Book of Common Prayer
Uthibitisho kutoka kwa Mungu
12 Mitume walipewa nguvu ya kufanya ishara nyingi za miujiza na maajabu katikati ya watu. Walikuwa wanakutanika pamoja mara kwa mara katika eneo la Hekalu lililoitwa Ukumbi wa Sulemani. 13 Hakuna mtu yeyote ambaye hakuwa mwamini alikaa na kushirikiana nao, lakini kila mtu alisema mambo mazuri juu yao. 14 Watu wengi zaidi na zaidi walimwamini Bwana; na watu wengi, wanaume kwa wanawake waliongezwa katika kundi la waamini. 15 Hivyo watu waliwatoa wagonjwa majumbani na kuwaweka mitaani katika vitanda vidogo na mikeka. Walitumaini kuwa ikiwa Petro atapita karibu yao na kivuli chake kikawaangukia watapona. 16 Watu walikuja kutoka katika miji kuzunguka Yerusalemu. Waliwaleta wagonjwa au waliosumbuliwa na pepo wachafu. Wote waliponywa.
Mitume Wakamatwa
17 Kuhani mkuu na wafuasi wake wote wa karibu, kundi liitwalo Masadukayo wakaingiwa wivu sana. 18 Waliwakamata mitume na kuwafunga katika gereza la mji. 19 Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana alifungua milango ya gereza. Malaika akawaongoza mitume nje ya gereza na kusema, 20 “Nendeni mkasimame katika eneo la Hekalu. Waelezeni watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya.” 21 Mitume waliposikia hili, walifanya kama walivyoambiwa. Walikwenda katika eneo la Hekalu asubuhi na mapema jua lilipokuwa linachomoza na kuanza kuwafundisha watu.
Kuhani mkuu na wafuasi wake wakakusanyika na kuitisha mkutano wa Baraza kuu na wazee wa Kiyahudi. Wakawatuma baadhi ya watu gerezani ili wawalete mitume kwao. 22 Watu wale walipokwenda gerezani, hawakuwaona mitume. Hivyo walirudi na kuwaambia viongozi wa Kiyahudi kuhusu hili. 23 Walisema, “Gereza lilikuwa limefungwa na milango ilikuwa imefungwa. Walinzi walikuwa wamesimama milangoni. Lakini tulipofungua milango, gereza lilikuwa tupu!” 24 Mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani walipolisikia hili, walichanganyikiwa na kujiuliza maana yake ni nini.
25 Ndipo mtu mwingine akaja na kuwaambia, “Sikilizeni! Watu mliowafunga gerezani wamesimama katika eneo la Hekalu wanawafundisha watu!” 26 Mkuu wa walinzi na askari walinzi wa Hekalu walikwenda na kuwarudisha mitume. Lakini askari hawakutumia nguvu, kwa sababu waliwaogopa watu. Waliogopa watu wangewapiga kwa mawe mpaka wafe.
Maneno Yangu Yataishi Milele
(Mt 24:32-35; Mk 13:28-31)
29 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Tazameni miti yote. Mtini ni mfano mzuri. 30 Unapochipua majani mnatambua kwamba majira ya joto yamekaribia. 31 Kwa namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yanatokea, mtajua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia kuja.
32 Ninawahakikishia kwamba, wakati mambo haya yote yatakapotokea, baadhi ya watu wanaoishi sasa watakuwa hai bado. 33 Ulimwengu wote, dunia yote na anga vitapita, lakini maneno yangu yataishi milele.
Kuweni Tayari Wakati Wote
34 Iweni waangalifu, msiutumie muda wenu katika sherehe za ulevi na kuhangaikia maisha haya. Mkifanya hivyo, hamtaweza kufikiri vyema na mwisho unaweza kuja mkiwa hamjajiandaa. 35 Mwisho utakuja kwa kushitukiza kwa kila mtu duniani. 36 Hivyo, iweni tayari kila wakati. Ombeni ili muepuke mambo haya yote yatakayotokea na mweze kusimama kwa ujasiri mbele za Mwana wa Adamu.”
© 2017 Bible League International