Book of Common Prayer
Luka Aandika Kitabu Kingine
1 Mpendwa Theofilo:
Katika kitabu cha kwanza niliandika kuhusu kila kitu ambacho Yesu alitenda na kufundisha tangu mwanzo 2 mpaka siku alipochukuliwa juu mbinguni. Kabla hajaondoka, alizungumza na mitume aliowachagua kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuhusu mambo waliyotakiwa kufanya. 3 Hii ilikuwa baada ya kifo chake, ambapo aliwathibitishia kwa namna nyingi kuwa alikuwa hai. Mitume walimwona Yesu mara nyingi kwa muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. Naye Yesu alizungumza nao kuhusu ufalme wa Mungu. 4 Wakati mmoja Yesu alipokuwa akila pamoja nao, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu. Aliwaambia, “Kaeni hapa mpaka mtakapopokea kile ambacho Baba aliahidi kutuma. Kumbukeni, niliwaambia juu yake. 5 Yohana aliwabatiza watu kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
Yesu Achukuliwa Juu Mbinguni
6 Mitume walipokuwa pamoja, walimwuliza Yesu, “Bwana, huu ni wakati wako wa kuwarudishia Waisraeli ufalme wao tena?”
7 Yesu akawaambia, “Baba peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na nyakati. Si juu yenu kujua. 8 Lakini Roho Mtakatifu atawajia na kuwapa nguvu. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu. Mtawahubiri watu kuhusu mimi kila mahali, kuanzia humu Yerusalemu, Uyahudi yote, katika Samaria na hatimaye kila mahali ulimwenguni.”
9 Baada ya kusema haya, alichukuliwa juu mbinguni. Walipokuwa wanaangalia juu angani, wingu lilimficha na hawakuweza kumwona. 10 Walikuwa bado wanatazama angani alipokuwa anakwenda. Ghafla malaika wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama pembeni mwao. 11 Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mmesimama hapa na mnatazama angani? Mlimwona Yesu akichukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni. Atarudi katika namna hii hii kama mlivyomwona akienda.”
Mtume Mpya Achaguliwa
12 Ndipo mitume walirudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, ulio umbali wa kama kilomita moja[a] kutoka Yerusalemu. 13 Walipoingia mjini, walikwenda kwenye chumba cha ghorofani walikokuwa wanakaa. Hawa ndiyo wale waliokuwepo: Petro, Yohana, Yakobo, na Andrea, Filipo, Thomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo (mwana wa Alfayo), na Simoni Mzelote, na Yuda (mwana wa Yakobo).
14 Mitume hawa wote walikuwa pamoja na waliomba kwa nia moja. Baadhi ya wanawake, Mariamu mama wa Yesu na wadogo zake Bwana Yesu walikuwepo pale pamoja na mitume.
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mt 21:33-46; Mk 12:1-12)
9 Yesu akawaambia watu kisa hiki; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Kisha akalikodisha kwa wakulima, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwa wakulima wale ili wampe sehemu yake ya zabibu. Lakini wakulima wale walimpiga yule mtumishi na wakamfukuza bila kumpa kitu. 11 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi mwingine. Wakulima walimpiga mtumishi huyu pia, wakamwaibisha na kumfukuza bila kumpa kitu. 12 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi wa tatu. Wakulima wakampiga sana mtumishi huyu na wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.
13 Mmiliki wa shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa. Yumkini watamheshimu.’ 14 Lakini wakulima walipomwona mwana wa mwenye shamba, wakajadiliana wakisema, ‘Huyu ni mwana wa mmiliki wa shamba. Shamba hili la mizabibu litakuwa lake. Tukimwua, litakuwa letu.’ 15 Hivyo wakulima wakamtupa mwana wa mmiliki wa shamba nje ya shamba la mizabibu na wakamwua.
Je, mmiliki wa shamba la mizabibu atafanya nini? 16 Atakuja na atawaua wale wakulima, kisha atalikodisha shamba kwa wakulima wengine.”
Watu waliposikia mfano huu, wakasema, “Hili lisije kutokea!” 17 Lakini Yesu akawakazia macho na akasema, “Hivyo basi, Maandiko haya yanamaanisha nini:
‘Jiwe lililokataliwa na wajenzi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni?’[a]
18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika na ikiwa jiwe hilo litaangukia, litakusaga!”
19 Walimu wa sheria na wakuu wa makuhani waliposikia kisa hiki, walijua unawahusu wao. Hivyo walitaka kumkamata Yesu wakati huo huo, lakini waliogopa watu wangewadhuru.
© 2017 Bible League International