Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Luka 24

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Yh 20:1-10)

24 Asubuhi mapema sana siku ya Jumapili, wanawake walikwenda kaburini ulikolazwa mwili wa Yesu. Walibeba manukato yanayonukia vizuri waliyoyaandaa. Walikuta jiwe kubwa lililokuwa limeziba mlango wa kaburi limevingirishwa kutoka kwenye mlango wa kaburi. Waliingia kaburini, lakini hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. Hawakulielewa hili. Walipokuwa wangali wanashangaa, watu wawili waliovaa mavazi yaliyong'aa walisimama pembeni mwao. Wanawake waliogopa sana. Waliinama nyuso zao zikaelekea chini. Wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai hapa? Hapa ni mahali pa waliokufa. Yesu hayuko hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu. Mnakumbuka alivyosema alipokuwa Galilaya? Alisema kwamba, ‘Mwana wa Adamu lazima atatolewa kwa mamlaka ya watu wenye dhambi, lazima atauawa msalabani na kufufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu.’” Ndipo wanawake wakakumbuka Yesu alivyosema.

Wanawake wakaondoka kaburini na kurudi kwa mitume kumi na mmoja na wafuasi wengine. Waliwaeleza kila kitu kilichotokea kaburini. 10 Wanawake hawa walikuwa Mariamu Magdalena, Yoana, na Mariamu, mama yake Yakobo na wanawake wengine. Waliwaambia mitume kila kitu kilichotokea. 11 Lakini mitume hawakuamini yale waliyosema. Ilionekana kama upuuzi. 12 Lakini Petro alinyanyuka na kukimbia kwenda kaburini kuona. Alitazama ndani, lakini aliona nguo tu iliyotumika kuufunga mwili wa Yesu. Petro aliondoka kwenye kaburi akarudi nyumbani alikokuwa anakaa, akijiuliza nini kilichotokea.[a]

Njiani Kwenda Emausi

(Mk 16:12-13)

13 Siku hiyo hiyo, wafuasi wawili[b] wa Yesu walikuwa wanakwenda kwenye mji mdogo uitwao Emausi, uliokuwa yapata kilomita kumi na mbili[c] kutoka Yerusalemu. 14 Walikuwa wanazungumza kuhusu mambo yote yaliyotokea. 15 Walipokuwa wakizungumza, wakijadiliana juu ya mambo haya, Yesu mwenyewe aliwasogelea na akawa anatembea nao. 16 Lakini hawakuruhusiwa kumtambua. 17 Yesu akawauliza, “Ni mambo gani ninayosikia mnajadiliana mnapotembea?”

Wale wafuasi wawili wakasimama, sura zao zilionekana zenye huzuni. 18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa akasema, “Lazima wewe ni mtu pekee katika Yerusalemu ambaye hujui yaliyotokea huko.”

19 Yesu akasema, “Unasema kuhusu nini?”

Wakasema, “Ni kuhusu Yesu, kutoka Nazareti, alikuwa nabii mkuu mbele za Mungu na watu wote. Alisema na kutenda mambo makuu mengi. 20 Lakini viongozi wetu na viongozi wa makuhani walimtoa ili ahukumiwe na kuuawa. Wakampigilia msalabani. 21 Tulitegemea kuwa ndiye atakayeiweka huru Israeli. Lakini sasa haya yote yametokea.

Na sasa kitu kingine: Imekuwa ni siku tatu tangu alipouawa, 22 lakini leo baadhi ya wanawake kutoka kwenye kundi letu walituambia jambo la kushangaza. Mapema asubuhi hii walikwenda kaburini ambako mwili wa Yesu ulilazwa. 23 Lakini hawakuuona mwili wake pale. Walikuja na kutuambia kuwa wamewaona malaika. Malaika waliwaambia Yesu yu hai! 24 Hivyo baadhi ya watu walio katika kundi letu walikwenda kaburini pia. Ilikuwa kama wanawake walivyosema. Waliliona kaburi, lakini hawakumwona Yesu.”

25 Ndipo Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga na wazito wa kuyakubali yale waliyoandika manabii. 26 Manabii waliandika kwamba Masihi lazima ateseke kwa mambo haya kabla hajaingia katika utukufu wa ufalme wake.” 27 Kisha akaanza kufafanua kila kitu walichosema manabii kuhusu yeye. Alianzia katika vitabu vya Musa na kusema yale waliyosema manabii kuhusu yeye.

28 Wakakaribia mji wa Emausi, na Yesu akafanya kama vile alikuwa anaendelea mbele. 29 Lakini walimtaka akae, wakamsihi: “Kaa nasi. Tayari ni usiku. Mchana unakaribia kwisha.” Hivyo aliingia ndani kukaa nao.

30 Alipokuwa mezani pamoja nao ili kula chakula cha usiku, Yesu akachukua mkate na kushukuru. Kisha akaumega na kuwapa. 31 Baada ya kufanya hivyo, wafuasi wale wawili wakaruhusiwa kumtambua. Lakini walipojua yeye ni nani, alitoweka. 32 Wakasemezana, “Alivyokuwa anazungumza nasi tulipokuwa barabarani, tulijisikia kama moto unawaka ndani yetu. Ilitusisimua sana alipotufafanulia maana halisi ya Maandiko!”

33 Hivyo wafuasi wale wawili wa Bwana Yesu wakasimama na kurudi Yerusalemu haraka. Walipofika Yerusalemu waliwakuta mitume kumi na mmoja wamekusanyika pamoja na wafuasi wengine wa Bwana Yesu. 34 Kundi likawaambia wale wafuasi wawili, “Hakika Bwana amefufuka kutoka kwa wafu! Alimtokea Simoni.”

35 Ndipo wafuasi wawili wakaeleza kilichotokea barabarani. Wakaeleza jinsi walivyomtambua Yesu aliposhiriki mkate pamoja nao.

Yesu Awatokea Wafuasi Wake

(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)

36 Wakati wafuasi wawili wakiwa bado wanawaeleza mambo haya wafuasi wengine, Yesu mwenyewe akaja na kusimama katikati yao. Akawaambia, “Amani iwe kwenu.”

37 Wafuasi walishituka na wakaogopa. Walidhani wanaona mzimu. 38 Lakini Yesu akasema, “Kwa nini mnaogopa? Na kwa nini mnakitilia mashaka kile mnachokiona? 39 Angalieni mikono na miguu yangu. Hakika ni mimi. Niguseni. Mtaweza kuona kuwa nina mwili wenye nyama na mifupa; mzimu hauna mwili kama huu.”

40 Mara baada ya Yesu kusema haya, aliwaonesha mikono na miguu yake. 41 Wafuasi walishangaa na kufurahi sana walipoona kuwa Yesu alikuwa hai. Kwa kuwa bado walikuwa hawaamini wanachokiona, akawaambia, “Mna chakula chochote hapa?” 42 Wakampa kipande cha samaki aliyepikwa. 43 Wafuasi wake wakiwa wanaangalia akakichukua na kukila.

44 Yesu akawaambia, “Mnakumbuka nilipokuwa pamoja nanyi? Nilisema kila kitu kilichoandikwa kuhusu mimi katika Sheria ya Musa, vitabu vya manabii na Zaburi lazima kitimilike.”

45 Kisha Yesu akawafafanulia Maandiko ili waelewe maana yake halisi. 46 Yesu akawaambia, “Imeandikwa kuwa Masihi atauawa na atafufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu. 47-48 Mliona mambo haya yakitokea, ninyi ni mashahidi. Na maandiko yanasema inawapasa mwende na kuwahubiri watu kuwa ni lazima wabadilike na kumgeukia Mungu, ili awasamehe. Ni lazima mwanzie Yerusalemu na mhubiri ujumbe huu kwa jina langu kwa watu wa mataifa yote. 49 Kumbukeni kwamba nitamtuma kwenu yule ambaye Baba yangu aliahidi. Kaeni jijini mpaka mtakapopewa nguvu hiyo kutoka mbinguni.”

Yesu Arudi Mbinguni

(Mk 16:19-20; Mdo 1:9-11)

50 Yesu akawaongoza wafuasi wake kutoka nje ya Yerusalemu hadi karibu na Bethania. Akanyenyua mikono yake na kuwabariki wafuasi wake. 51 Alipokuwa anawabariki, alitenganishwa nao na kuchukuliwa mbinguni. 52 Wafuasi wake walimwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha sana. 53 Walikuwa katika Hekalu wakati wote, wakimsifu Mungu.

Yohana 20-21

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Lk 24:1-12)

20 Asubuhi na mapema siku ya Jumapili, wakati bado lilikuwepo giza, Mariamu Magdalena akaenda kwenye kaburi la Yesu. Naye akaona kuwa lile jiwe kubwa lilikuwa limeondolewa kutoka mlangoni. Hivyo akakimbia kwenda kwa Simoni Petro na kwa mfuasi mwingine (yule ambaye Yesu alimpenda sana). Akasema, “Wamemwondoa Bwana kutoka kaburini na hatujui wamemweka wapi.”

Kwa hiyo Petro na yule mfuasi mwingine wakaanza kuelekea kwenye kaburi. Wote walikuwa wakikimbia, lakini yule mfuasi mwingine alikimbia kwa kasi zaidi kuliko Petro na kuwasili wa kwanza kaburini. Alipofika akainama chini na kuchungulia ndani ya kaburi. Humo akaviona vipande vya nguo za kitani vikiwa pale chini, lakini hakuingia ndani.

Hatimaye Simoni Petro akafika kaburini na kuingia ndani. Naye aliviona vipande vile vya nguo za kitani vikiwa chini mle ndani. Pia aliiona nguo iliyokuwa imezungushwa kichwani kwa Yesu. Hii ilikuwa imekunjwa na kuwekwa upande mwingine tofauti na pale zilipokuwepo nguo za kitani. Kisha mfuasi mwingine, yule aliyefika kwanza kaburini, akaingia ndani. Yeye aliona yaliyotokea na akaamini. (Wafuasi hawa walikuwa bado hawajayaelewa yale Maandiko kwamba Yesu alipaswa kufufuka kutoka wafu.)

Yesu Amtokea Mariamu Magdalena

(Mk 16:9-11)

10 Kisha wafuasi wakarudi nyumbani. 11 Lakini Mariamu akabaki amesimama nje ya kaburi, akilia. Aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi alipokuwa akilia. 12 Mle ndani akawaona malaika wawili waliovaa nguo nyeupe na wameketi mahali ulipokuwa mwili wa Yesu. Mmoja amekaa sehemu kilipolazwa kichwa na mwingine aliketi sehemu miguu ilipokuwa imewekwa.

13 Malaika wakamwuliza Mariamu, “Mwanamke, kwa nini unalia?”

Mariamu akajibu, “Wameuondoa mwili wa Bwana wangu, na sijui wameuweka wapi.” 14 Wakati Mariamu aliposema hivi, akageuka nyuma na kumwona Yesu amesimama pale. Lakini hakujua kuwa huyo alikuwa ni Yesu.

15 Akamwuliza, “Mwanamke, kwa nini unalia? Je, unamtafuta nani?”

Yeye alifikiri kuwa huyu alikuwa ni mtunzaji wa bustani. Hivyo akamwambia, “Je, ulimwondoa Bwana? Niambie umemweka wapi. Nami nitaenda kumchukua.” 16 Yesu akamwita, “Mariamu.”

Mariamu akamgeukia na kumwambia kwa Kiaramu, “Raboni”, (hii ikiwa na maana “Mwalimu”).

17 Yesu akamwambia, “Hupaswi kunishika! Kwani bado sijapaa kwenda huko juu kwa Baba yangu. Lakini nenda ukawaambie wafuasi wangu[a] maneno haya: ‘Ninarudi kwa Baba yangu ambaye pia ni Baba yenu. Ninarudi kwa Mungu wangu ambaye pia ni Mungu wenu.’”

18 Mariamu Magdalena akaenda kwa wafuasi na kuwaambia, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaeleza yale Yesu aliyomwambia.

Yesu Awatokea Wafuasi Wake

(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Lk 24:36-49)

19 Ilikuwa siku ya Jumapili, na jioni ile wafuasi walikuwa pamoja. Nao walikuwa wamefunga milango kwa kuwa waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Ghafla, Yesu akawa amesimama pale katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 Mara baada ya kusema haya, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Wafuasi walipomwona Bwana, walifurahi sana.

21 Kisha Yesu akasema tena, “Amani iwe nanyi. Kama vile Baba alivyonituma, nami sasa nawatuma ninyi vivyo hivyo.” 22 Kisha akawapumulia pumzi na kusema, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Mkisamehe dhambi zake mtu yeyote, dhambi zake hizo zitasamehewa. Kama kuna mtu yeyote ambaye hamtamsamehe dhambi zake, dhambi zake huyo hazitasamehewa.”

Yesu Amtokea Tomaso

24 Tomaso (aliyeitwa Pacha) alikuwa ni mmoja wa wale kumi na mbili, lakini hakuwapo pamoja na wafuasi wengine Yesu alipokuja. 25 Wakamwambia, “Tulimwona Bwana.” Tomaso akasema, “Hiyo ni ngumu kuamini. Ninahitaji kuona makovu ya misumari katika mikono yake, niweke vidole vyangu ubavuni. Ndipo tu nitakapoamini.” 26 Juma moja baadaye wafuasi walikuwemo katika nyumba ile tena, na Tomaso alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja na kusimama katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa. Iangalie mikono yangu. Weka mkono wako hapa ubavuni mwangu. Acha kuwa na mashaka na uamini.”

28 Tomaso akamwambia Yesu, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

29 Yesu akamwambia, “Unaamini kwa sababu umeniona. Wana baraka nyingi watu wale wanaoniamini bila kuniona!”

Kwa Nini Yohana Aliandika Kitabu hiki

30 Yesu alifanya ishara nyingine nyingi za miujiza ambazo wafuasi wake waliziona, na ambazo hazikuandikwa kwenye kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili muweze kuamini kwamba Yesu ni Masihi, Mwana wa Mungu. Kisha, kwa kuamini, mpate uzima kupitia jina lake.

Yesu Awatokea wafuasi Wake Saba

21 Baadaye, Yesu akawatokea tena wafuasi wake karibu na Ziwa Galilaya. Hivi ndivyo ilivyotokea: Baadhi ya wafuasi wake walikuwa pamoja; Simoni Petro, Tomaso (aliyeitwa Pacha), Nathanaeli kutoka Kana kule Galilaya, wana wawili wa Zebedayo, na wafuasi wengine wawili. Simoni Petro akasema, “Ninaenda kuvua samaki.”

Wafuasi wengine wakasema, “Sisi sote tutaenda pamoja nawe.” Hivyo wote wakatoka na kwenda kwenye mashua. Usiku ule walivua lakini hawakupata kitu.

Asubuhi na mapema siku iliyofuata Yesu akasimama ufukweni mwa bahari. Hata hivyo wafuasi wake hawakujua kuwa alikuwa ni yeye Yesu. Kisha akawauliza, “Rafiki zangu, mmepata samaki wo wote?”

Wao wakajibu, “Hapana.”

Yesu akasema, “Tupeni nyavu zenu kwenye maji upande wa kulia wa mashua yenu. Nanyi mtapata samaki huko.” Nao wakafanya hivyo. Wakapata samaki wengi kiasi cha kushindwa kuzivuta nyavu na kuziingiza katika mashua.

Mfuasi aliyependwa sana na Yesu akamwambia Petro, “Mtu huyo ni Bwana!” Petro aliposikia akisema kuwa alikuwa Bwana, akajifunga joho lake kiunoni. (Alikuwa amezivua nguo zake kwa vile alitaka kufanya kazi.) Ndipo akaruka majini. Wafuasi wengine wakaenda ufukweni katika mashua. Wakazivuta nyavu zilizojaa samaki. Nao hawakuwa mbali sana na ufukwe, walikuwa kadiri ya mita 100[b] tu. Walipotoka kwenye mashua na kuingia kwenye maji, wakaona moto wenye makaa yaliokolea sana. Ndani ya moto huo walikuwemo samaki na mikate pia. 10 Kisha Yesu akasema leteni baadhi ya samaki mliowavua.

11 Simoni Petro akaenda kwenye mashua na kuvuta wavu kuelekea ufukweni. Wavu huo ulikuwa umejaa samaki wakubwa, wapatao 153 kwa ujumla! Lakini pamoja na wingi wa samaki hao, nyavu hazikukatika. 12 Yesu akawaambia, “Njooni mle.” Hakuna hata mfuasi mmoja aliyemwuliza, “Wewe ni nani?” Walijua yeye alikuwa ni Bwana. 13 Yesu akatembea ili kuchukua mikate na kuwapa. Akawapa samaki pia.

14 Hii sasa ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.

Yesu Azungumza na Petro

15 Walipomaliza kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohana, je, unanipenda kuliko watu wote hawa wanavyonipenda?”

Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, unajua kuwa nakupenda.”

Kisha Yesu akamwambia, “Wachunge wanakondoo[c] wangu.”

16 Kwa mara nyingine Yesu akamwambia, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”

Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, wewe unajua kuwa nakupenda.”

Kisha Yesu akasema, “Watunze kondoo wangu.”

17 Mara ya tatu Yesu akasema, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”

Petro akahuzunika kwa sababu Yesu alimuuliza mara tatu, “Unanipenda?” Akasema, “Bwana, unafahamu kila kitu. Unajua kuwa nakupenda!”

Yesu akamwambia, “Walinde kondoo wangu. 18 Ukweli ni huu, wakati ulipokuwa mdogo, ulijifunga mwenyewe mkanda wako kiunoni na kwenda ulikotaka. Lakini utakapozeeka, utainyoosha mikono yako,[d] na mtu mwingine atakufunga mkanda wako. Watakuongoza kwenda mahali usikotaka kwenda.” 19 (Yesu alisema hivi kumwonyesha jinsi Petro atakavyokufa ili kumpa utukufu Mungu.) Kisha akamwambia Petro, “Nifuate!”

20 Petro akageuka na kumwona yule mfuasi mwingine aliyependwa sana na Yesu akitembea nyuma yao. (Huyu alikuwa ni mfuasi aliyejilaza kwa Yesu wakati wa chakula cha jioni na kusema, “Bwana, ni nani atakayekusaliti kwa maadui zako?”) 21 Petro alipomwona nyuma yao, akamwuliza Yesu, “Bwana, vipi kuhusu yeye?”

22 Yesu akajibu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali. Wewe nifuate!”

23 Kwa hiyo habari ikaenea miongoni mwa wafuasi wa Yesu. Wao walikuwa wakisema kuwa mfuasi huyo asingekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa asingekufa. Yeye alisema tu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali.”

24 Huyo mfuasi ndiye yeye anayesimulia habari hizi. Ndiye ambaye sasa ameziandika habari zote hizi. Nasi tunajua kuwa anayoyasema ni kweli.

25 Kuna mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu. Kama kila moja ya hayo yote yangeandikwa, nafikiri ulimwengu wote usingevitosha vitabu ambavyo vingeandikwa.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International