Book of Common Prayer
Yatoeni Maisha Yenu kwa Mungu
12 Hivyo, dada na kaka zangu, upokeeni wema mkuu ambao Mungu alituonyesha. Itoeni miili yenu[a] kama sadaka hai kwake. Ishini kwa ajili ya Mungu tu na mweze kumpendeza yeye. Mkizingatia kwa makini yale aliyoyatenda, ni sahihi na inapasa kumwabudu Mungu kwa njia hii. 2 Msifikiri au kuenenda kama watu wa ulimwengu huu, bali mruhusuni Mungu aibadilishe namna yenu ya kufikiri ndani yenu. Ndipo mtaweza kuelewa na kuyathibitisha yale Mungu anayotaka kutoka kwenu; yote yaliyo mema, yanayompendeza yeye na yaliyo makamilifu.
3 Mungu amenipa mimi zawadi maalumu, na ndiyo sababu nina kitu cha kusema na kila mmoja wenu. Msifikiri kuwa ninyi ni bora kuliko jinsi mlivyo kwa asili. Mnapaswa kujiona kadri mlivyo. Mjipime wenyewe jinsi mlivyo kwa imani ambayo Mungu alimpa kila mmoja wetu. 4 Kila mmoja wetu anao mwili mmoja, na mwili huo una viungo vingi. Viungo hivi vyote havifanyi mambo yanayofanana. 5 Kwa jinsi hiyo hiyo, sisi ni watu wengi, lakini kwa sababu ni wa Kristo, sote ni mwili mmoja. Sisi sote ni viungo vya mwili huo, na kila kiungo ni sehemu ya viungo vingine vyote.
6 Sote tunazo karama tofauti tofauti. Kila karama ilikuja kwa sababu ya neema aliyotupa Mungu. Yule aliye na karama ya unabii anapaswa kuitumia karama hiyo kwa namna inayokubalika kiimani. 7 Aliye na karama ya kuhudumia anapaswa kuhudumia. Aliye na karama ya kufundisha anapaswa kufundisha. 8 Aliye na karama ya kufariji wengine anapaswa kufanya hivyo. Aliye na karama ya kuhudumia mahitaji ya wengine anapaswa kutoa kwa moyo mweupe. Aliye na karama ya kuongoza anapaswa kufanya kwa juhudi katika hiyo. Aliye na karama ya kuonesha wema kwa wengine anapaswa kufanya hivyo kwa furaha.
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mk 14:1-2; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)
26 Yesu alipomaliza akasema haya yote, akawaambia wafuasi wake, 2 “Mnajua kuwa kesho kutwa ni Pasaka. Siku hiyo Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwa maadui zake ili auawe msalabani.”
3 Ndipo viongozi wa makuhani na wazee walikutana katika nyumba ya Kayafa kuhani mkuu. 4 Katika mkutano huo walitafuta njia ya kumkamata na kumwua Yesu kwa siri pasipo mtu yeyote kujua. 5 Wakasema, “Hatuwezi kumkamata Yesu wakati wa sherehe ya Pasaka. Hatutaki watu wakasirike na kusababisha vurugu.”
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mk 14:3-9; Yh 12:1-8)
6 Yesu alipokuwa Bethania katika nyumba ya Simoni aliyekuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. 7 Mwanamke alimwendea, akiwa na chupa yenye manukato ya thamani kubwa. Yesu akiwa anakula, mwanamke huyo akamwagia manukato hayo kichwani.
8 Wanafunzi walipomwona mwanamke akifanya hivi walimkasirikia. Walisema, “Kwa nini kuharibu manukato hayo? 9 Yangeuzwa na pesa nyingi ingepatikana, na pesa hiyo wangepewa maskini.”
10 Lakini Yesu alijua kilichokuwa kinaendelea. Akasema, “Kwa nini mnamsumbua mwanamke huyu? Amenifanyia jambo zuri sana. 11 Mtaendelea kuishi na maskini siku zote.[a] Lakini ninyi hamtakuwa nami siku zote. 12 Mwanamke huyu amenimwagia manukato. Amefanya hivi kuniandaa kwa ajili ya mazishi baada ya kufa. 13 Habari Njema itahubiriwa kwa watu wote ulimwenguni. Na ninaweza kuwathibitishia kuwa kila mahali ambako Habari Njema zitahubiriwa, jambo alilofanya mwanamke huyu litahubiriwa pia, na watu watamkumbuka.”
Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu
(Mk 14:10-11; Lk 22:3-6)
14 Ndipo Yuda Iskariote, mmoja wa wanafunzi kumi na wawili wa Yesu alikwenda kuzungumza na wakuu wa makuhani. 15 Akasema, “Nikimkabidhi Yesu kwenu, mtanilipa nini?” Makuhani walimpa sarafu thelathini za fedha. 16 Kuanzia siku hiyo, Yuda alianza kutafuta muda mzuri wa kumsaliti Yesu.
© 2017 Bible League International