Book of Common Prayer
Msaada kwa Watu wa Mungu Katika Uyahudi
8 Na sasa, kaka na Dada zetu, tunataka kuwaambia kile ambacho neema ya Mungu imefanya katika makanisa ya makedonia. 2 Waamini hawa wamepitia katika masumbufu makubwa, na ni maskini sana. Lakini furaha yao kubwa iliwafanya kuwa wakarimu zaidi katika kutoa kwao. 3 Ninaweza kuwaambia kwamba walitoa kulingana na uwezo wao na hata zaidi ya uwezo wao. Hakuna mtu yeyote aliyewaambia kufanya hivyo. Hilo lilikuwa wazo lao. 4 Walituuliza tena na tena na walitusihi tuwaruhusu kushiriki katika huduma hii kwa ajili ya watu wa Mungu. 5 Na walitoa kwa namna ambayo sisi wenyewe hatukutegemea: kwanza walijitoa wenyewe kwa Mungu na kwetu kabla ya kutoa fedha zao. Hili ndilo Mungu anataka. 6 Kwa hiyo tulimwomba Tito awasaidie ninyi kuikamilisha kazi hii maalum ya kutoa. Tito ndiye aliyeianzisha kazi hii kwanza miongoni mwenu. 7 Ninyi ni matajiri kwa kila kitu; katika imani, katika uwezo wa kuzungumza, katika maarifa, katika utayari wa kusaidia kwa njia yo yote, na katika upendo mliojifunza kutoka kwetu. Hivyo sasa tunawataka muwe matajiri katika kazi hii ya kutoa pia.
8 Siwashurutishi ninyi kutoa, ila nataka niujaribu upendo wenu kuona ni wa kiasi gani kuwalinganisha na wengine ambao wamekuwa tayari na wana hiari ya kusaidia. 9 Mnaifahamu neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mnafahamu kuwa aliacha utajiri wake mbinguni na kufanyika maskini kwa ajili yenu. Aliacha kila kitu ili ninyi mbarikiwe kwa wingi zaidi.
10 Hili ndilo ninafikiri mnapaswa kufanya: mwaka jana mlikuwa wa kwanza kutaka kutoa, na mkawa wa kwanza kutoa. 11 Hivyo sasa ikamilisheni kazi mliyoianzisha. Kisha kutenda kwenu kutakuwa sawa na “kutaka” kwenu “kutenda”. Toeni kutokana na kile mlicho nacho. 12 Ikiwa mnataka kutoa, sadaka yenu itapokelewa. Sadaka yenu itahukumiwa kutokana na kile mlicho nacho, si kwa kile msichonacho. 13 Hatupendi muwe na mizigo wakati wengine wanastarehe. Tunataka kila kitu kiwe katika hali ya usawa. 14 Wakati huu mnavyo vingi na kuzidi na mnaweza kuwapa kila wanachohitaji. Kisha baadaye, watakapokuwa navyo vingi, wataweza kuwapa mnavyohitaji. Kisha kila mmoja atakuwa na mgao ulio sawa. 15 Kama Maandiko yanavyosema,
“Wale waliokusanya vingi hawakuwa na vingi zaidi,
na wale waliokusanya kidogo hawakuwa na vichache zaidi.”(A)
Tito na Wale Watakaosafiri Pamoja Naye
16 Namshukuru Mungu kwa sababu alimpa Tito upendo ule ule nilionao mimi kwenu.
Mungu Atawajibu Watu Wake
18 Kisha Yesu akawafundisha wafuasi wake kwamba wanapaswa kuomba daima bila kupoteza tumaini. Akatumia simulizi hii kuwafundisha. 2 Akasema, “Kulikuwa na mwamuzi katika mji fulani. Hakumcha Mungu wala hakujali watu walikuwa wanamfikiriaje. 3 Na katika mji huo huo alikuwepo mwanamke mjane. Huyu alimjia mwamuzi huyu mara nyingi akimwambia, ‘Kuna mtu anayenitendea mambo mabaya. Nipe haki yangu!’ 4 Mwanzoni mwamuzi hakutaka kumsaidia yule mwanamke. Lakini baada ya muda kupita, akawaza moyoni mwake yeye mwenyewe, ‘Simchi Mungu. Na sijali watu wananifikiriaje. 5 Lakini mwanamke huyu ananisumbua. Nikimpa haki yake ataacha kunisumbua. Nisipomsaidia, ataendelea kunijia na anaweza kunishambulia.’”
6 Bwana akasema, “Sikilizeni, maneno aliyosema mwamuzi mbaya yana mafundisho kwa ajili yenu. 7 Daima Mungu atawapa mahitaji yao wateule wanaomwomba usiku na mchana. Hatachelewa kuwajibu. 8 Ninawaambia, Mungu atawapa haki yao watu wake haraka. Lakini Mwana wa Adamu atakaporudi, atawakuta duniani watu ambao bado wanamwamini?”
© 2017 Bible League International