Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 27

Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato

(Mk 15:1; Lk 23:1-2; Yh 18:28-32)

27 Mapema asubuhi, viongozi wote wa makuhani na viongozi wazee walikutana na kuamua kumwua Yesu. Wakamfunga kamba, wakamwondoa na kwenda kumkabidhi kwa Pilato, gavana wa Kirumi.

Yuda Ajiua

(Mdo 1:18-19)

Baada ya kumkabidhi Yesu, Yuda aliona kila kitu kilichotokea na kujua kuwa wameamua kumwua Yesu. Naye alihuzunika sana kutokana na kile alichokifanya. Hivyo alirudisha vile vipande thelathini vya sarafu vya fedha kwa wakuu wa makuhani na viongozi wazee. Yuda aliwaambia, “Nimetenda dhambi. Nimemsaliti kwenu mtu asiye na hatia ili auawe.”

Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Hilo halituhusu. Ni tatizo lako, siyo letu sisi.”

Hivyo Yuda akavitupa vipande thelathini vya fedha Hekaluni, kisha akatoka akaenda kujinyonga.

Viongozi wa makuhani wakaviokota vile vipande vya fedha Hekaluni. Wakasema, “Sheria yetu haituruhusu kuweka fedha hii katika hazina ya Hekalu, kwa sababu fedha hii imelipwa kwa ajili ya kifo, ni fedha yenye damu.” Hivyo wakaamua kutumia fedha hiyo kwa kununulia shamba linaloitwa Shamba la Mfinyanzi kwa ajili ya kuwazikia wageni wanapokufa wakiwa ziarani katika mji wa Yerusalemu. Ndiyo sababu eneo hilo bado linaitwa Shamba la Damu. Hili lilitimiza maneno ya nabii Yeremia aliposema:

“Walichukua sarafu thelathini za fedha. Hicho ni kiasi ambacho Waisraeli waliamua kulipa kwa ajili ya uhai wake. 10 Walizitumia sarafu hizo thelathini za fedha kununulia shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniamuru.”[a]

Gavana Pilato Amhoji Yesu

(Mk 15:2-5; Lk 23:3-5; Yh 18:33-38)

11 Yesu alisimama mbele ya Gavana, Pilato, ambaye alimwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Waweza kusema hivyo.”

12 Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walipomshutumu, hakusema kitu.

13 Hivyo Pilato akamwambia, “Husikii mashtaka haya yote wanayokushtaki wewe? Kwa nini hujibu?”

14 Lakini Yesu hakujibu kitu, gavana alishangaa sana.

Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu

(Mk 15:6-15; Lk 23:13-25; Yh 18:39-19:16)

15 Kila mwaka wakati wa Pasaka, gavana angemwachia huru mfungwa mmoja yeyote ambaye watu wangetaka aachiwe huru. 16 Wakati huo alikuwepo mtu gerezani aliyejulikana kuwa ni mtu mbaya. Mtu huyu aliitwa Baraba.

17 Kundi la watu lilipokusanyika, Pilato aliwaambia, “Nitamwacha huru mtu mmoja. Mnataka nani nimwache huru: Baraba au Yesu aitwaye Masihi?” 18 Pilato alijua kuwa viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu walikuwa wanamwonea wivu.

19 Pilato alipokuwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akamtumia ujumbe uliosema, “Usifanye jambo lolote juu ya huyo mtu. Hana hatia. Nimeota ndoto juu yake usiku, na ndoto hiyo imenihangaisha sana.”

20 Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi waliwaambia watu waombe Baraba aachiwe huru na Yesu auawe.

21 Pilato akasema, “Nina Baraba na Yesu. Je, mnataka nimwache huru yupi?”

Watu wakajibu, “Baraba!”

22 Pilato akauliza, “Sasa nimfanye nini Yesu, aitwaye Masihi?”

Watu wote wakasema, “Mwue msalabani!”

23 Pilato akauliza, “Kwa nini mnataka nimwue Yesu? Amefanya kosa gani?”

Lakini walipaza sauti wakisema, “Mwue msalabani!”

24 Pilato akaona hakuna jambo ambalo angefanya ili kubadili nia yao. Kiukweli ilionekana wazi kuwa kungetokea fujo. Hivyo alichukua maji na kunawa mikono yake[b] mbele yao wote. Akasema, “Sina hatia na kifo cha mtu huyu. Ninyi ndio mnaofanya hili!”

25 Watu wakajibu, “Tutawajibika kwa kifo chake sisi wenyewe na hata watoto wetu!”

26 Kisha Pilato akamwachia huru Baraba. Na akawaambia baadhi ya askari wamchape Yesu viboko. Kisha akamkabidhi Yesu kwa askari ili akauawe msalabani.

Askari wa Pilato Wamdhihaki Yesu

(Mk 15:16-20; Yh 19:2-3)

27 Kisha askari wa Pilato wakamchukua Yesu mpaka kwenye nyumba ya gavana, kikosi kizima cha wale askari kikakusanyika pamoja kumzunguka Yesu. 28 Wakamvua nguo zake na kumvalisha kivazi chekundu.[c] 29 Kisha wakatengeneza taji kutokana na matawi ya miiba na kuiweka kwenye kichwa chake na wakaweka fimbo kwenye mkono wake wa kulia. Kisha kwa kumdhihaki, wakainama mbele zake. Wakasema, “Tunakusalimu, mfalme wa Wayahudi!” 30 Walimtemea mate. Kisha wakachukua fimbo yake na kuanza kumpiga nayo kichwani. 31 Baada ya kumaliza kumdhihaki, askari walimvua kivazi chekundu na kumvalisha nguo zake. Kisha wakamwongoza kwenda kuuawa msalabani.

Yesu Awambwa Msalabani

(Mk 15:21-32; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)

32 Askari walipokuwa wanatoka mjini wakiwa na Yesu, walimwona mtu mmoja kutoka Kirene aliyeitwa Simoni, na wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 33 Walifika mahali palipoitwa Golgotha. (Yaani “Eneo la Fuvu la Kichwa”.) 34 Askari walimpa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo.[d] Lakini alipoionja, alikataa kuinywa.

35 Askari walimgongomea Yesu msalabani, kisha wakacheza kamari ili wagawane nguo za Yesu. 36 Askari walikaa pale ili kumlinda. 37 Wakaweka alama juu ya kichwa chake kuonesha mashtaka dhidi yake yaliyosema: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.

38 Wahalifu wawili waligongomewa kwenye misalaba pamoja na Yesu, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto wa Yesu. 39 Watu waliokuwa wakipita pale walitikisa vichwa vyao na kumtukana Yesu matusi 40 kwa kusema, “Ulisema ungeweza kubomoa Hekalu na kulijenga tena katika siku tatu. Jiokoe mwenyewe! Teremka chini kutoka kwenye huo msalaba ikiwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu!”

41 Viongozi wa Makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwepo pale pia. Nao pia walimdhihaki Yesu kama watu wengine walivyofanya. 42 Walisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa yeye mwenyewe! Watu husema kuwa yeye ni mfalme wa Israeli. Ikiwa yeye ni mfalme, ashuke kutoka msalabani. Ndipo tutamwamini. 43 Alimtumaini Mungu. Hivyo Mungu amwokoe sasa, ikiwa hakika Mungu anamtaka. Yeye mwenyewe alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44 Hata wale wahalifu wawili waliokuwa misalabani upande wa kulia na wa kushoto wa Yesu walimtukana.

Yesu Afariki

(Mk 15:33-41; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)

45 Ilipofika adhuhuri, giza liliifunika Israeli yote kwa muda wa masaa matatu. 46 Yapata saa tisa alasiri Yesu alilia kwa sauti kuu akisema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha peke yangu?”(A)

47 Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hili wakasema, “Anamwita Eliya.”[e]

48 Mtu mmoja alikimbia haraka akaenda kuchukua sponji, akaijaza siki, akaifunga kwenye fimbo na akanyoosha fimbo ili kumpa Yesu sponji ili anywe siki. 49 Lakini wengine walisema, “Usimjali. Tunataka tuone ikiwa Eliya atakuja kumsaidia.”

50 Yesu akalia kwa sauti kuu tena, kisha akafa.[f]

51 Yesu alipokufa, pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili. Mpasuko wake ulianzia juu mpaka chini. Kulitokea pia tetemeko la ardhi na miamba ilipasuka. 52 Makaburi yalifunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa walifufuka kutoka kwa wafu. 53 Walitoka makaburini. Na baada ya Yesu kufufuliwa kutoka kwa wafu, walikwenda kwenye mji mtakatifu wa Yerusalemu, na watu wengi waliwaona.

54 Afisa wa jeshi na askari waliokuwa wanamlinda Yesu walitetemeka sana kwa kuogopa tetemeko la ardhi na kila walichokiona kikitokea. Wakasema, “Hakika alikuwa Mwana wa Mungu!”

55 Wanawake wengi waliomfuata Yesu kutoka Galilaya kumhudumia walikuwepo pale wakiangalia wakiwa wamesimama mbali na msalaba. 56 Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu na pia mama yao Yakobo na Yohana[g] alikuwepo pale.

Yesu Azikwa

(Mk 15:42-47; Lk 23:50-56; Yh 19:38-42)

57 Jioni ile, mtu mmoja tajiri aliyeitwa Yusufu alikuja Yerusalemu. Alikuwa mfuasi wa Yesu kutoka katika mji wa Arimathaya. 58 Alikwenda kwa Pilato na akamwomba mwili wa Yesu. Pilato akawaamuru askari wampe Yusufu wa Arimathaya mwili wa Yesu. 59 Aliuchukua mwili na kuuvingirisha katika kitambaa mororo cha kitani safi. 60 Yusufu akauzika mwili wa Yesu katika kaburi mpya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba mlimani. Kisha akalifunga kaburi kwa kuvingirisha jiwe kubwa kuziba mlango wa kaburi. Baada ya kufanya hivi, akaondoka. 61 Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu walikuwa wamekaa karibu na kaburi.

Kaburi la Yesu Lalindwa

62 Siku ile ilikuwa Siku ya Maandalizi. Siku iliyofuata, viongozi wa makuhani na Mafarisayo walimwendea Pilato. 63 Wakamwambia, “Mkuu, tunakumbuka kuwa yule mwongo alipokuwa hai alisema, ‘Nitafufuka kutoka kwa watu katika siku tatu.’ 64 Hivyo amuru ili kaburi lilindwe kwa siku tatu. Wafuasi wake wanaweza kuja na kujaribu kuiba mwili. Kisha wataweza kumwambia kila mtu kuwa alifufuka kutoka kwa wafu. Uongo huo utakuwa hatari zaidi ya hata waliyosema juu yake alipokuwa hai.”

65 Pilato akasema, “Chukueni baadhi ya askari, na mwende mkalinde kaburi kwa namna mnavyojua.” 66 Kisha walikwenda kaburini na kuliweka salama dhidi ya wezi. Walifanya hivi kwa kuliziba kwa jiwe langoni na kuwaweka askari wa kulinda kaburi.

Marko 15

Gavana Pilato Amhoji Yesu

(Mt 27:1-2,11-14; Lk 23:1-5; Yh 18:28-38)

15 Asubuhi na mapema, Mara tu ilipofika asubuhi viongozi wa makuhani, viongozi wazee wa Kiyahudi, walimu wa sheria, na baraza kuu lote la Wayahudi liliamua jambo la kufanya kwa Yesu. Walimfunga Yesu, wakamwondoa pale, na wakamkabidhi kwa Pilato.

Na Pilato akamwuliza: “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu “Hayo ni maneno yako mwenyewe.”

Na viongozi wa makuhani wakamshitaki Yesu kwa mambo mengi. Kwa hiyo Pilato akamwuliza Yesu swali lingine. Akasema, “Wewe hata kujibu hujibu? Angalia una mashitaka mengi wanayokuletea!”

Lakini Yesu hakujibu kitu chochote, na Pilato akastaajabu.

Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu

(Mt 27:15-31; Lk 23:13-25; Yh 18:39-19:16)

Kila mwaka wakati wa Sherehe ya Pasaka Pilato atamweka huru mfungwa mmoja atakayechaguliwa na watu. Mtu mmoja aliyeitwa Baraba alikuwa gerezani amefungwa pamoja na waasi. Watu hawa walifanya mauaji wakati wa fujo.

Watu walikuja Kwa Pilato na kumwomba amweke huru mfungwa kama alivyofanya siku zote. Yeye akawauliza, “Je, mnataka nimwache huru mfalme wa Wayahudi?” 10 Pilato alilisema hili kwa sababu alijua kuwa viongozi wa makuhani walimleta kwake kwa ajili ya wivu tu. 11 Lakini wale viongozi wa makuhani walimchochea amwache Baraba badala ya Yesu.

12 Lakini Pilato akawauliza watu tena, “Kwa hiyo nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”

13 Wakapiga kelele “Muue kwenye msalaba.”

14 Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini? Je, amefanya kosa gani?”

Lakini wote wakapiga kelele zaidi, “Muue kwenye msalaba!”

15 Pilato alitaka kuwaridhisha watu, kwa hiyo alimweka huru Baraba kwa ajili yao. Akaamuru maaskari wampige Yesu viboko na kisha akamtoa kwao ili akauawe kwenye msalaba.

16 Maaskari wakamwongoza Yesu hadi ndani ya baraza la jumba la gavana (lililojulikana kama Praitorio). Huko wakakiita pamoja kikosi cha maaskari. 17 Wakamvalisha Yesu joho la zambarau na wakafuma taji ya miiba na kumvisha kichwani. 18 Kisha wakaanza kumpigia saluti wakisema: “Heshima kwa Mfalme wa Wayahudi!” 19 Wakampiga tena na tena kichwani kwa fimbo na wakamtemea mate. Kisha wakapiga magoti mbele yake na kujifanya wanampa heshima kama mfalme. 20 Walipomaliza kumkejeli walimvua joho lile la kizambarau, na kumvisha mavazi yake mwenyewe. Baada ya hapo wakamtoa nje ili waweze kumsulubisha.

Yesu Awambwa Msalabani

(Mt 27:32-44; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)

21 Wakiwa njiani walikutana na mtu kutoka Kirenio aliyeitwa Simoni, akitoka vijijini kuja mjini. Yeye alikuwa baba yake Iskanda na Rufo. Wale wanajeshi wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 22 Wakamleta Yesu hadi mahali palipoitwa Golgotha (Yaani Mahali pa Fuvu la Kichwa) 23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na siki, lakini yeye alikataa kuinywa. 24 Pale wakampigilia kwa misumari msalabani. Wakagawana mavazi yake miongoni mwao nao wakayapigia kura ili kuona kila mtu atapata nini.

25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipompigilia kwa misumari msalabani. 26 Ilani ya mashtaka dhidi yake ilikuwa na maandishi haya juu yake: “Mfalme wa Wayahudi.” 27 Hapo waliwapigilia msalabani wahalifu wawili pembeni mwa Yesu, mmoja kushoto kwake na mwingine kuume kwake. 28 [a]

29 Watu waliopita mahali pale walimtukana. Walitikisa vichwa vyao na kusema, “Haya! Wewe ndiye yule awezaye kuliharibu hekalu na kulijenga tena kwa siku tatu. 30 Hebu shuka msalabani na uyaokoe maisha yako.”

31 Kwa njia hiyo hiyo, viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria walimfanyia dhihaka na wakasema wao kwa wao, “Aliwaokoa wengine lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32 Ikiwa yeye kweli ni Masihi Mfalme wa Israeli, iinampasa ashuke sasa toka msalabani, tukiliona hilo nasi tutamwamini.” Wale wahalifu waliokuwa katika misalaba ile mingine pembeni waliosulubiwa pamoja naye nao walimtukana.

Yesu Afariki

(Mt 27:45-56; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)

33 Ilipofika saa sita mchana giza ilifunika nchi yote. Giza liliendelea hadi saa tisa. 34 Mnamo saa tisa Yesu alipiga kelele kwa sauti na kusema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”(A)

35 Na baadhi ya wale waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hivi, walisema, “sikilizeni anamwita Eliya.”[b]

36 Mtu mmoja alikimbia na kujaza sifongo kwenye siki, akaliweka kwenye ufito, na akampa Yesu anywe akisema, “Subiri! Tuone ikiwa Eliya atashuka na kumshusha chini.”

37 Yesu akalia kwa sauti kubwa na kisha akafa.

38 Hapo pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili kutoka juu hadi chini. 39 Yule afisa wa jeshi aliyekuwa amesimama pale mbele na kuona jinsi Yesu alivyokufa. Afisa huyu alisema, “mtu huyu hakika alikuwa mwana wa Mungu!”

40 Baadhi ya wanawake walikuwa wakiangalia mambo haya toka mbali. Miongoni mwao alikuwapo Maria Magdalena, Salome, na Maria mama yake Yakobo na Yose. 41 Wanawake hawa ni wale waliomfuata Yesu huko Galilaya na kumhudumia. Wanawake wengi wengine waliofuatana naye kuja Yerusalemu walikuwapo pale pia.

Yesu Azikwa

(Mt 27:57-61; Lk 23:50-56; Yh 19:38-42)

42 Siku hii ilikuwa ni Siku ya Maandalizi ya Sabato. (Maana yake siku kabla ya Siku ya Sabato.) Jua lilikuwa bado halijazama. 43 Yusufu wa Arimathea alifika. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Kiyahudi aliyeheshimiwa, ambaye pia alikuwa anautazamia ufalme wa Mungu unaokuja. Kwa ujasiri mkubwa aliingia kwa Pilato na kuuomba mwili wa Yesu.

44 Pilato alishangaa Yesu angekuwa amekufa kwa haraka namna hii, hivyo alimwita yule akida na kumwuliza kama Yesu alikuwa tayari amekufa. 45 Aliposikia taarifa kutoka kwa yule afisa wa jeshi, ndipo alipoutoa mwili wa Yesu na kumpa Yusufu wa Arimathea.

46 Hivyo Yusufu alinunua mavazi kadhaa ya hariri, na akamshusha Yesu toka msalabani, akauzungushia mwili wake na hariri hiyo, na kumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika mwamba. Kisha alivingirisha jiwe kubwa na kuliweka mlangoni mwa kaburi. 47 Mariamu Magdalena na Maria mama yake Yose aliona pale alipolazwa Yesu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International