Chronological
Gavana Pilato Amhoji Yesu
(Mt 27:1-2,11-14; Mk 15:1-5; Yh 18:28-38)
23 Kisha kundi lote likasimama, wakampeleka Yesu kwa Pilato. 2 Wakaanza kumshitaki Yesu na kumwambia Pilato, “Tumemkamata mtu huyu akijaribu kuwapotosha watu wetu. Anasema tusilipe kodi kwa Kaisari. Anajiita Masihi, mfalme.”
3 Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu, “Ndiyo, unaweza kusema hivyo.”
4 Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na watu, “Sioni kosa lolote kwa mtu huyu.”
5 Lakini waliendelea kusema, “Mafundisho yake yanasababisha matatizo katika Uyahudi yote. Alianzia Galilaya na sasa yupo hapa!”
Pilato Ampeleka Yesu Kwa Herode
6 Pilato aliposikia hili, akauliza, “Mtu huyu anatoka Galilaya?” 7 Akatambua kuwa Yesu yuko chini ya mamlaka ya Herode. Siku hizo Herode alikuwa Yerusalemu, hivyo Pilato alimpeleka Yesu kwake.
8 Herode alipomwona Yesu alifurahi sana. Alikuwa akisikia habari zake na kwa muda mrefu alikuwa anataka kukutana na Yesu. Herode alitaka kuona muujiza, hivyo alitegemea kwamba Yesu angefanya muujiza mmoja. 9 Akamwuliza Yesu maswali mengi, lakini Yesu hakusema chochote. 10 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wamesimama pale wakipaza sauti zao wakimshitaki kwa Herode. 11 Ndipo Herode na askari wake wakamcheka. Wakamfanyia mzaha kwa kumvalisha mavazi kama ambayo wafalme huvaa. Kisha Herode akamrudisha Yesu kwa Pilato. 12 Nyakati za nyuma Pilato na Herode walikuwa maadui daima. Kuanzia siku ile wakawa marafiki.
Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu
(Mt 27:15-26; Mk 15:6-15; Yh 18:39-19:16)
13 Pilato aliwaita viongozi wa makuhani, viongozi wa Kiyahudi na watu wote pamoja. 14 Akawaambia, “Mlimleta mtu huyu kwangu. Mlisema alikuwa anawapotosha watu. Lakini nimemchunguza mbele yenu nyote na sijaona hatia juu ya kitu chochote mnachomshitakia. 15 Hata Herode hakumwona kuwa ana hatia yo yote. Akamrudisha kwetu. Tazameni, hajafanya jambo lolote baya linalostahili adhabu ya kifo. 16 Kwa hiyo, baada ya kumwadhibu kidogo nitamwacha aende zake.” 17 [a]
18 Lakini wote walipaza sauti zao pamoja, “Mwue! Mwachie huru Baraba!” 19 (Baraba alifungwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo mjini na kwa mauaji.)
20 Pilato alitaka amwachie huru Yesu. Hivyo Pilato akawaambia atamwachilia. 21 Lakini walipaza sauti tena wakisema, “Mwue, Mwue msalabani!”
22 Mara ya tatu Pilato akawaambia watu, “Kwa nini? Amefanya kosa gani? Hana hatia. Sioni sababu ya kumwua. Hivyo nitamwachia huru baada ya kumwadhibu kidogo.”
23 Lakini watu waliendelea kupaza sauti. Walidai Yesu auawe msalabani. Kelele zao zikawa kubwa kiasi kwamba 24 Pilato aliamua kuwapa kile walichotaka. 25 Walitaka Baraba aliyekuwa gerezani kwa sababu ya kuanzisha fujo na mauaji aachiwe huru. Pilato akamwachia Baraba. Na kumtoa Yesu ili auawe. Hili ndilo watu walitaka.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mt 27:32-44; Mk 15:21-32; Yh 19:17-27)
26 Askari wakamwongoza Yesu kumtoa nje ya mji. Wakati huo huo mtu mmoja kutoka Kirene alikuwa anaingia mjini kutoka maeneo nje ya Yerusalemu. Askari wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu na kumfuata Yesu kwa nyuma.
27 Kundi kubwa wakamfuata Yesu. Baadhi ya wanawake waliokuwemo kwenye kundi walilia na kuomboleza. Walimwonea huruma. 28 Lakini Yesu aligeuka na kuwaambia, “Wanawake wa Yerusalemu, msinililie. Jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29 Wakati unakuja ambapo watu watasema, ‘Wanawake wasioweza kuwa na watoto ndio ambao Mungu amewabariki. Hakika ni baraka kwamba hawana watoto wa kutunza.’ 30 Watu wataiambia milima, ‘Tuangukieni!’ Wataviambia vilima, ‘Tufunikeni!’(A) 31 Kama hili linaweza kutokea kwa mtu aliye mwema, nini kitatokea kwa wenye hatia?”
32 Walikuwepo pia wahalifu wawili waliotolewa nje ya mji pamoja na Yesu ili wauawe. 33 Walipelekwa mahali palipoitwa “Fuvu la Kichwa.” Askari walimpigilia Yesu msalabani pale. Waliwapigilia misalabani wahalifu pia, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine kushoto kwa Yesu.
34 Na Yesu alikuwa anasema, “Baba uwasamehe watu hawa, kwa sababu hawajui wanalofanya.”
Askari waligawana nguo zake kwa kutumia kamari. 35 Watu walisimama pale wakiangalia kila kitu kilichokuwa kinatokea. Viongozi wa Kiyahudi walimcheka Yesu. Walisema, “Kama kweli yeye ni Masihi, Mfalme Mteule wa Mungu, basi ajiokoe. Je, hakuwaokoa wengine?”
36 Hata askari walimcheka Yesu na kumfanyia mizaha. Walikuja na kumpa siki ya mvinyo. 37 Wakasema, “Ikiwa wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe!” 38 Waliandika maneno haya kwenye kibao msalabani juu ya kichwa chake: “Huyu ni Mfalme wa Wayahudi”.
39 Mmoja wa wahalifu aliyekuwa ananing'inia pale akaanza kumtukana Yesu: “Wewe siye Masihi? Basi jiokoe na utuokoe sisi pia!”
40 Lakini mhalifu mwingine alimnyamazisha asiendelee kumtukana Yesu. Akasema, “Unapaswa kumwogopa Mungu. Sisi sote tutakufa muda si mrefu. 41 Wewe na mimi tuna hatia, tunastahili kufa kwa sababu tulitenda mabaya. Lakini mtu huyu hajafanya chochote kibaya.” 42 Kisha akamwambia Yesu, “Unikumbuke utakapoanza kutawala kama mfalme!”
43 Yesu akamwambia, “Ninakwambia kwa uhakika, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Yesu Afariki
(Mt 27:45-56; Mk 15:33-41; Yh 19:28-30)
44 Ilikuwa yapata saa sita mchana, lakini kulibadilika kukawa giza mpaka saa tisa alasiri, 45 kwa sababu jua liliacha kung'aa. Pazia ndani ya Hekalu lilichanika vipande viwili. 46 Yesu alipaza sauti akasema, “Baba, ninaiweka roho yangu mikononi mwako!”(B) Baada ya Yesu kusema haya, akafa.
47 Mkuu wa askari wa Kirumi aliyekuwa pale alipoona yaliyotokea, alimsifu Mungu, akisema, “Ninajua mtu huyu alikuwa mtu mwema!”
48 Watu wengi walikuwa wametoka mjini kuja kuona tukio hili. Walipoona, wakahuzunika, wakaondoka wakiwa wanapiga vifua vyao. 49 Watu waliokuwa marafiki wa karibu wa Yesu walikuwepo pale. Pia, walikuwepo baadhi ya wanawake waliomfuata Yesu kutoka Galilaya. Walisimama mbali kutoka msalabani, waliyaona mambo haya.
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Yh 19:38-42)
50-51 Mtu mmoja aliyeitwa Yusufu kutoka mji wa Uyahudi ulioitwa Arimathaya alikuwapo pale. Alikuwa mtu mwema, aliyeishi namna Mungu alivyotaka. Alikuwa anausubiri ufalme wa Mungu uje. Yusufu alikuwa mjumbe wa baraza la Kiyahudi. Lakini hakukubali pale viongozi wengine wa Kiyahudi walipoamua kumwua Yesu. 52 Alikwenda kwa Pilato na kumwomba mwili wa Yesu. 53 Aliushusha mwili kutoka msalabani na kuufunga kwenye nguo. Kisha akauweka ndani ya kaburi lililochimbwa katika ukuta wa mwamba. Kaburi hili lilikuwa halijatumika bado. 54 Ilikuwa jioni Siku ya Maandalizi ya Sabato. Sabato ilikuwa ianze baada ya jua kuzama.
55 Wanawake waliotoka Galilaya pamoja na Yesu walimfuata Yusufu. Wakaliona kaburi. Ndani yake wakaona mahali alipouweka mwili wa Yesu. 56 Kisha wakaenda kuandaa manukato yanayonukia vizuri ili kuupaka mwili wa Yesu.
Siku ya Sabato walipumzika, kama ilivyoamriwa katika Sheria ya Musa.
Yesu Akamatwa
(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Lk 22:47-53)
18 Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka pamoja na wafuasi wake kwenda ng'ambo kuvuka bonde la Kidroni. Akaenda katika bustani mahali hapo, akiwa bado pamoja na wafuasi wake.
2 Yuda, yule aliyehusika kumsaliti Yesu, alipafahamu mahali pale. Alipajua kwa sababu Yesu mara nyingi alikutana na wafuasi wake pale. 3 Kwa hiyo Yuda akaongoza kundi la askari hadi katika bustani hiyo pamoja na walinzi wengine kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Hawa walikuwa wamebeba mienge, taa, na silaha.
4 Yesu alikwisha kujua yote ambayo yangempata. Hivyo aliwaendea na kuwauliza, “Je, ni nani mnayemtafuta?”
5 Wakamjibu, “Yesu kutoka Nazareti.”
Akawaambia, “Mimi ni Yesu.”[a] (Yuda yule aliyehusika kumsaliti Yesu alikuwa amesimama hapo pamoja nao.) 6 Yesu aliposema, “Mimi ni Yesu,” wale watu walirudi nyuma na kuanguka chini.
7 Akawauliza tena, “Je, ni nani mnayemtafuta?”
Wakasema, “Yesu kutoka Nazareti.”
8 Yesu akasema, “Nimewaambia kwamba mimi ndiye Yesu. Hivyo kama mnanitafuta mimi, basi waacheni huru watu hawa waende zao.” 9 Hii ilikuwa kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu mapema: “Sikumpoteza hata mmoja wa wale ulionipa.”
10 Simoni Petro akauchomoa upanga aliokuwa ameufunga kiunoni. Akampiga nao mtumishi wa Kuhani Mkuu, na kulikata sikio lake la kulia. (Jina la mtumishi huyo lilikuwa ni Maliko.) 11 Yesu akamwambia Petro, “Rudisha jambia lako mahali pake! Ninapaswa kunywa toka kikombe[b] ambacho Baba amenipa nikinywee.”
Yesu Aletwa Mbele ya Anasi
(Mt 26:57-58; Mk 14:53-54; Lk 22:54)
12 Kisha askari hao pamoja na mkuu wao na walinzi wa Kiyahudi wakamkamata Yesu. Wakamfunga, 13 nao wakampeleka kwanza kwa Anasi, baba mkwe wa Kayafa. Kayafa alikuwa Kuhani Mkuu kwa mwaka huo. 14 Naye ndiye aliyewashauri viongozi wengine wa Kiyahudi kwamba ingemfaa mtu mmoja afe[c] kwa ajili ya watu wote.
Petro Amkana Yesu
(Mt 26:69-70; Mk 14:66-68; Lk 22:55-57)
15 Simoni Petro na mmoja wa wafuasi wengine wa Yesu walienda pamoja na Yesu. Mfuasi huyu alimfahamu kuhani mkuu. Hivyo akaingia pamoja na Yesu ndani ya uwanja wa nyumba ya kuhani mkuu. 16 Lakini Petro alisubiri nje karibu na mlango. Yule mfuasi aliyemjua kuhani mkuu alirudi nje na kuongea na mlinda mlango. Kisha alimleta Petro ndani. 17 Msichana aliyekuwepo langoni alimwambia Petro, “Je! Wewe pia ni mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro akajibu, “Hapana, mimi siye!”
18 Ilikuwa baridi, hivyo watumishi na walinzi waliwasha moto wa kuni. Walikuwa wameuzunguka, wakipasha joto miili yao naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao.
Kuhani Mkuu Amhoji Yesu
(Mt 26:59-66; Mk 14:55-64; Lk 22:66-71)
19 Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu maswali kuhusu wafuasi wake pamoja na mafundisho aliyowapa. 20 Yesu akamjibu, “Daima nimesema wazi kwa watu wote. Siku zote nimefundisha kwenye masinagogi na kwenye eneo la Hekalu. Wayahudi wote hukusanyika pale. Sijawahi kusema jambo lo lote kwa siri. 21 Sasa kwa nini unaniuliza? Waulize watu waliosikia mafundisho yangu. Wao wanajua niliyosema!”
22 Yesu aliposema hivyo, mmoja wa walinzi aliyekuwa amesimama hapo akampiga. Mlinzi huyo akasema, “Hupaswi kusema hivyo kwa kuhani mkuu!”
23 Yesu akajibu, “Kama nimesema vibaya jambo lo lote, mwambie kila mtu hapa kosa lenyewe. Lakini kama niliyosema ni sahihi, kwa nini basi unanipiga?”
24 Hivyo Anasi akampeleka Yesu kwa Kayafa kuhani mkuu. Naye alikuwa bado amefungwa.
Petro Amkana Yesu tena
(Mt 26:71-75; Mk 14:69-72; Lk 22:58-62)
25 Simoni Petro alikuwa amesimama karibu na moto, akijipasha joto. Watu wengine wakamwambia Petro, “Je, wewe si mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”
Petro alikataa hilo. Akasema, “Hapana, mimi siye.”
26 Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu alikuwapo pale. Naye alikuwa ni jamaa wa mtu yule aliyekatwa sikio na Petro. Mtumishi akamwambia Petro, “Nadhani nilikuona pamoja naye pale kwenye bustani!”
27 Lakini kwa mara nyingine Petro akasema, “Hapana, sikuwa pamoja naye!” Mara tu alipomaliza kusema hayo, jogoo akawika.
Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato
(Mt 27:1-2,11-31; Mk 15:1-20; Lk 23:1-25)
28 Kisha walinzi wakamchukua Yesu kutoka katika nyumba ya Kayafa kwenda kwenye jumba la mtawala wa Kirumi. Nayo ilikuwa ni mapema asubuhi. Wayahudi waliokuwa pale wasingeweza kuingia ndani ya jumba hilo. Wao hawakutaka kujinajisi wenyewe kwa sababu walitaka kuila karamu ya Pasaka. 29 Kwa hiyo Pilato akatoka nje kuwafuata na akawauliza, “Mnasema mtu huyu amefanya makosa gani?”
30 Wakajibu, “Yeye ni mtu mbaya. Ndiyo maana tumemleta kwako.”
31 Pilato akawaambia, “Mchukueni wenyewe na kumhukumu kufuatana na sheria yenu.” Viongozi wa Wayahudi wakamwambia, “Lakini sheria yako haituruhusu sisi kumwadhibu mtu yeyote kwa kumwua.” 32 (Hii ilikuwa ni kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu juu ya jinsi ambavyo angekufa.)
33 Kisha Pilato alirudi ndani ya jumba lile. Aliagiza Yesu aje na akamuuliza, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”
34 Yesu akajibu, “Je, hilo ni swali lako mwenyewe au watu wengine wamekuambia juu yangu?”
35 Pilato akajibu, “Mimi sio Myahudi! Ni watu wako mwenyewe na viongozi wa makuhani waliokuleta kwangu. Je, umefanya kosa gani?”
36 Yesu akajibu, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ungekuwa hivyo, watumishi wangu wangenipigania ili nisikabidhiwe kwa viongozi wa Wayahudi. Hapana, ufalme wangu sio wa kidunia.”
37 Pilato akasema, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?”
Yesu akamjibu, “Uko sahihi unaposema kuwa mimi ni mfalme. Nami nilizaliwa kwa ajili ya hili: kuwaeleza watu juu ya kweli. Ni kwa sababu hii nalikuja ulimwenguni. Kila mmoja aliye wa upande wa kweli hunisikiliza.”
38 Pilato akasema, “Kweli ndiyo nini?” Kisha alitoka nje tena kwenda kwa viongozi wa Wayahudi na kuwaimbia, “Mimi sipati kitu chochote kibaya cha kumpinga mtu huyu. 39 Lakini ni moja ya desturi zenu kwangu mimi kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”
40 Wakajibu kwa kupiga kelele wakisema, “Hapana, siyo yeye! Mwache huru Baraba!” (Baraba alikuwa jambazi.)
19 Kisha Pilato akaamuru Yesu aondolewe akachapwe viboko. 2 Askari wakatengeneza taji kutokana na matawi yenye miiba na kuiweka kichwani kwake. Kisha wakamzungushia vazi la rangi ya zambarau mwilini mwake. 3 Wakaendelea kumkaribia wakisema, “Salamu kwako mfalme wa Wayahudi!” Kisha wakampiga Yesu usoni.
4 Kwa mara nyingine Pilato alienda nje na kuwaambia viongozi wa Wayahudi, “Tazameni! Ninamtoa nje Yesu na kumleta kwenu. Ninataka mfahamu kuwa sijapata kwake jambo lolote ambalo kwa hilo naweza kumshitaki.” 5 Kisha Yesu akatoka nje akiwa amevishwa taji ya miiba na vazi la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu ndiye mtu mwenyewe!”
6 Viongozi wa makuhani na walinzi wa Kiyahudi walipomwona Yesu wakapiga kelele, “Mpigilieni misumari msalabani! Mpigilieni misumari msalabani!”
Lakini Pilato akajibu, “Mchukueni na mpigilieni msalabani ninyi wenyewe. Mimi sioni kosa lolote la kumshitaki.”
7 Viongozi wa Wayahudi wakasema, “Tunayo sheria inayosema kuwa ni lazima afe, kwa sababu alisema kuwa yeye ni Mwana wa Mungu.”
8 Pilato aliposikia haya, aliogopa zaidi. 9 Hivyo akarudi ndani ya jumba lake na kumwuliza Yesu, “Wewe unatoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu kitu. 10 Pilato akasema, “Unakataa kusema nami? Kumbuka, ninao uwezo wa kukuweka huru au kukuua msalabani.”
11 Yesu akajibu, “Uwezo pekee ulio nao juu yangu ni ule uwezo uliopewa na Mungu. Kwa hiyo yule aliyenitoa mimi kwenu anayo hatia ya dhambi kubwa zaidi.”
12 Baada ya hayo, Pilato alijaribu kumwacha huru Yesu. Lakini viongozi wa Wayahudi wakapiga kelele, “Yeyote anayejiweka mwenyewe kuwa mfalme yuko kinyume cha Kaisari. Hivyo kama utamwacha huru mtu huyu, hiyo itakuwa na maana kuwa wewe si rafiki wa Kaisari.”
13 Pilato aliposikia maneno hayo, akamtoa nje Yesu na kumweka mahali palipoitwa “Sakafu ya Mawe.” (Kwa Kiaramu jina lake ni Gabatha.) Pale Pilato akaketi katika kiti cha hakimu. 14 Wakati huu, ilikuwa imekaribia kuwa saa sita adhuhuri katika Siku ya Matayarisho ya juma la Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”
15 Wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Mwue msalabani!”
Pilato akawauliza, “Mnanitaka nimwue mfalme wenu msalabani?”
Viongozi wa makuhani wakajibu, “Kaisari ndiye Mfalme pekee tuliye naye!”
16 Hivyo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili auawe juu ya msalaba. Askari wakamchukua Yesu.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mt 27:32-44; Mk 15:21-32; Lk 23:26-43)
17 Naye Yesu akaubeba msalaba wake hadi mahali panapoitwa “Fuvu la Kichwa”. (Kwa Kiaramu mahali hapo paliitwa “Golgotha”.) 18 Hapo wakampigilia Yesu kwa misumari katika msalaba. Pia wakawapigilia kwa misumari watu wengine wawili kwenye misalaba miwili tofauti. Kila mmoja akawekwa pembeni upande wa kushoto na kuume wa msalaba wa Yesu naye akawa katikati yao.
19 Pilato akawaambia waandike kibao na kisha kukiweka juu ya msalaba. Kibao hicho kiliandikwa na kilisema, “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi.” 20 Kibao hicho kiliandikwa kwa Kiaramu, Kirumi na Kiyunani. Wayahudi walio wengi walikisoma kibao hicho, kwa sababu mahali ambapo Yesu alipigiliwa kwa misumari msalabani palikuwa karibu na mji.
21 Viongozi wa makuhani wa Kiyahudi wakamwambia Pilato, “Usiandike, ‘Mfalme wa Wayahudi.’ Bali andika, ‘Mtu huyu alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’”
22 Pilato akawajibu, “Sitayabadili yale niliyokwisha kuyaandika.”
23 Hivyo baada ya askari kumpigilia Yesu kwa misumari msalabani, walizichukua nguo zake na kuzigawa katika mafungu manne. Kila askari alipata fungu moja. Pia wakalichukua vazi lake lililokuwa limefumwa kwa kipande kimoja tu cha kitambaa kutoka juu hadi chini. 24 Hivyo askari wakasemezana wao kwa wao, “Hatutalichana vazi hili vipande vipande. Hebu tulipigie kura kuona nani atakayelipata.” Hili lilitokea ili kuweka wazi maana kamili ya yale yanayosemwa katika Maandiko:
“Waligawana miongoni mwao mavazi yangu,
na wakakipigia kura kile nilichokuwa nimevaa.”(A)
Hivyo ndivyo maaskari walivyofanya.
25 Mama yake Yesu alisimama karibu na msalaba wa mwanawe, Dada yake mamaye Yesu pia alikuwa amesimama pale pamoja na Mariamu mke wake Kleopa, na Mariamu Magdalena. 26 Yesu akamwona mama yake na akamwona pia mfuasi aliyempenda sana akisimama pale. Akamwambia mama yake, “Mama mpendwa, mwangalie huyo, naye ni mwanao sasa.” 27 Kisha akamwambia yule mfuasi, “Huyu hapa ni mama yako sasa.” Kisha baada ya hayo, mfuasi huyo akamchukua mama yake Yesu na kuishi naye nyumbani kwake.
Yesu Afariki
(Mt 27:45-56; Mk 15:33-41; Lk 23:44-49)
28 Baadaye, Yesu akajua kuwa kila kitu kimekwisha kamilika. Ili kuyafanya Maandiko yatimie akasema, “Nina kiu.”[d] 29 Palikuwapo na bakuli lililojaa siki[e] mahali pale, wale askari wakachovya sponji ndani yake. Wakaiweka ile sponji kwenye tawi la mwanzi na kuliinua hadi kinywani kwa Yesu. 30 Alipoionja ile siki, akasema, “Imekwisha.” Baada ya hapo akainamisha kichwa chake na kufa.
31 Hii ilikuwa Ijumaa, Siku ya Matayarisho. Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya Sabato maalumu. Viongozi wa Kiyahudi hawakuitaka ile miili ya waliosulubiwa ikae juu misalabani katika siku ya Sabato. Hivyo wakamwomba Pilato atoe amri kuwa miguu ya wale watu misalabani ivunjwe. Pia wakaomba ile miili ishushwe kutoka kwenye misalaba. 32 Kwa hiyo askari wakaja na kuivunja miguu[f] ya watu wale wawili kwenye misalaba kando ya Yesu. 33 Lakini askari walipomkaribia Yesu, wakaona kuwa tayari alikuwa amekwisha kufa. Hivyo hawakuivunja miguu yake.
34 Lakini mmoja wa askari akauchoma ubavu wa Yesu kwa mkuki wake. Mara hiyo hiyo damu na maji vikamtoka mwilini mwake. 35 (Yeye aliyeona haya yakitokea ametueleza. Aliyaeleza haya ili ninyi pia muweze kuamini. Mambo anayosema ni ya kweli. Yeye anajua kuwa anasema kweli.) 36 Mambo haya yalitokea ili kutimiza Maandiko yaliyosema, “Hakuna mfupa wake utakaovunjwa”[g] 37 na “Watu watamwangalia yeye waliyemchoma.”(B)
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Lk 23:50-56)
38 Baadaye, mtu mmoja aliyeitwa Yusufu wa kutoka Arimathaya akamwomba Pilato mwili wa Yesu. (Yusufu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini hakumweleza mtu yeyote, kwa sababu aliwaogopa viongozi wa Kiyahudi.) Pilato akasema Yusufu anaweza kuuchukua mwili wa Yesu, hivyo naye akaja na kuuchukua.
39 Nikodemu akaenda pamoja na Yusufu. Nikodemu, alikuwa ni yule mtu aliyekuja kwa Yesu hapo kabla na kuzungumza naye usiku. Huyu alileta kadiri ya lita[h] mia moja ya marashi yenye mchanganyiko wa manemane na uvumba. 40 Watu hawa wawili wakauchukua mwili wa Yesu na wakauzungushia vipande vya sanda ya kitani pamoja na marashi yale. (Hivi ndivyo Wayahudi walivyowazika watu.) 41 Pale msalabani sehemu alipouawa Yesu, palikuwepo na bustani. Katika bustani ile palikuwemo na kaburi[i] jipya la kuzikia. Hakuna mtu aliyewahi kuzikwa ndani ya kaburi lile. 42 Wanaume wakauweka mwili wa Yesu katika kaburi lile kwa kuwa lilikuwa karibu, na Wayahudi walikuwa wakijiandaa kuianza siku yao ya Sabato.
© 2017 Bible League International