Book of Common Prayer
Paulo Azungumzia Kazi Yake
14 Kaka na dada zangu, najua pasipo mashaka kuwa mmejaa wema na mnayo maarifa yote mnayohitaji. Hivyo kwa hakika mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi. 15 Lakini nimewaandikia ninyi kwa ujasiri wote kuhusu mambo fulani niliyotaka mkumbuke. Nilifanya hivi kwa sababu Mungu alinipa karama hii maalumu: 16 kuwa mtumishi wa Kristo Yesu kwa ajili ya wasio Wayahudi. Natumika kama kuhani ambaye kazi yake ni kuhubiri Habari Njema kutoka kwa Mungu. Alinipa mimi jukumu hili ili ninyi msio Wayahudi mweze kuwa sadaka atakayoikubali, sadaka iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
17 Na hii ndiyo sababu najisikia vizuri kuhusu yale yote yaliyofanyika kwa ajili ya Mungu kwa kuwa mimi ni mali ya Kristo Yesu. 18 Sitazungumzia chochote nilichofanya mwenyewe. Nitazungumza tu kuhusu yale Kristo aliyofanya akinitumia mimi katika kuwaongoza wale wasiokuwa Wayahudi katika kutii. Ni yeye aliyetenda kazi katika yale niliyosema na kufanya. 19 Alitenda kazi kwa ishara za miujiza kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Matokeo yake ni kuwa nimewahubiri watu Habari Njema kuhusu Kristo kuanzia Yerusalemu na kuzunguka kote mpaka Iliriko. Na hivyo nimemaliza sehemu hiyo ya wajibu wangu. 20 Imekuwa shabaha yangu daima kuzihubiri Habari Njema katika sehemu ambako watu hawajawahi kusikia juu ya Kristo. Nafanya hivi kwa sababu sitaki kujenga katika kazi ambayo tayari mtu mwingine amekwisha kuianza. 21 Kama Maandiko yanavyosema,
“Wale ambao hawakuambiwa kuhusu yeye wataona,
na wale ambao hawajasikia juu yake wataelewa.”(A)
Mpango wa Paulo Kwenda Rumi
22 Kazi hiyo imenifanya niwe na shughuli nyingi sana na mara nyingi imenizuia kuja kuwaona.
23 Kwa miaka mingi nimetamani kuwatembelea, na sasa nimekamilisha kazi yangu katika maeneo haya. 24 Hivyo nitawatembelea nitakapoenda Hispania. Ndiyo, napanga kusafiri kwenda Hispania na natumaini kuwatembelea nikiwa njiani. Nitakaa kwa muda na kufurahi pamoja nanyi. Kisha natumaini mtanisaidia kuendelea na safari yangu.
Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato
(Mk 15:1; Lk 23:1-2; Yh 18:28-32)
27 Mapema asubuhi, viongozi wote wa makuhani na viongozi wazee walikutana na kuamua kumwua Yesu. 2 Wakamfunga kamba, wakamwondoa na kwenda kumkabidhi kwa Pilato, gavana wa Kirumi.
Yuda Ajiua
(Mdo 1:18-19)
3 Baada ya kumkabidhi Yesu, Yuda aliona kila kitu kilichotokea na kujua kuwa wameamua kumwua Yesu. Naye alihuzunika sana kutokana na kile alichokifanya. Hivyo alirudisha vile vipande thelathini vya sarafu vya fedha kwa wakuu wa makuhani na viongozi wazee. 4 Yuda aliwaambia, “Nimetenda dhambi. Nimemsaliti kwenu mtu asiye na hatia ili auawe.”
Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Hilo halituhusu. Ni tatizo lako, siyo letu sisi.”
5 Hivyo Yuda akavitupa vipande thelathini vya fedha Hekaluni, kisha akatoka akaenda kujinyonga.
6 Viongozi wa makuhani wakaviokota vile vipande vya fedha Hekaluni. Wakasema, “Sheria yetu haituruhusu kuweka fedha hii katika hazina ya Hekalu, kwa sababu fedha hii imelipwa kwa ajili ya kifo, ni fedha yenye damu.” 7 Hivyo wakaamua kutumia fedha hiyo kwa kununulia shamba linaloitwa Shamba la Mfinyanzi kwa ajili ya kuwazikia wageni wanapokufa wakiwa ziarani katika mji wa Yerusalemu. 8 Ndiyo sababu eneo hilo bado linaitwa Shamba la Damu. 9 Hili lilitimiza maneno ya nabii Yeremia aliposema:
“Walichukua sarafu thelathini za fedha. Hicho ni kiasi ambacho Waisraeli waliamua kulipa kwa ajili ya uhai wake. 10 Walizitumia sarafu hizo thelathini za fedha kununulia shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniamuru.”[a]
© 2017 Bible League International