Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 23

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mk 12:38-40; Lk 11:37-52; 20:45-47)

23 Kisha Yesu akazungumza na watu pamoja na wafuasi wake, akasema, “Walimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kuwaambia Sheria ya Musa inasema nini. Hivyo mnapaswa kuwatii. Fanyeni kila wanachowaambia. Lakini maisha yao sio mfano mzuri wa kuufuata. Hawatendi wale wanayofundisha. Hutengeneza orodha ndefu ya kanuni na kujaribu kuwalazimisha watu kuzifuata. Lakini sheria hizi ni kama mizigo mizito ambayo watu hawawezi kuibeba, na viongozi hawa hawatazirahisisha kupunguza mzigo kwa watu.

Wao wanatenda mambo mema tu ili waonwe na watu wengine. Hufanya visanduku vidogo vya Maandiko[a] wanavyovaa kuwa vikubwa zaidi. Hufanya mashada ya urembo[b] kwenye mavazi yao ya nje kuwa marefu zaidi ili waonwe na watu. Watu hawa wanapenda kukaa sehemu za heshima kwenye sherehe na kwenye viti muhimu zaidi katika masinagogi. Wanapenda kuitwa ‘Mwalimu’ Na kusalimiwa kwa heshima na watu kwenye masoko.

Ninyi nyote ni ndugu, dada na kaka kwa sababu mnaye mwalimu mmoja tu. Hivyo msikubali kuitwa ‘Mwalimu’. Nanyi msimwite mtu yeyote duniani ‘Baba’, maana mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni. 10 Msikubali kuitwa ‘Mwalimu’, kwa sababu mnaye Mwalimu mmoja tu, naye ni Masihi. 11 Kila atakayetumika kama mtumishi ndiyo mkuu zaidi kati yenu. 12 Wanaojifanya kuwa bora kuliko wengine watanyenyekezwa kwa lazima. Lakini watu wanaojinyenyekeza wenyewe watafanywa kuwa wakuu.

13 Ole wenu[c] walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnawafungia watu njia ya kuingia katika ufalme wa Mungu, kwa kuwa ninyi wenyewe hamwingii na mnawazuia wale wanaojaribu kuingia. 14 [d]

15 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki. Mnasafiri kuvuka bahari na nchi nyingine ili kumtafuta mtu mmoja atakayefuata njia zenu. Mnapompata mtu huyo, mnamfanya astahili maradufu kwenda Jehanamu kama ninyi mlivyo!

16 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona. Mnasema, ‘Mtu yeyote akiweka kiapo au nadhiri kwa jina la Hekalu, haimaanishi kitu. Lakini yeyote atakayeweka kiapo kwa kutumia dhahabu iliyo Hekaluni lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 17 Ninyi ni wasiyeona mlio wajinga! Hamwoni kuwa Hekalu ni kuu kuliko dhahabu iliyo ndani yake? Hekalu ndilo huifanya dhahabu kuwa takatifu!

18 Na mnasema, ‘Mtu yeyote akitumia madhabahu kuweka nadhiri au kiapo, haina maana yeyote. Lakini kila anayetumia sadaka iliyo kwenye madhabahu na kuapa au kuweka nadhiri, lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 19 Ninyi ni wasiyeona! Hamwoni kuwa madhabahu ni kuu kuliko sadaka yo yote iliyo juu yake? Madhabahu ndiyo inaifanya sadaka kuwa takatifu! 20 Kila anayeitumia madhabahu kuapa au kuweka nadhiri ni dhahiri anatumia madhabahu na kila kitu kilicho juu yake. 21 Na kila anayetumia Hekalu kuapa au kuweka nadhiri kwa hakika analitumia Hekalu na Mungu, anayeishi ndani humo. 22 Kila anayetumia mbingu kuapa au kuweka nadhiri anakitumia kiti cha enzi cha Mungu na yule aketiye juu yake.

23 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata,[e] hata mnanaa, binzari na jira.[f] Lakini hamtii mambo ya muhimu katika mafundisho ya sheria; kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya. Na mwendelee pia kufanya mambo hayo mengine. 24 Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona![g] Ninyi ni kama mtu anayemtoa nzi katika kinywa chake na kisha anammeza ngamia!

25 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnaosha vikombe na sahani zenu kwa nje. Lakini ndani yake vimejaa vitu mlivyopata kwa kuwadang'anya wengine na kujifurahisha ninyi wenyewe. 26 Mafarisayo, ninyi ni wasiyeona! Safisheni kwanza vikombe kwa ndani ili viwe safi. Ndipo vikombe hivyo vitakuwa safi hata kwa nje.

27 Ole wenu walimu wa sheria na ninyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Ninyi ni kama makaburi yaliyopakwa rangi nyeupe, lakini ndani yake yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28 Ndivyo ilivyo hata kwenu. Watu wanawatazama na kudhani kuwa ninyi ni wenye haki, lakini mmejaa unafiki na uovu ndani yenu.

29 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii, na kuyaheshimu makaburi ya wenye haki waliouawa. 30 Na mnasema, ‘Ikiwa tungeishi nyakati za mababu zetu, tusingewasaidia kuwaua manabii hawa.’ 31 Hivyo mnathibitisha kuwa ninyi ni uzao wa wale waliowaua manabii. 32 Na mtaimalizia dhambi waliyoianza mababu zenu!

33 Enyi nyoka! Ninyi mlio wa uzao wa nyoka wenye sumu kali! Hamtaikwepa adhabu. Mtahukumiwa na kutupwa Jehanamu! 34 Hivyo ninawaambia: Ninawatuma manabii na walimu wenye hekima na wanaojua Maandiko. Lakini mtawaua, mtawatundika baadhi yao kwenye misalaba na kuwapiga wengine katika masinagogi yenu. Mtawafukuza kutoka katika mji mmoja hadi mwingine.

35 Hivyo mtakuwa na hatia kutokana vifo vyote vya watu wema wote waliouawa duniani. Mtakuwa na hatia kwa kumwua mtu wa haki Habili, na mtakuwa na hatia kwa kuuawa kwa Zakaria[h] mwana wa Barakia mliyemwua kati ya Hekalu na madhabahu. Mtakuwa na hatia ya kuwaua watu wote wema walioishi kati ya wakati wa Habili mpaka wakati wa Zakaria. 36 Niaminini ninapowaambia kuwa mambo haya yote yatawapata ninyi watu mnaoishi sasa.

Yesu Awaonya Watu wa Yerusalemu

(Lk 13:34-35)

37 Ee Yerusalemu, Yerusalemu! Unayewaua manabii. Unawapiga kwa mawe wale ambao Mungu amewatuma kwako. Mara nyingi nimetaka kuwasaidia watu wako. Nimetaka kuwakusanya watu wako kama kuku anavyowakusanya vifaranga wake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu kufanya hivyo. 38 Sasa Hekalu lako litaachwa ukiwa kabisa. 39 Ninakwambia, hautaniona tena mpaka wakati utakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(A)

Luka 20-21

Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu

(Mt 21:23-27; Mk 11:27-33)

20 Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu katika eneo la Hekalu. Alikuwa anawahubiri Habari njema. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikwenda kuzungumza na Yesu. Wakamwambia, “Tuambie, una mamlaka gani kutenda mambo haya! Ni nani aliyekupa mamlaka hii?”

Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali pia. Niambieni: Yohana alipobatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa watu fulani?”

Makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kwa pamoja kuhusu hili. Wakasema, “Kama tukijibu ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ Lakini kama tukisema ulitoka kwa watu fulani, watu hawa watatupiga kwa mawe mpaka tufe. Kwa sababu wote wanaamini Yohana alikuwa nabii.” Hivyo wakajibu, “Hatujui.”

Ndipo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni nani alinipa mamlaka kufanya mambo haya.”

Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu

(Mt 21:33-46; Mk 12:1-12)

Yesu akawaambia watu kisa hiki; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Kisha akalikodisha kwa wakulima, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwa wakulima wale ili wampe sehemu yake ya zabibu. Lakini wakulima wale walimpiga yule mtumishi na wakamfukuza bila kumpa kitu. 11 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi mwingine. Wakulima walimpiga mtumishi huyu pia, wakamwaibisha na kumfukuza bila kumpa kitu. 12 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi wa tatu. Wakulima wakampiga sana mtumishi huyu na wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.

13 Mmiliki wa shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa. Yumkini watamheshimu.’ 14 Lakini wakulima walipomwona mwana wa mwenye shamba, wakajadiliana wakisema, ‘Huyu ni mwana wa mmiliki wa shamba. Shamba hili la mizabibu litakuwa lake. Tukimwua, litakuwa letu.’ 15 Hivyo wakulima wakamtupa mwana wa mmiliki wa shamba nje ya shamba la mizabibu na wakamwua.

Je, mmiliki wa shamba la mizabibu atafanya nini? 16 Atakuja na atawaua wale wakulima, kisha atalikodisha shamba kwa wakulima wengine.”

Watu waliposikia mfano huu, wakasema, “Hili lisije kutokea!” 17 Lakini Yesu akawakazia macho na akasema, “Hivyo basi, Maandiko haya yanamaanisha nini:

‘Jiwe lililokataliwa na wajenzi,
    limekuwa jiwe kuu la pembeni?’[a]

18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika na ikiwa jiwe hilo litaangukia, litakusaga!”

19 Walimu wa sheria na wakuu wa makuhani waliposikia kisa hiki, walijua unawahusu wao. Hivyo walitaka kumkamata Yesu wakati huo huo, lakini waliogopa watu wangewadhuru.

Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego

(Mt 22:15-22; Mk 12:13-17)

20 Hivyo viongozi wa Kiyahudi walitafuta namna ya kumtega Yesu. Walituma watu waliojifanya kuwa wenye haki, ili waweze kumnasa ikiwa angesema jambo ambalo wangeweza kutumia kinyume naye. Ikiwa angesema jambo lolote baya, wangemkamata na kumpeleka kwa gavana wa Kirumi, mwenye mamlaka ya kumhukumu na kumwadhibu. 21 Hivyo wale watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunafahamu kwamba yale unayosema na kufundisha ni kweli. Haijalishi ni nani anasikiliza, unafundisha sawa kwa watu wote. Daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. 22 Tuambie, ni sahihi sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au si sahihi?”

23 Lakini Yesu alitambua watu hawa walikuwa wanajaribu kumtega. Akawaambia, 24 “Nionesheni sarafu ya fedha,” Kisha akauliza, “Jina na picha katika sarafu hii ni ya nani?”

Wakamjibu, “Ya Kaisari.”

25 Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari vilivyo vya Kaisari, na mpeni Mungu vilivyo vya Mungu.”

26 Watu wale wakashangaa jibu lake la hekima. Hawakusema kitu. Hawakuweza kumtega Yesu pale mbele za watu. Hakusema chochote kibaya ambacho wangekitumia ili kumnasa.

Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu

(Mt 22:23-33; Mk 12:18-27)

27 Baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. (Masadukayo wanaamini watu hawatafufuka kutoka kwa wafu.) Wakamwuliza, 28 “Mwalimu, Musa aliandika kwamba mtu aliyeoa akifa na hakuwa na watoto, kaka au mdogo wake amwoe mjane wake, ili wawe na watoto kwa ajili ya yule aliyekufa.[b] 29 Walikuwepo ndugu saba. Wa kwanza alioa mke lakini akafa bila ya kuwa na watoto. 30 Wa pili akamuoa yule mwanamke kisha akafa. 31 Na wa tatu akamwoa mwanamke na akafa. Kitu kile kile kikawatokea ndugu wote saba. Walikufa bila ya kuwa na watoto. 32 Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 33 Lakini ndugu wote saba walimwoa. Sasa, watu watakapofufuka kutoka kwa wafu, atakuwa mke wa yupi?”

34 Yesu akawaambia Masadukayo, “Watu huoana katika ulimwengu huu. 35 Baadhi ya watu watastahili kufufuliwa kutoka kwa wafu na kuishi tena katika ulimwengu ujao. Katika maisha yale hawataoa kamwe. 36 Katika maisha hayo, watu watakuwa kama malaika na hawatakufa. Ni watoto wa Mungu, kwa sababu wamefufuliwa kutoka kwa wafu. 37 Musa alionesha dhahiri kwamba watu hufufuliwa kutoka kwa wafu. Alipoandika kuhusu kichaka kilichokuwa kinaungua,[c] alisema kwamba Bwana ni ‘Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’(A) 38 Ni Mungu wa wanaoishi tu. Hivyo watu hawa kwa hakika hawakuwa wamekufa. Ndiyo, kwa Mungu watu wote bado wako hai.”

39 Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, jibu lako ni zuri.” 40 Hakuna hata mmoja aliyekuwa na ujasiri wa kumwuliza swali jingine.

Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?

(Mt 22:41-46; Mk 12:35-37)

41 Kisha Yesu akasema, “Kwa nini watu husema kwamba Masihi ni Mwana wa Daudi? 42 Katika kitabu cha Zaburi, Daudi mwenyewe anasema,

‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kulia,
43     na nitawaweka adui zako chini ya mamlaka yako.’[d](B)

44 Hivyo ikiwa Daudi anamwita Masihi, ‘Bwana’. Inawezekanaje Masihi awe mwana wa Daudi?”

Tahadhali Juu ya Walimu wa Sheria

(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 11:37-54)

45 Watu wote walipokuwa wanamsikiliza Yesu, akawaambia wafuasi wake, 46 “Iweni waangalifu dhidi ya walimu wa sheria. Wanapenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi yanayoonekana ya heshima. Na wanapenda pale watu wanapowasalimu kwa heshima maeneo ya masoko. Wanapenda kukaa sehemu za heshima katika masinagogi na sehemu za watu maarufu katika sherehe. 47 Lakini huwalaghai wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha kujionesha kuwa waongofu wa mioyo kuomba sala ndefu. Mungu atawaadhibu kwa hukumu kuu.”

Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli

(Mk 12:41-44)

21 Yesu alitazama na kuwaona matajiri wakimtolea Mungu sadaka zao katika sanduku la sadaka ndani ya Hekalu. Kisha akamwona mjane maskini akiweka sarafu mbili za shaba kwenye sanduku. Akasema, “Mjane huyu maskini ametoa sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kuwa, ametoa zaidi ya hao matajiri wote. Wale wanavyo vingi, na wametoa vile ambavyo hawavihitaji. Lakini mwanamke huyu ni maskini sana, lakini ametoa vyote alivyokuwa akitegemea ili aishi.”

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mt 24:1-14; Mk 13:1-13)

Baadhi ya watu walikuwa wanazungumza kuhusu uzuri wa Hekalu lililojengwa kwa mawe safi na kupambwa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo watu humtolea Mungu ili kutimiza nadhili zao.

Lakini Yesu akasema, “Wakati utafika ambao yote mnayoyaona hapa yatateketezwa. Kila jiwe katika majengo haya litatupwa chini. Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jingine.”

Baadhi ya watu wakamwuliza Yesu, “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Dalili ipi itatuonyesha kwamba ni wakati wa mambo haya kutokea?”

Yesu akasema, “Iweni waangalifu, msije mkarubuniwa. Watu wengi watakuja wakitumia jina langu, watasema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[e] na ‘Wakati sahihi umefika!’ Lakini msiwafuate. Mtakaposikia kuhusu vita na machafuko, msiogope. Mambo haya lazima yatokee kwanza. Lakini mwisho hautakuja haraka.”

10 Kisha Yesu akawaambia, “Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. 11 Kutakuwa matetemeko makubwa, kutakuwa njaa na magonjwa ya kutisha sehemu nyingi. Mambo ya kutisha yatatokea, na mambo ya kushangaza yatatokea kutoka mbinguni ili kuwaonya watu.

12 Lakini kabla ya mambo haya yote kutokea, watu watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawahukumu katika masinagogi yao na kuwafunga gerezani. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na magavana. Watawatendea mambo haya yote kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. 13 Lakini hili litawapa ninyi fursa ya kuhubiri juu yangu. 14 Msihofu namna mtakavyojitetea, 15 Nitawapa hekima kusema mambo ambayo adui zenu watashindwa kuyajibu. 16 Hata wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa, na marafiki watawageuka. Watawaua baadhi yenu. 17 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. 18 Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. 19 Mtayaokoa maisha yenu ikiwa mtaendelea kuwa imara katika imani mnapopita katika mambo haya yote.

Kuharibiwa Kwa Mji wa Yerusalemu

(Mt 24:15-21; Mk 13:14-19)

20 Mtakapoona majeshi yameuzunguka mji wa Yerusalemu, ndipo mtajua kuwa wakati wa kuharibiwa kwake umefika. 21 Watu walioko katika Uyahudi wakati huo wakimbilie milimani. Mtu yeyote atakaye kuwa Yerusalemu wakati huo aondoke haraka. Ikiwa utakuwa karibu na mji, usiingie mjini! 22 Manabii waliandika mambo mengi kuhusu wakati ambao Mungu atawaadhibu watu wake. Wakati ninaouzungumzia ni wakati ambao mambo haya yote lazima yatokee. 23 Wakati huu utakuwa mgumu kwa wanawake wenye mimba au wanaonyonyesha watoto wadogo, kwa sababu mambo mabaya yatakuja katika nchi hii. Mungu atawaadhibu watu wake kwa sababu wamemkasirisha. 24 Baadhi ya watu watauawa, wengine watafanywa watumwa na kuchukuliwa katika nchi mbalimbali. Mji mtakatifu wa Yerusalemu utatekwa na kuwekwa chini ya utawala wa wageni mpaka wakati ulioruhusiwa wao kufanya hivi utakapokwisha.

Msiogope

(Mt 24:29-31; Mk 13:24-27)

25 Mambo ya kushangaza yatatokea kwenye jua, mwezi na nyota na watu katika dunia yote wataogopa na kuchanganyikiwa kutokana na kelele za bahari na mawimbi yake. 26 Watazimia kwa hofu na kuogopa watakapoona mambo yanayoupata ulimwengu. Kila kitu katika anga kitabadilishwa. 27 Kisha watu watamwona Mwana wa Adamu akija katika wingu mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28 Mambo haya yakianza kutokea, simameni imara na msiogope. Jueni kuwa wakati wa Mungu kuwaweka huru umekaribia!”

Maneno Yangu Yataishi Milele

(Mt 24:32-35; Mk 13:28-31)

29 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Tazameni miti yote. Mtini ni mfano mzuri. 30 Unapochipua majani mnatambua kwamba majira ya joto yamekaribia. 31 Kwa namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yanatokea, mtajua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia kuja.

32 Ninawahakikishia kwamba, wakati mambo haya yote yatakapotokea, baadhi ya watu wanaoishi sasa watakuwa hai bado. 33 Ulimwengu wote, dunia yote na anga vitapita, lakini maneno yangu yataishi milele.

Kuweni Tayari Wakati Wote

34 Iweni waangalifu, msiutumie muda wenu katika sherehe za ulevi na kuhangaikia maisha haya. Mkifanya hivyo, hamtaweza kufikiri vyema na mwisho unaweza kuja mkiwa hamjajiandaa. 35 Mwisho utakuja kwa kushitukiza kwa kila mtu duniani. 36 Hivyo, iweni tayari kila wakati. Ombeni ili muepuke mambo haya yote yatakayotokea na mweze kusimama kwa ujasiri mbele za Mwana wa Adamu.”

37 Wakati wa mchana Yesu aliwafundisha watu katika eneo la Hekalu. Usiku alitoka nje ya mji na kukaa usiku kucha kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. 38 Kila asubuhi watu wote waliamka mapema kwenda kumsikiliza Yesu katika Hekalu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International