Book of Common Prayer
17 Kaka na dada zangu, ninataka muwe macho na wale wanaosababisha mabishano na kuumiza imani za watu kwa kufundisha mambo ambayo ni kinyume cha yale mliyojifunza. Mjitenge nao. 18 Watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu. Wanajifurahisha wenyewe tu. Wanatumia mazungumzo matamu na kusema mambo yanayopendeza ili kuwadanganya wale wasiojua kuhusu uovu. 19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu kwa Bwana, nami nafurahi sana juu ya hilo. Lakini ninataka muwe werevu kuhusu yaliyo mema na kutokujua lolote kuhusu yaliyo maovu.
20 Mungu mwenye kuleta amani atamwangamiza Shetani mapema na kuwapa nguvu juu yake.
Neema ya Bwana wetu Yesu iwe pamoja nanyi.
21 Timotheo, mtumishi pamoja nami, anawatumieni salamu. Pia Lukio, Yasoni na Sosipatro (hawa ni jamaa zangu) wanawatumieni salamu.
22 Mimi Tertio, ninayeandika barua hii kwa ajili ya Paulo. Ninawasalimu kama mmoja aliye wa Bwana.
23 Gayo ameniruhusu na kanisa lote hapa kuitumia nyumba yake. Anawatumia salamu zake. Erasto na kaka yetu Kwarto pia wanatuma salamu. Erasto ndiye mtunza hazina wa mji hapa. 24 [a]
25 Atukuzwe Mungu! Yeye ndiye anayeweza kuzitumia Habari Njema ninazozifundisha kuwaimarisha katika imani. Ni ujumbe ninaowaambia watu kuhusu Yesu Kristo. Ujumbe huo ni siri ya ukweli iliyofichwa kwa karne nyingi sana lakini sasa imefunuliwa. 26 Na kweli hiyo sasa imeonyeshwa kwetu. Ilijulishwa kwa yale ambayo manabii waliandika katika Maandiko, kama Mungu wa milele alivyoagiza. Na sasa imejulikana kwa mataifa yote ili waweze kuamini na kumtii yeye. 27 Utukufu wa milele ni kwa Mungu mwenye hekima pekee kwa njia ya Yesu Kristo. Amina.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mk 15:21-32; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)
32 Askari walipokuwa wanatoka mjini wakiwa na Yesu, walimwona mtu mmoja kutoka Kirene aliyeitwa Simoni, na wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 33 Walifika mahali palipoitwa Golgotha. (Yaani “Eneo la Fuvu la Kichwa”.) 34 Askari walimpa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo.[a] Lakini alipoionja, alikataa kuinywa.
35 Askari walimgongomea Yesu msalabani, kisha wakacheza kamari ili wagawane nguo za Yesu. 36 Askari walikaa pale ili kumlinda. 37 Wakaweka alama juu ya kichwa chake kuonesha mashtaka dhidi yake yaliyosema: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.
38 Wahalifu wawili waligongomewa kwenye misalaba pamoja na Yesu, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto wa Yesu. 39 Watu waliokuwa wakipita pale walitikisa vichwa vyao na kumtukana Yesu matusi 40 kwa kusema, “Ulisema ungeweza kubomoa Hekalu na kulijenga tena katika siku tatu. Jiokoe mwenyewe! Teremka chini kutoka kwenye huo msalaba ikiwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu!”
41 Viongozi wa Makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwepo pale pia. Nao pia walimdhihaki Yesu kama watu wengine walivyofanya. 42 Walisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa yeye mwenyewe! Watu husema kuwa yeye ni mfalme wa Israeli. Ikiwa yeye ni mfalme, ashuke kutoka msalabani. Ndipo tutamwamini. 43 Alimtumaini Mungu. Hivyo Mungu amwokoe sasa, ikiwa hakika Mungu anamtaka. Yeye mwenyewe alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44 Hata wale wahalifu wawili waliokuwa misalabani upande wa kulia na wa kushoto wa Yesu walimtukana.
© 2017 Bible League International