Book of Common Prayer
Mungu Hajawakataa Watu wake
11 Hivyo ninauliza, “Je, Mungu aliwakataa watu wake?” Hapana! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, wa ukoo wa Ibrahimu, katika kabila la Benjamini. 2 Mungu aliwachagua Waisraeli wawe watu wake kabla hawajazaliwa. Na hajawakataa. Hakika mnajua Maandiko yanavyosema kuhusu Eliya anapomwomba Mungu dhidi ya watu wa Israeli. Anasema, 3 “Bwana, wamewaua manabii wako na kuharibu madhabahu zako. Mimi ndiye nabii pekee niliyebaki hai, na sasa wanajaribu kuniua mimi pia.”(A) 4 Lakini ni jibu gani Mungu alilompa Eliya? Mungu alisema, “Nimejihifadhia watu elfu saba wasiomwabudu Baali.”(B)
5 Ndivyo ilivyo sasa. Mungu amewachagua watu wachache kwa neema yake. 6 Na kama aliwachagua kwa neema yake, hivyo si kwa sababu ya matendo yao yaliyowafanya wawe watu wake. Kama wangefanywa kuwa watu wake kutokana na matendo yao, zawadi yake ya neema isingekuwa zawadi halisi.
7 Hivyo hivi ndivyo ilivyotokea: Watu wa Israeli wanazitaka sana baraka za Mungu, lakini si wote waliozipata. Watu aliowachagua walipata baraka zake, lakini wengine wakawa wagumu na wakakataa kumsikiliza. 8 Kama Maandiko yanavyosema,
“Mungu aliwafanya watu walale usingizi.”(C)
“Mungu aliyafumba macho yao ili wasione,
na aliyaziba masikio yao ili wasisikie.
Hili linaendelea hata sasa.”(D)
9 Na Daudi anasema,
“Watu hawa na wakamatwe na kunaswa
katika tafrija wanazofurahia.
Nyakati hizo nzuri ziwasababishe waanguke
ili wapate adhabu wanayoistahili.
10 Yapofushe macho yao ili wasiweze kuona.
Ipindishe migongo yao kwa mzigo wa matatizo.”(E)
11 Hivyo nauliza: Pale watu wa Mungu walipojikwaa na kuanguka, Je, hawakuweza kuinuka tena? Hakika hapana! Lakini kujikwaa kwao katika mwendo kulileta wokovu kwa wale wasio Wayahudi. Kusudi la hili lilikuwa kuwafanya Wayahudi wapate wivu. 12 Kosa lao na hasara yao vilileta baraka za utajiri kwa ulimwengu kwa wasio Wayahudi. Hivyo fikirini ni kwa kiasi gani baraka hizi zitakuwa kubwa kwa ulimwengu pale idadi ya kutosha ya Wayahudi watakapokuwa watu wa aina ile anayoitaka Mungu.
Wanawali Kumi
25 Nyakati hizo, ufalme wa Mungu utafanana na wanawali kumi waliokwenda kusubiri kuwasili kwa bwana arusi wakiwa na taa zao. 2 Watano kati yao walikuwa na hekima, na watano walikuwa wajinga. 3 Wanawali wajinga walichukua taa zao bila ya kubeba mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao. 4 Wanawali wenye hekima walichukua taa zao pamoja na mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao katika chupa. 5 Bwana arusi alipochelewa sana, walichoka na wote wakasinzia.
6 Usiku wa manane ulipofika, ikatangazwa, ‘Bwana arusi anakuja! Njooni mumlaki!’
7 Wasichana wote waliamka. Wakatayarisha taa zao. 8 Lakini wanawali wajinga wakawaambia wanawali wenye hekima, ‘Tupeni mafuta kiasi kwa sababu mafuta katika taa zetu yamekwisha.’
9 Wanawali wenye hekima wakajibu, ‘Hapana! Mafuta tuliyonayo hayatatutosha sisi sote. Lakini nendeni kwa wauza mafuta mkanunue.’
10 Hivyo wanawali wajinga wakaenda kununua mafuta. Walipoondoka, bwana arusi akafika. Wanawali waliokuwa tayari wakaingia kwenye sherehe ya arusi pamoja na bwana arusi. Kisha mlango ukafungwa.
11 Baadaye wanawali waliokwenda kununua mafuta wakarudi. Wakasema, ‘bwana, bwana! Fungua mlango tuingie.’
12 Lakini bwana arusi akajibu, ‘Kwa hakika hapana! Wala siwajui ninyi.’
13 Hivyo iweni tayari kila wakati. Hamjui siku wala muda ambao Mwana wa Adamu atakuja.
© 2017 Bible League International