Book of Common Prayer
25 Ndugu zangu, ieleweni siri hii ya ukweli. Kweli hii itawasaidia ninyi mjue kuwa hamfahamu kila kitu. Kweli ni hii: Sehemu ya Israeli wamefanywa kuwa wakaidi, lakini hiyo itabadilika wasio Wayahudi, wengi, watakapokuja kwa Mungu. 26 Na hivyo ndivyo Israeli wote watakavyookolewa. Kama Maandiko yanavyosema,
“Mwokozi atakuja kutoka Sayuni;
atauondoa uovu kutoka kwa wazaliwa wa Yakobo.
27 Nami nitalifanya patano hili na watu wale
nitakapoziondoa dhambi zao.”(A)
28 Kwa sasa, Wayahudi wanaokataa kuzipokea Habari Njema wamekuwa adui wa Habari Njema. Hili limetokea kwa manufaa yenu ninyi msio Wayahudi. Lakini bado Wayahudi ni wateule wa Mungu, na anawapenda kwa sababu ya ahadi alizozifanya kwa baba zao. 29 Mungu habadili mawazo yake kuhusu watu anaowaita. Kamwe haamui kuzirudisha baraka alizokwisha kuwapa. 30 Wakati mmoja ninyi pia mlikataa kumtii Mungu. Lakini sasa mmeipokea rehema, kwa sababu Wayahudi walikataa kutii. 31 Na sasa wao ndiyo wanaokataa kutii, kwa sababu Mungu aliwaonesha ninyi rehema zake. Lakini hili limetokea ili nao pia waweze kupokea rehema kutoka kwake. 32 Mungu amemfungia kila mmoja katika gereza la kutokutii. Lakini amefanya hivi ili aweze kuonesha rehema yake kwa wote.
Sifa kwa Mungu
33 Ndiyo, utajiri wa Mungu ni mkuu sana! Hekima yake na ufahamu wake havina mwisho! Hakuna awezaye kuelezea yale Mungu anayoyaamua. Hayupo awezaye kuzielewa njia zake. 34 Kama Maandiko yanavyosema,
“Nani anaweza kuyajua yaliyo katika mawazo ya Bwana?
Nani anaweza kumshauri?”(B)
35 “Nani amewahi kumpa Mungu kitu chochote?
Mungu hadaiwi kitu chochote na mtu yeyote.”(C)
36 Ndiyo, Mungu ameviumba vitu vyote. Na kila kitu kinaendelea kuwepo kwa njia na kwa ajili yake. Utukufu uwe kwa Mungu milele yote! Amina.
Yesu, Mwana wa Adamu Atawahukumu Watu Wote
31 Mwana wa Adamu atakuja akiwa katika utukufu wake, pamoja na malaika wote. Ataketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa mfalme. 32 Watu wote wa ulimwenguni watakusanywa mbele zake, kisha atawagawa katika makundi mawili. Itakuwa kama mchungaji anavyowatenga kondoo kutoka katika kundi la mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wa kushoto.
34 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kuume, ‘Njooni, baba yangu ana baraka kuu kwa ajili yenu. Ufalme alioahidi ni wenu sasa. Uliandaliwa kwa ajili yenu tangu dunia ilipoumbwa. 35 Ni wenu kwa sababu nilipokuwa na njaa, mlinipa chakula. Nilipokuwa na kiu, mlinipa maji ya kunywa. Nilipokosa mahali pa kukaa, mlinikaribisha katika nyumba zenu. 36 Nilipokosa nguo, mlinipa mavazi ya kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa, mlinijali. Nilipofungwa gerezani, mlikuja kunitembelea.’
37 Kisha wenye haki watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakupa chakula? Lini tulikuona una kiu tukakupa maji ya kunywa? 38 Lini tulikuona huna mahali pa kukaa tukakukaribisha katika nyumba zetu? Lini tulikuona huna nguo za kuvaa na tukakuvisha? 39 Lini tulikuona unaumwa au uko gerezani tukaja kukuona?’
40 Kisha mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, kila mlichowafanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si watu wa thamani, mlinifanyia mimi pia.’
41 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu. Mungu amekwisha amua kuwa mtaadhibiwa. Nendeni katika moto uwakao milele, moto ulioandaliwa kwa ajili ya yule Mwovu na malaika zake. 42 Ondokeni kwa sababu nilipokuwa na njaa, hamkunipa chakula nile. Nilipokuwa na kiu, hamkunipa maji ya kunywa. 43 Nilipokosa mahali pa kukaa, hamkunikaribisha katika nyumba zenu. Nilipokosa nguo za kuvaa, hamkunipa nguo za kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa au mfungwa gerezani hamkunijali.’
44 Ndipo watu hao watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu? Lini tulikuona huna mahali pa kukaa? Au ni lini tulikuona huna nguo au mgonjwa au ukiwa gerezani? Tuliona haya yote lini na hatukukusaidia?’
45 Mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, chochote mlichokataa kumfanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si wa muhimu, mlikataa kunifanyia mimi.’
46 Ndipo watu hawa watakapondolewa ili kuadhibiwa milele. Lakini wenye haki watakwenda kuyafurahia maisha ya milele.”
© 2017 Bible League International