Book of Common Prayer
13 Je, hii ina maana kuwa kitu ambacho ni kizuri kiliniletea kifo? Hapana, ni dhambi iliyoitumia amri nzuri ndiyo iliyoniletea kifo. Hii inaonesha kwa hakika kuwa dhambi ni dhambi. Dhambi inaweza kutumia amri iliyo nzuri na kuleta matokeo yanayoonesha ubaya wake mkubwa.
Vita ndani Yetu
14 Tunafahamu kuwa sheria ni ya rohoni, lakini mimi si wa rohoni. Mimi ni mwanadamu hasa. Dhambi inanitawala kana kwamba mimi ni mtumwa wake. 15 Sielewi ni kwa nini ninatenda jinsi ninavyotenda. Sitendi mema ninayotaka kuyatenda, bali ninatenda maovu ninayoyachukia. 16 Na ikiwa ninatenda kile nisichotaka kutenda, inamaanisha kuwa ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini kwa hakika siyo mimi mwenyewe ninayetenda maovu. Bali dhambi inayokaa ndani yangu ndiyo inatenda hayo. 18 Ndiyo, ninajua kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu, nina maana kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu kisichokuwa cha rohoni. 19 Sitendi mema ninayotaka nitende. Ninatenda maovu nisiyotaka kutenda. 20 Hivyo ikiwa ninatenda yale nisiyotaka kutenda, hakika si mimi ninayeyatenda hayo. Bali dhambi inayoishi ndani yangu ndiyo inayotenda.
21 Hivyo nimejifunza hivi kuhusu sheria: Ninapotaka kutenda mema ambayo sheria inaamrisha, uovu unakuwa hapo hapo pamoja nami. 22 Moyoni mwangu nafurahi kuifuata sheria ya Mungu. 23 Lakini naiona “sheria” nyingine ikitenda kazi ndani yangu, nayo imo vitani dhidi ya sheria inayokubalika akilini mwangu. “Sheria” hii nyingine ni utawala wa dhambi inayonishinda na inanifanya kuwa mfungwa wake. 24 Mimi ni mtu mwenye taabu kiasi gani! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu unaoniletea kifo? 25 Namshukuru Mungu kwa wokovu wake kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo katika ufahamu wangu mimi ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika udhaifu wangu wa kibinadamu mimi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mk 12:1-12; Lk 20:9-19)
33 Sikilizeni simulizi hii: Alikuwepo mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Alijenga uzio kuzunguka shamba lile la mizabibu na akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu.[a] Kisha akajenga mnara wa lindo. Akalikodisha shamba kwa wakulima kisha akasafiri. 34 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, akawatuma watumishi wake waende kwa wakulima ili apate gawio lake la zabibu.
35 Lakini wakulima waliwakamata wale watumishi na kumpiga mmoja wao. Wakamwua mwingine na wa tatu wakampiga kwa mawe mpaka akafa. 36 Hivyo mwenye shamba akawatuma baadhi ya watumishi wengine wengi zaidi ya aliowatuma hapo kwanza. Lakini wakulima wakawatendea kama walivyowatendea watumishi wa kwanza. 37 Hivyo mwenye shamba akaamua kumtuma mwanaye kwa wakulima. Alisema, ‘Wakulima watamheshimu mwanangu.’
38 Lakini wakulima walipomwona mwanaye, wakaambizana, ‘Huyu ni mwana wa mwenye shamba. Shamba hili litakuwa lake. Tukimwua, shamba la mizabibu litakuwa letu.’ 39 Hivyo wakulima wakamchukua mwana wa mwenye shamba, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu na kumwua.
40 Hivyo mmiliki wa shamba la mizabibu atawafanya nini wakulima hawa atakaporudi?”
41 Makuhani wa Kiyahudi na viongozi wakasema, “Kwa hakika atawaua watu hao waovu. Kisha atawakodishia wakulima wengine shamba hilo, watakaompa gawio la mazao yake wakati wa mavuno.”
42 Yesu akawaambia, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko:
‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Bwana amefanya hivi,
na ni ajabu kubwa kwetu kuliona.’(A)
43 Hivyo ninawaambia kuwa, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na watapewa watu wanaofanya mambo anayoyataka Mungu katika ufalme wake. 44 Kila aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika na litamsaga kila linayemwangukia.”[b]
45 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia simulizi hizi, wakajua kuwa Yesu alikuwa anawasema wao. 46 Walitaka kumkamata Yesu. Lakini waliogopa kwani watu waliamini kuwa Yesu ni nabii.
© 2017 Bible League International