Chronological
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mk 16:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)
28 Alfajiri mapema siku iliyofuata baada ya siku ya Sabato, yaani siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu alikwenda kuliangalia kaburi.
2 Ghafla malaika wa Bwana akaja kutoka mbinguni, na tetemeko kubwa likatokea. Malaika alikwenda kaburini na kulivingirisha jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi. Kisha akaketi juu ya jiwe. 3 Malaika alikuwa anang'aa kama miali ya radi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4 Askari waliokuwa wanalinda kaburi walimwogopa sana malaika, walitetemeka kwa woga na wakawa kama watu waliokufa.
5 Malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope. Ninajua mnamtafuta Yesu, aliyeuawa msalabani. 6 Lakini hayupo hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu, kama alivyosema. Njooni mwone mahali ulipokuwa mwili wake. 7 Nendeni haraka mkawaambie wafuasi wake, ‘Yesu amefufuka kutoka kwa wafu. Amekwenda Galilaya na atafika huko kabla yenu. Na mtamwona huko.’” Kisha malaika akasema, “Sasa nimewaambia.”
8 Hivyo wanawake wakaondoka haraka kaburini. Waliogopa sana, lakini walijawa na furaha. Walipokuwa wanakimbia kwenda kuwaambia wafuasi wake kilichotokea, 9 ghafla Yesu alisimama mbele yao. Akasema, “Salamu!” Wanawake wakamwendea wakamshika miguu na wakamwabudu. 10 Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie wafuasi wangu[a] waende Galilaya, wataniona huko.”
Taarifa ya Kufufuka Yesu Yawafikia Viongozi wa Kiyahudi
11 Wanawake wakaenda kuwaambia wafuasi. Na wakati huo huo baadhi ya askari waliokuwa wanalinda kaburi waliingia mjini. Walikwenda kuwaambia viongozi wa makuhani kila kitu kilichotokea. 12 Ndipo makuhani wakakutana na viongozi wazee wa Kiyahudi na kufanya mpango. Wakawalipa wale askari pesa nyingi 13 na kuwaambia, “Waambieni watu kuwa wafuasi wake walikuja usiku na kuuiba mwili mlipokuwa mmesinzia. 14 Gavana atakaposikia juu ya hili, tutazungumza naye ili msiadhibiwe.” 15 Hivyo wale askari wakachukua pesa na kuwatii makuhani. Na jambo hili[b] bado linasambaa miongoni mwa Wayahudi hata hivi leo.
Yesu Azungumza na Wafuasi Wake
(Mk 16:14-18; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)
16 Wale wafuasi kumi na mmoja walikwenda Galilaya, kwenye mlima ambao Yesu aliwaambia waende. 17 Wakiwa mlimani, wafuasi wale walimwona Yesu na wakamwabudu. Lakini baadhi ya wafuasi hawakuwa na uhakika kama alikuwa Yesu. 18 Kisha Yesu akawajia na akasema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Hivyo nendeni ulimwenguni kote mkawafanye watu kuwa wafuasi wangu. Mkiwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. 20 Wafundisheni kutii kila kitu nilichowaambia. Na tambueni hili: Niko pamoja nanyi daima. Na nitaendelea kuwa pamoja nanyi hata mwisho wa wakati.”
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mt 28:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)
16 Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalena, Maria mama yake Yakobo, na Salome wakanunua manukato yenye harufu nzuri ili kuyapaka kwenye mwili wa Yesu. 2 Alfajiri na mapema Jumapili, mara tu baada ya jua kuchomoza, walienda kwenye kaburi la Yesu. 3 Nao walikuwa wakiambiana wao kwa wao, ni nani atakayelivingirisha jiwe litoke katika mlango wa kaburi kwa ajili yetu?
4 Kisha wakatazama juu na wakaona kuwa jiwe lile kubwa lilikuwa limevingirishwa tayari litoke mlangoni mwa kaburi la Yesu. 5 Walipoingia kaburini, wakamwona kijana mmoja ameketi upande wa kulia naye alikuwa amevaa vazi jeupe, nao wakastaajabu.
6 Naye akamwambia, “Usistaajabu. Unamtafuta Yesu wa Nazareti, aliyesulubiwa? Tazama amefufuka! Hayupo hapa. Angalieni mahali walipokuwa wameweka mwili wake. 7 Hata hivyo nendeni na kuwaeleza wafuasi wake pamoja na Petro kwamba: ‘Ametangulia mbele yenu kuelekea Galilaya. Mtamkuta kule, kama alivyowaambia.’”
8 Kwa hiyo wale wanawake walitoka na kukimbia kutoka kaburini, kwa sababu hofu na mshangao ulikuwa umewajia. Nao hawakusema chochote kwa mtu yeyote kwani waliogopa.[a]
Baadhi ya Wafuasi Wamwona Yesu
(Mt 28:9-10; Yh 20:11-18; Lk 24:13-35)
9 Baada ya Yesu kufufuka alfajiri na mapema siku ya Jumapili, alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye awali alifukuza mashetani saba kutoka kwake. 10 Baada ya Mariamu kumwona Yesu, alienda na kuwaeleza wanafunzi wake. Walikuwa wamehuzunishwa sana na walikuwa wakilia. 11 Lakini Mariamu aliwaambia kwamba Yesu yu hai. Aliwaambia ya kwamba yeye amemwona, lakini wao hawakumwamini.
12 Baada ya hayo, Yesu kwa namna tofauti akawatokea wanafunzi wake wawili walipokuwa wakitembea kuelekea mashambani. 13 Hawa kisha walirudi na wakawasimulia wengine wote, lakini nao hawakuwaamini.
Yesu Awatokea Wafuasi Wake
(Mt 28:16-20; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)
14 Baadaye, Yesu aliwatokea wale mitume kumi na mmoja walipokuwa wakila. Naye akawakaripia kwa kutokuwa na imani. Walikuwa wakaidi na walikataa kuwaamini wale waliomwona Yesu baada ya kufufuka kwake.
15 Naye akawaambia, “Nendeni ulimwenguni pote, na mkahubiri Habari Njema kwa uumbaji wote. 16 Yeyote atakayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Na wale waaminio wataweza kufanya ishara hizi kama uthibitisho: watafukuza mashetani kwa jina langu; watasema kwa lugha mpya wasizojifunza bado; 18 watakamata nyoka kwa mikono yao; na ikiwa watakunywa sumu yoyote, haitawadhuru; wataweka mikono yao kwa wagonjwa, nao watapona.”
Yesu Arudi Mbinguni
(Lk 24:50-53; Mdo 1:9-11)
19 Hivyo baada ya Bwana Yesu kuzungumza nao, alichukuliwa mbinguni, kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu. 20 Na mitume wakatoka na kwenda kuhubiri kila mahali, na Bwana alifanya kazi pamoja nao akithibitisha kuwa ujumbe wao ni wa kweli kwa ishara zilizofuatana na mahubiri yao.
© 2017 Bible League International