Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 17:1-18:18

Paulo na Sila Wakiwa Thesalonike

17 Paulo na Sila walisafiri kupitia miji ya Amfipoli na Apolonia. Wakafika katika mji wa Thesalonike, ambako kulikuwa sinagogi la Kiyahudi. Paulo aliingia katika sinagogi kuwaona Wayahudi kama alivyokuwa akifanya. Wiki tatu zilizofuatia, kila siku ya Sabato alijadiliana nao kuhusu Maandiko. Alifafanua Maandiko kuwaonesha kuwa Masihi ilikuwa afe na kufufuka kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Masihi.” Baadhi ya Wayahudi pale waliwaamini Paulo na Sila na waliamua kujiunga nao. Idadi kubwa ya Wayunani waliokuwa wanamwabudu Mungu wa kweli na wanawake wengi maarufu walijiunga nao pia.

Lakini Wayahudi ambao hawakuamini wakaingiwa na wivu, hivyo wakawakusanya baadhi ya watu wabaya katikati ya mji ili kufanya vurugu. Wakaunda kundi na wakanzisha vurugu mjini. Walikwenda nyumbani kwa Yasoni kuwatafuta Paulo na Sila. Walitaka kuwaleta mbele ya watu. Walipowakosa wakamkamata na kumburuta Yasoni na baadhi ya waamini wengine na kuwapeleka kwa viongozi wa mji. Watu wakapasa sauti na kusema, “Watu hawa Wamesababisha matatizo mengi kila mahali ulimwenguni, na sasa wamekuja hapa pia! Yasoni amewaweka nyumbani mwake. Wanavunja sheria za Kaisari. Wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu.”

Viongozi wa mji na watu wengine waliposikia hili waliudhika sana. Wakawalazimisha Yasoni na waamini wengine kuweka dhamana ya fedha kuthibitisha kuwa hakutakuwa vurugu tena. Kisha wakawaruhusu kuondoka.

Paulo na Sila Waenda Berea

10 Usiku ule ule waamini wakawapeleka Paulo na Sila katika mji mwingine ulioitwa Berea. Walipofika pale, walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi. 11 Watu wa Berea walikuwa radhi kujifunza kuliko watu wa Thesalonike. Walifurahi waliposikia ujumbe aliowaambia Paulo. Waliyachunguza Maandiko kila siku ili kuhakikisha kuwa waliyoyasikia ni ya kweli. 12 Matokeo yake ni kuwa watu wengi miongoni mwao waliamini, wakiwemo wanawake maarufu Wayunani na wanaume.

13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipojua kuwa Paulo alikuwa anawahubiri Ujumbe wa Mungu katika mji wa Berea, walikwenda huko pia. Waliwakasirisha watu na kufanya vurugu. 14 Hivyo waamini walimpeleka Paulo sehemu za pwani, lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. 15 Wale waliokwenda na Paulo walimpeleka katika mji wa Athene. Waliporudi Berea, waliwapa ujumbe kutoka kwa Paulo Timotheo na Sila kuwa waende kuungana naye haraka kadiri watakavyoweza.

Paulo Akiwa Athene

16 Paulo alipokuwa akiwasubiri Sila na Timotheo katika mji wa Athene, aliudhika kwa sababu aliona mji ulikuwa umejaa sanamu. 17 Alipokuwa katika sinagogi alizungumza na Wayahudi na Wayunani waliokuwa wakimwabudu Mungu wa kweli. Alikwenda pia katika sehemu za wazi za umma za mikutano na kuzungumza na kila aliyekutana naye. 18 Baadhi ya wanafalsafa Waepikureo[a] na baadhi ya wanafalsafa Wastoiko[b] walibishana naye.

Baadhi yao walisema, “Mtu huyu hakika hajui anachokisema. Anajaribu kusema nini?” Paulo alikuwa anawaambia Habari Njema kuhusu Yesu na ufufuo. Hivyo walisema, “Anaonekana anatueleza kuhusu baadhi ya miungu wa kigeni.”

19 Walimchukua Paulo kwenye mkutano wa baraza la Areopago. Wakasema, “Tafadhali tufafanunile hili wazo jipya ambalo umekuwa ukifundisha. 20 Mambo unayosema ni mapya kwetu. Hatujawahi kusikia mafundisho haya, na tunataka kufahamu yana maana gani.” 21 (Watu wa Athene na wageni walioishi pale walitumia muda wao bila kufanya kazi yoyote isipokuwa kusikiliza na kuzungumza kuhusu mawazo mapya.)

22 Ndipo Paulo alisimama mbele ya mkutano wa baraza la Areopago na kusema, “Watu wa Athene, kila kitu ninachokiona hapa kinanionyesha kuwa ninyi ni watu wa dini sana. 23 Nilikuwa natembea katika mji wenu na nimeona mambo mnayoyaabudu. Niliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya juu yake: ‘Kwa Mungu Asiyejulikana.’ Mnamwabudu mungu msiyemjua. Huyu ni Mungu ninayetaka kuwaambia habari zake.

24 Ni Mungu aliyeumba ulimwengu na kila kitu ndani yake. Ni Bwana wa mbingu na nchi. Haishi katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya kibinadamu. 25 Ndiye anayewapa watu uzima, pumzi na kila kitu wanachohitaji. Hahitaji msaada wowote kutoka kwao. Ana kila kitu anachohitaji. 26 Mungu alianza kwa kumwumba mtu mmoja, na kutoka kwake aliumba mataifa yote mbalimbali, na akawaweka kila mahali ulimwenguni. Na aliamua ni wakati gani na wapi ambapo angewaweka ili waishi.

27 Mungu alitaka watu wamtafute yeye, na pengine kwa kumtafuta kila mahali, wangempata. Lakini hayuko mbali na kila mmoja wetu. 28 Ni kupitia Yeye tunaweza kuishi, kufanya yale tunayofanya na kuwa kama tulivyo. Kama baadhi ya methali zenu zilivyokwisha sema, ‘Sote tunatokana naye.’

29 Huo ndio ukweli. Sote tunatokana na Mungu. Hivyo ni lazima msifikiri kuwa Yeye ni kama kitu ambacho watu hukidhania au kukitengeneza. Hivyo ni lazima tusifikiri kuwa ametengenezwa kwa dhahabu, fedha au jiwe. 30 Hapo zamani watu hawakumwelewa Mungu, naye Mungu hakulijali hili. Lakini sasa anawaagiza wanadamu kila mahali kubadilika na kumgeukia Yeye. 31 Amekwisha chagua siku ambayo atawahukumu watu wote ulimwenguni katika namna isiyo na upendeleo. Atafanya hili kwa kumtumia mtu aliyemchagua zamani zilizopita. Na alithibitisha kwa kila mtu kwamba huyu ndiye mtu atakayefanya. Alilithibitisha kwa kumfufua kutoka kwa wafu!”

32 Watu waliposikia kuhusu mtu kufufuliwa kutoka kwa kifo, baadhi yao walicheka. Lakini wengine walisema, “Tutasikiliza mengi kuhusu hili kutoka kwako baadaye.” 33 Hivyo Paulo akaondoka kwenye mkutano wa baraza. 34 Lakini baadhi ya watu waliungana na Paulo na kuwa waamini. Miongoni mwao walikuwa Dionisi, ambaye alikuwa mjumbe wa baraza la Areopago, na mwanamke aliyeitwa Damari na baadhi ya wengine.

Paulo Akiwa Korintho

18 Baadaye, Paulo aliondoka Athene na kwenda katika mji wa Korintho. Akiwa huko alikutana na Myahudi aliyeitwa Akila, aliyezaliwa katika jimbo la Ponto. Lakini yeye na mke wake aliyeitwa Prisila, walikuwa tu ndiyo wamehamia Korintho kutoka Italia. Waliondoka Italia kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ametoa amri Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo alikwenda kuwatembelea Akila na Prisila. Walikuwa watengenezaji wa mahema,[c] kama alivyokuwa Paulo, hivyo alikaa na kufanya kazi pamoja nao.

Kila siku ya Sabato Paulo alikwenda kwenye sinagogi na kuzungumza na Wayahudi na Wayunani, akijaribu kuwashawishi wamwamini Yesu. Lakini baada ya Sila na Timotheo kufika kutoka Makedonia, Paulo alitumia muda wake wote kuuhubiri ujumbe wa Mungu kwa Wayahudi, akiwaeleza kuwa Yesu ndiye Masihi. Lakini walimpinga Paulo na wakaanza kumtukana. Hivyo Paulo akakung'uta mavumbi kutoka kwenye nguo zake.[d] Akawaambia, “Msipookolewa, itakuwa makosa yenu ninyi wenyewe! Nimefanya yote ninayoweza kufanya. Baada ya hili nitawaendea watu wasio Wayahudi tu.”

Paulo aliondoka katika sinagogi na kuhamia nyumbani kwa Tito Yusto, mtu aliyekuwa anamwabudu Mungu wa Kweli, nyumba yake ilikuwa jirani na sinagogi. Krispo aliyekuwa kiongozi wa sinagogi lile, pamoja na watu wote waliokuwa wanaishi nyumbani mwake walimwamini Bwana Yesu. Watu wengi katika mji wa Korintho walimsikiliza Paulo, wakaamini na wakabatizwa.

Wakati wa usiku, Paulo aliona maono. Bwana alimwambia, “Usiogope, na usiache kuzungumza na watu. 10 Niko pamoja nawe, na hakuna atakayeweza kukudhuru. Kuna watu wangu wengi katika mji huu.” 11 Paulo alikaa pale kwa mwaka mmoja na nusu akiwafundisha watu ujumbe wa Mungu.

Paulo Afikishwa Mbele ya Galio

12 Galio alipokuwa gavana wa Akaya, baadhi ya Wayahudi walikusanyika wakawa kinyume cha Paulo. Wakampeleka mahakamani. 13 Wakamwambia Galio, “Mtu huyu anawafundisha watu kumwabudu Mungu kwa namna ambavyo ni kunyume na sheria yetu!”

14 Paulo alikuwa tayari kuzungumza, lakini Galio aliwaambia Wayahudi, “Ningewasikiliza ikiwa malalamiko yenu yangehusu dhuluma au kosa jingine. 15 Lakini yanahusu maneno na majina tu, mabishano yanayohusu sheria zenu wenyewe. Ni lazima mtatue tatizo hili ninyi wenyewe. Sitaki kuwa mwamuzi wa jambo hili.” 16 Hivyo Galio akawafanya waondoke mahakamani.

17 Kisha wote kwa pamoja wakamkamata Sosthenesi, kiongozi wa sinagogi. Wakampiga mbele ya mahakama. Lakini Galio hakulijali hili pia.

Paulo Arudi Antiokia

18 Paulo alikaa na waamini kwa siku nyingi. Kisha aliondoka na kusafiri majini kwenda Shamu. Prisila na Akila walikuwa pamoja naye pia. Walipofika Kenkrea Paulo akanyoa nywele zake kwa sababu aliweka nadhiri[e] kwa Mungu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International