na wema na kuwaleta kwenye sherehe. Na jumba la sherehe likawa na wageni wengi.
11 Mfalme alipoingia ili kuwasalimu wageni, alimwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi rasmi la harusi. 12 Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki ilikuwaje ukaruhusiwa kuingia humo? Hujavaa vazi nadhifu kwa arusi!’ Lakini mtu yule hakuwa na neno la kusema. 13 Hivyo mfalme akawaambia baadhi ya wale waliokuwa wanawahudumia watu kwa chakula, ‘Mfungeni mtu huyu mikono na miguu yake na mtupeni gizani, ambako watu wanalia na kusaga meno yao kwa maumivu.’
14 Ndiyo, watu wengi wamealikwa, lakini wachache tu ndiyo waliochaguliwa.”
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mk 12:13-17; Lk 20:20-26)
15 Kisha Mafarisayo wakaondoka mahali ambapo Yesu alikuwa anafundisha. Wakapanga mpango wa kumfanya aseme kitu ambacho wangekitumia dhidi yake. 16 Wakawatuma kwake baadhi ya wafuasi wao na baadhi ya watu kutoka katika kundi la Maherode. Watu hawa walipofika kwa Yesu wakasema, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu mwema na kwamba daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu, bila kujali ni nani anakusikiliza. Huna wasiwasi namna ambavyo wengine wanaweza wakasema. 17 Sasa tuambie, unadhani ni sahihi kulipa kodi kwa Kaisari au la?”
18 Lakini Yesu alijua kuwa watu hawa walikuwa wanamtega. Hivyo akasema, “Enyi wanafiki! Kwa nini mnajaribu kunitega ili niseme jambo lililo kinyume? 19 Nionesheni sarafu inayotumika kulipa kodi.” Wakamwonesha Yesu sarafu iliyotengenezwa kwa fedha. 20 Kisha Yesu akauliza, “Picha iliyo kwenye sarafu hii ni ya nani? Na jina lililo kwenye sarafu hii ni la nani?”
21 Wakajibu, “Ni picha ya Kaisari na ni jina la Kaisari.”
Ndipo Yesu akawajibu, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake na mpeni Mungu vilivyo vyake.”
22 Waliposikia yale Yesu aliyosema, wakashangaa na kuondoka.
© 2017 Bible League International