Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 26

Mpango wa Kumwua Yesu

(Mk 14:1-2; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)

26 Yesu alipomaliza akasema haya yote, akawaambia wafuasi wake, “Mnajua kuwa kesho kutwa ni Pasaka. Siku hiyo Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwa maadui zake ili auawe msalabani.”

Ndipo viongozi wa makuhani na wazee walikutana katika nyumba ya Kayafa kuhani mkuu. Katika mkutano huo walitafuta njia ya kumkamata na kumwua Yesu kwa siri pasipo mtu yeyote kujua. Wakasema, “Hatuwezi kumkamata Yesu wakati wa sherehe ya Pasaka. Hatutaki watu wakasirike na kusababisha vurugu.”

Mwanamke Ampa Yesu Heshima

(Mk 14:3-9; Yh 12:1-8)

Yesu alipokuwa Bethania katika nyumba ya Simoni aliyekuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Mwanamke alimwendea, akiwa na chupa yenye manukato ya thamani kubwa. Yesu akiwa anakula, mwanamke huyo akamwagia manukato hayo kichwani.

Wanafunzi walipomwona mwanamke akifanya hivi walimkasirikia. Walisema, “Kwa nini kuharibu manukato hayo? Yangeuzwa na pesa nyingi ingepatikana, na pesa hiyo wangepewa maskini.”

10 Lakini Yesu alijua kilichokuwa kinaendelea. Akasema, “Kwa nini mnamsumbua mwanamke huyu? Amenifanyia jambo zuri sana. 11 Mtaendelea kuishi na maskini siku zote.[a] Lakini ninyi hamtakuwa nami siku zote. 12 Mwanamke huyu amenimwagia manukato. Amefanya hivi kuniandaa kwa ajili ya mazishi baada ya kufa. 13 Habari Njema itahubiriwa kwa watu wote ulimwenguni. Na ninaweza kuwathibitishia kuwa kila mahali ambako Habari Njema zitahubiriwa, jambo alilofanya mwanamke huyu litahubiriwa pia, na watu watamkumbuka.”

Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu

(Mk 14:10-11; Lk 22:3-6)

14 Ndipo Yuda Iskariote, mmoja wa wanafunzi kumi na wawili wa Yesu alikwenda kuzungumza na wakuu wa makuhani. 15 Akasema, “Nikimkabidhi Yesu kwenu, mtanilipa nini?” Makuhani walimpa sarafu thelathini za fedha. 16 Kuanzia siku hiyo, Yuda alianza kutafuta muda mzuri wa kumsaliti Yesu.

Karamu ya Pasaka

(Mk 14:12-21; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)

17 Ilipofika siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wafuasi wake walimjia Yesu na kumwambia, “Tutaandaa kila kitu kwa ajili yako ili ule mlo wa Pasaka. Unataka tuandae wapi mlo wa Pasaka?”

18 Yesu akajibu, “Nendeni mjini kwa mtu ninayemfahamu. Mwambieni kuwa Mwalimu anasema, ‘Muda uliowekwa kwa ajili yangu umekaribia sana. Mimi na wafuasi wangu tutakula mlo wa Pasaka katika nyumba yako.’” 19 Walitii na kufanya kama Yesu alivyowaambia. Waliandaa mlo wa Pasaka.

20 Jioni ilipowadia, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. 21 Walipokuwa wakila Yesu akasema, “Niaminini, ninapowaambia kuwa mmoja wenu ninyi kumi na wawili atanikabidhi kwa maadui zangu.”

22 Wanafunzi walisikitika sana waliposikia hili. Kila mmoja akasema, “Bwana, hakika si mimi!”

23 Yesu akajibu, “Yeye aliyechovya mkate wake katika kikombe kile kile nilichochovya mimi ndiye atakayenisaliti. 24 Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama Maandiko yanavyosema. Lakini ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe. Ni bora mtu huyo asingezaliwa.”

25 Ndipo Yuda, ambaye ndiye angemsaliti, akamwambia Yesu, “Mwalimu, hakika si mimi unayemzungumzia, ama ndiye?”

Yesu akamjibu, “hicho ndicho unachosema.”

Chakula cha Bwana

(Mk 14:22-26; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)

26 Walipokuwa wakila, Yesu alichukua baadhi ya mikate na akamshukuru Mungu. Alimega baadhi ya vipande, akawapa wafuasi wake na akasema, “Chukueni mkate huu na mle. Ni mwili wangu.”

27 Kisha akachukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu na akawapa. Akasema, “Kila mmoja wenu anywe divai iliyo katika kikombe hiki. 28 Divai hii ni damu yangu, itakayomwagika ili kusamehe dhambi za watu wengi na kuanza Agano Jipya ambalo Mungu analifanya na watu wake. 29 Ninataka mjue kuwa, hii ni mara ya mwisho nitakunywa divai mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”

30 Waliimba wimbo kwa pamoja kisha wakaenda kwenye Mlima wa Mizeituni.

Yesu Asema Wafuasi Wake Watamwacha

(Mk 14:27-31; Lk 22:31-34; Yh 13:36-38)

31 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Usiku wa leo ninyi nyote mtapoteza imani yangu kwangu. Maandiko yanasema,

‘Nitamwua mchungaji,
    na kondoo watatawanyika.’(A)

32 Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka Kisha nitakwenda Galilaya. Nitakuwa huko kabla ninyi hamjaenda huko.”

33 Petro akajibu, “Wafuasi wengine wote wanaweza kupoteza imani juu yako. Lakini imani yangu haitatetereka.”

34 Yesu akajibu, “Ukweli ni huu, usiku wa leo utasema haunifahamu. Utanikana mara tatu kabla jogoo hajawika.”

35 Lakini Petro akajibu, “Sitasema kwamba sikufahamu! Mimi hata nitakufa pamoja nawe!” Na wafuasi wengine wote wakasema kitu hicho hicho.

Yesu Aomba Akiwa Peke Yake

(Mk 14:32-42; Lk 22:39-46)

36 Kisha Yesu akaondoka pamoja na wafuasi wake na kwenda mahali panapoitwa Gethsemane. Akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda mahali pale kuomba.” 37 Alimwambia Petro na wana wawili wa Zebedayo waende pamoja naye. Kisha akaanza kuhuzunika na kuhangaika. 38 Yesu akamwambia Petro na wana wa Zebedayo, “Moyo wangu ni mzito na wenye huzuni hata kujisikia kana kwamba huzuni hiyo itaniua. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”

39 Kisha Yesu akaenda mbele kidogo. Akainama hadi chini uso wake ukiigusa nchi akiomba na akasema, “Baba yangu, ikiwezekana, usifanye nikinywee kikombe hiki cha mateso.[b] Lakini fanya lile ulitakalo na si lile ninalolitaka mimi.” 40 Kisha akarudi walipokuwa wafuasi wake na akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Je hamkuwa na uwezo wa kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 Amkeni kesheni na kuomba ili muyashinde majaribu. Roho zenu zinataka kufanya mambo sahihi, lakini miili yenu ni dhaifu.”

42 Kisha Yesu akaenda mara ya pili na akaomba akisema, “Baba yangu, ikiwa ni lazima nikinywee kikombe hiki na haiwezekani nikakwepa, basi mapenzi yako na yatimizwe.”

43 Kisha akarudi na kwenda walipokuwa wafuasi wake, akawakuta wamelala tena. Hawakuweza kukesha. 44 Hivyo akawaacha akaenda tena kuomba. Mara hii ya tatu alipokuwa anaomba akasema kama alivyosema hapo mwanzo.

45 Kisha Yesu akawarudia wafuasi wake na akasema, “Bado mnalala na kupumzika? Wakati wa Mwana wa Adamu kukabidhiwa kwa wenye dhambi umewadia. 46 Simameni! Tuondoke. Tazama yeye atakayenikabidhi anakuja.”

Yesu Akamatwa

(Mk 14:43-50; Lk 22:47-53; Yh 18:3-12)

47 Yesu alipokuwa anazungumza, Yuda mmoja wa wanafunzi wake kumi na mbili alifika akiwa na kundi kubwa la watu, waliokuwa wamebeba majambia na marungu. Walikuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48 Yuda aliyekuwa amkabidhi Yesu kwao, alipanga kufanya kitu cha kuwajulisha yupi kati ya wafuasi alikuwa Yesu. Alisema, “Mtu nitakayembusu ndiye mtakayemkamata.” 49 Hivyo Yuda alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Salamu, Mwalimu!” Kisha akambusu.

50 Yesu akajibu, “Rafiki yangu, fanya ulilokuja kufanya.”

Kisha wale watu wakaja na kumkamata Yesu. 51 Jambo hili lilipotokea, mmoja wa wafuasi wa Yesu alichukua jambia lake na kumkata sikio mtumishi wa kuhani mkuu.

52 Yesu akamwambia, “Rudisha jambia lako mahali pake. Atumiaye jambia atauawa kwa jambia. 53 Hakika unajua kuwa ningemwomba Baba yangu yeye angenipa zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika. 54 Lakini hilo lisingekubaliana na yale Maandiko, yanayosema hivi ndivyo ilivyopasa itokee.”

55 Kisha Yesu akaliambia kundi, “Kwa nini mnakuja kunikamata mkiwa na mikuki na marungu kama vile mimi ni mhalifu? Nimekuwa nakaa eneo la Hekalu nikifundisha kila siku. Kwa nini hamkunikamata kule? 56 Lakini mambo haya yote yametokea ili kutimiza Maandiko yaliyoandikwa na manabii.” Ndipo wafuasi wake wote wakamwacha na kukimbia.

Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini

(Mk 14:53-65; Lk 22:54-55,63-71; Yh 18:13-14,19-24)

57 Wale waliomkamata Yesu wakampeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu. Walimu wa Sheria na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwa wamekusanyika huko. 58 Petro alimfuata Yesu lakini alikuwa mbali kidogo. Alimfuata mpaka katika ua wa nyumba ya kuhani mkuu. Petro alienda uani na akakaa pamoja na walinzi. Alitaka kuona nini kingetokea.

59 Viongozi wa makuhani na baraza kuu walijaribu kutafuta kosa ili waweze kumwua Yesu. Walijaribu kutafuta watu ili wadanganye kuwa Yesu alifanya kosa. 60 Watu wengi walikuja na akasema uongo kuhusu Yesu. Lakini baraza lilishindwa kupata ushahidi wa kuutumia ili kumwua. Ndipo watu wawili walikuja 61 na akasema, “Mtu huyu[c] alisema, ‘Ninaweza kuliharibu Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’”

62 Kisha kuhani mkuu alisimama na kumwambia Yesu, “Huna neno lolote la kujitetea dhidi ya mashtaka haya juu yako? Wanasema kweli?” 63 Lakini Yesu hakusema neno lolote.

Kisha kuhani mkuu akamwambia Yesu, “Apa mbele za Mungu aliye hai kwamba utatuambia kweli. Je, wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu?”

64 Yesu akajibu, “Unaweza akasema hivyo, Mimi ndiye. Lakini ninawaambia, kitambo kidogo mtamwona Mwana wa Adamu akiwa amekaa upande wa kuume wa Mungu, mwenye Nguvu. Na mtamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65 Kuhani mkuu aliposikia hili, alilarua vazi lake kwa hasira. Akasema, “Mtu huyu amemtukana Mungu! Hatuhitaji mashahidi zaidi. Ninyi nyote mmesikia matusi yake. 66 Mnasemaje?”

Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ana hatia, na ni lazima afe.”

67 Na baadhi ya waliokuwa pale wakamtemea mate Yesu usoni na kumpiga makonde na wengine walimpiga makofi. 68 Wakasema, “Tuonyeshe kuwa wewe ni nabii, Masihi! Nani amekupiga!”

Petro Amkana Yesu

(Mk 14:66-72; Lk 22:56-62; Yh 18:15-18,25-27)

69 Petro alipokuwa amekaa nje uani, msichana mtumishi akamwendea. Akasema, “Ulikuwa pamoja na Yesu, yule mtu kutoka Galilaya.”

70 Lakini Petro akamwambia kila mtu aliyekuwa pale kuwa si kweli. Akasema “Sijui unachosema.”

71 Kisha akaondoka uani. Akiwa kwenye lango msichana mtumishi akamwona na akawaambia watu waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.”

72 Kwa mara nyingine tena Petro akasema hakuwa pamoja na Yesu. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!”

73 Baada ya muda mfupi baadaye, watu waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro na kumwambia, “Tunajua wewe ni mmoja wao. Hata namna unavyoongea inaonesha wazi kuwa ndivyo hivyo.”

74 Kisha Petro akaanza kujiapiza mwenyewe ikiwa anaongopa. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!” Mara alipomaliza akasema hili, jogoo akawika. 75 Kisha akakumbuka maneno alivyoambiwa na Yesu kuwa: “Kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu sana.

Marko 14

Mpango wa Kumwua Yesu

(Mt 26:1-5; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)

14 Ilikuwa yapata siku mbili kabla ya Sikukuu ya Pasaka na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia, kwa ujanja fulani, ya kumkamata na kumuua Yesu. Kwani walikuwa wakisema “tusifanye hivi wakati wa sherehe, ama sivyo watu watafanya fujo.”

Mwanamke Ampa Yesu Heshima

(Mt 26:6-13; Yh 12:1-8)

Yesu alikuwa Bethania, katika nyumba ya Simoni mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Wakati ameketi mezani mwanamke mmoja alimwijia. Naye alikuwa na gudulia la mawe lililojaa manukato ya bei ghali yaliyotengenezwa kwa nardo safi. Mwanamke huyo alilifungua gudulia lile kwa kulivunja na kumwagia Yesu manukato kichwani mwake.

Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na kulalamika miongoni mwao, “Kwa nini kuwepo na ufujaji wa manukato namna hii? Gharama yake ni sawa na mshahara wa mwaka[a] mzima. Manukato haya yangeweza kuuzwa na fedha hiyo kupewa walio maskini.” Kisha wakamkosoa yule mwanamke kwa hasira kwa jambo alilolifanya.

“Lakini Yesu alisema mwacheni peke yake. Kwa nini mnamsumbua? Yeye amenifanyia kitendo chema. Kwani siku zote mnao maskini pamoja nanyi na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini hamtakuwa pamoja nami siku zote. Yeye amefanya kile alichokiweza kufanya. Ameumwagia manukato mwili wangu kabla ya wakati kuuandaa kwa ajili ya maziko. Ninawaambia kweli: Popote injili itakapohubiriwa ulimwenguni, kile alichokifanya kitasimuliwa kwa kumkumbuka.”

Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu

(Mt 26:14-16; Lk 22:3-6)

10 Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na mbili, aliwaendea viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. 11 Nao walifurahi kusikia hivyo, na wakaahidi kumpa fedha. Kwa hiyo Yuda akaanza kutafuta wakati unaofaa wa kumsaliti.

Karamu ya Pasaka

(Mt 26:17-25; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)

12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, ambapo kila mara mwana kondoo alitolewa sadaka kwa ajili ya Pasaka. Wanafunzi wa Yesu wakamwendea na kumwuliza, “Ni wapi unapotaka tuende kukuandalia ili uweze kuila Karamu ya Pasaka?”

13 Hivyo Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, naye akawaeleza, “ingieni mjini, na mtakutana na mtu mmoja aliyebeba gudulia la maji. Mfuateni, 14 popote pale atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba ile, ‘mwalimu anasema, utuonyeshe chumba ambacho yeye na wanafunzi wake wanaweza kuila Karamu ya Pasaka.’ 15 Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, klichoandaliwa tayari kwa ajili yetu. Basi mtuandalie chakula pale.”

16 Wanafunzi wa Yesu waliondoka na kuelekea mjini. Huko walikuta kila kitu kama vile Yesu alivyowaeleza Hivyo, waliandaa mlo wa Pasaka.

17 Wakati wa jioni Yesu alienda pamoja na wanafunzi wake kumi na mbili katika nyumba ile. 18 Wote walipokuwa wameketi mezani wakila, Yesu akasema, “Mniamini ninapowambia kwamba mmoja wenu, yule anayekula nami sasa atanitoa kwa maadui zangu.”

19 Wanafunzi walihuzunika sana kusikia jambo hili. Kila mmoja akamwambia Yesu, “Hakika siyo mimi?”

20 Akawaambia, “Ni mmoja wa wale kumi na mbili; na ni yule atakayechovya mkate katika bakuli pamoja nami. 21 Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama ilivyoandikwa juu yake. Lakini itakuwa ya kutisha namna gani kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu anasalitiwa. Itakuwa bora mtu huyu asingelikuwa amezaliwa.”

Chakula cha Bwana

(Mt 26:26-30; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)

22 Na walipokuwa wakila Yesu aliuchukua mkate, akamshukuru Mungu kwa huo. Akamega vipande, akawapa wanafunzi wake, na kusema, “Chukueni na mle mkate huu. Ni mwili wangu.”

23 Kisha akakichukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu kwa hicho, akawapa. Wote wakanywa toka kile kikombe. 24 Kisha akasema, “Kinywaji hiki ni damu yangu ambayo kwayo Mungu anafanya agano na watu wake. Damu yangu inamwagika kwa manufaa ya watu wengi. 25 Ninawaambia kweli sitakunywa diva tena mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya katika Ufalme wa Mungu.”

26 Na wao wakaimba mwimbo wa sifa na kutoka na kuelekea kwenye Mlima wa Miti ya Mizeituni.

Yesu Asema Wafuasi Wake Watamwacha

(Mt 26:31-35; Lk 22:31-34; Yh 13:36-38)

27 Yesu akawaambia, “Nyote mtaniacha, kwani imeandikwa,

‘Nitamuua mchungaji,
    na kondoo watatawanyika.’(A)

28 Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka kutoka kwa wafu. Kisha nitaenda Galilaya. Nitakuwa pale kabla ninyi hamjafika.”

29 Lakini Petro akamwambia, “Hata kama wengine wote watapoteza imani yao, mimi sitapoteza imani yangu.”

30 Ndipo Yesu akamjibu kusema, “Ukweli ni kwamba, usiku wa leo utasema kuwa hunijui. Utasema hivyo mara tatu kabla ya jogoo kuwika mara mbili.”

31 Petro akasema kwa kusisitiza zaidi, “Hata kama itanipasa kufa nawe, sitasema kuwa sikujui.” Na wengine wakasema hivyo.

Yesu Aomba Akiwa Peke Yake

(Mt 26:36-46; Lk 22:39-46)

32 Kisha wakafika mahali palipoitwa Gethsemane. Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati ninaomba.” 33 Naye Yesu akamchukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, naye akaanza kusumbuka sana. 34 Akawaambia, “Nina huzuni sana na ninafikiri inaweza kuniua. Kaeni hapa, na mjihadhari.”

35 Akiendelea mbele kidogo, alianguka chini, na akaomba ikiwezekana angeiepuka saa ya mateso. 36 Akasema, “Aba,[b] yaani Baba, vyote vinawezekana kwako wewe. Hebu kiondoe kikombe[c] hiki kutoka kwangu, Lakini usifanye kama ninavyopenda mimi, lakini kama unavyopenda wewe.”

37 Kisha Yesu akaja na kuwakuta wamelala, na akamwuliza Petro, “Simoni, je umelala? Je, hukuweza kukaa macho kwa muda wa saa moja tu? 38 Kaeni macho na kuomba, ili msije mkaingia majaribuni. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.”

39 Yesu akaondoka kwenda kuomba tena, akilisema jambo lile lile. 40 Kisha akarudi tena na kuwakuta wamelala, kwani macho yao yalikuwa yamechoka. Wao hawakujua la kusema kwake.

41 Alirudi mara ya tatu na kuwaambia, “Je, bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imefika. Mwana wa Adamu atasalitiwa mikononi mwa watenda dhambi. 42 Amkeni! Twendeni! Tazama! Yule atakayenisaliti amekaribia.”

Yesu Akamatwa

(Mt 26:47-56; Lk 22:47-53; Yh 18:3-12)

43 Mara moja, wakati Yesu akali akizungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na mbili, alitokea. Pamoja naye walikuwa kundi kubwa la watu waliokuwa na majambia na marungu wakitoka kwa viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na wazee.

44 Msaliti alikuwa tayari amewapa ishara: “Yule ambaye nitambusu ndiye mwenyewe. Mkamateni, mlindeni na muwe waangalifu mnapomwondoa.” 45 Mara tu Yuda alipowasili, alimwendea Yesu. Alipomkaribia alisema, “Mwalimu!” Kisha akambusu. 46 Ndipo walipomkamata na kumshikilia. 47 Mmoja wa wale waliosimama naye karibu akautoa upanga wake alani, akampiga nao mtumishi wa kuhani mkuu na kulikata sikio lake.

48 Kisha Yesu akawaambia, “Je, mlikuja kunikamata kwa upanga na marungu, kama vile mimi nimekuwa jambazi? 49 Kila siku nilikuwa nanyi, nikifundisha Hekaluni na hamkujaribu kunikamata wakati huo. Lakini Maandiko lazima yatimie.” 50 Wafuasi wake wote walimwacha na kumkimbia.

51 Miongoni mwa watu waliomfuata Yesu alikuwa kijana mmoja aliyevaa kipande cha nguo. Watu walipotaka kumkamata 52 alikiacha kile kipande cha nguo mikononi mwao na kukimbia akiwa uchi.

Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini

(Mt 26:57-68; Lk 22:54-55,63-71; Yh 18:13-14,19-24)

53 Nao wakamwongoza Yesu kumpeleka kwa kuhani mkuu, na viongozi wote wa makuhani, wazee, na walimu wa Sheria walikutanika. 54 Petro akamfuata Yesu kwa mbali kidogo hadi ndani ya baraza la nyumba ya kuhani mkuu. Petro alikuwa ameketi na wale walinzi akijipasha joto na moto walioukoka.

55 Viongozi wa makuhani na Baraza lote la Wayahudi walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu wa kuweza kumhukumu kifo, lakini hawakupata kitu chochote. 56 Watu wengi walikuja na kutoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini wote walisema vitu tofauti. Ushahidi wao ulipingana.

57 Kisha wengine walisimama na kushuhudia kinyume chake kwa uongo, wakisema, 58 “Tulimsikia mtu huyu[d] akisema, ‘Nitaliharibu Hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono ya wanadamu, na kwa siku tatu nitajenga lingine ambalo halikujengwa kwa mikono.’” 59 Lakini hata katika ushahidi wao huu hawakukubaliana.

60 Kisha kuhani mkuu akasimama mbele yao na akamwuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Nini ushahidi huu ambao watu wanaleta dhidi yako?” 61 Lakini Yesu alinyamaza kimya na hakutoa jibu lolote.

Kwa mara nyingine kuhani mkuu akamwuliza, “Je, wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu anayesifiwa?”

62 Yesu akasema, “Mimi ndiye. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye uweza wote akija pamoja na mawingu ya mbinguni.”[e]

63 Kuhani mkuu alichana mavazi yake na kusema, “Tuna haja gani ya kuleta mashahidi zaidi? 64 Ninyi wote mmesikia akimtolea Mungu matusi.”

Wote walimhukumu na kumwona kwa anastahili kifo. 65 Na wengine walianza kutema mate, na kufunika uso wake, na kumpiga, na kumwambia, “Uwe nabii na utuambie nani aliyekupiga.” Kisha wale walinzi walimchukua na kuendelea kumpiga.

Petro Amkana Yesu

(Mt 26:69-75; Lk 22:56-62; Yh 18:15-18,25-27)

66 Wakati Petro alipokuwa bado barazani, mtumishi wa kike wa kuhani mkuu alifika pale. 67 Alipomwona Petro akijipasha moto, alimkazia macho na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

68 Lakini Petro alisema, “Hii si kweli, mie sifahamu wala kuelewa kile unachokisema.” Baada ya hapo Petro alitoka na kwenda barazani na hapo hapo jogoo akawika.

69 Yule mtumishi wa kike alipomwona alirudia tena kuwaeleza wale waliokuwa wamesimama pale, “Mtu huyu ni mmoja wao!” 70 Kwa mara nyingine tena Petro alikataa.

Baada ya muda mfupi wale waliokuwa wamesimama pale wakarudia tena kumwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa sababu wewe pia ni Mgalilaya.”

71 Petro akaanza kutoa maneno makali na kusema, “Naapa kwa Mungu, simjui mtu huyu mnayemzungumzia!”

72 Mara jogoo akawika kwa mara ya pili, na Petro akakumbuka lile neno la Yesu alilomwambia: “Kabla kogoo hajawika mara ya pili utanikana mara tatu.” Naye akavunjika moyo na kuanza kulia.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International