Book of Common Prayer
21 Ninaona aibu kusema haya, lakini tulikuwa “dhaifu sana” kuyafanya mambo kama hayo kwenu.
Lakini kama kuna mtu aliye jasiri vya kutosha kujivuna, nami nitajivuna pia. (Ninaongea hivi kama mjinga.) 22 Je, watu hao ni Wayahudi? Mimi pia. Je, ni Waebrania? Mimi pia. Je, wanatoka katika familia ya Ibrahimu? Mimi pia. 23 Je, wanamtumikia Kristo? Mimi ninamtumikia zaidi sana. (Je, mimi ni mwendawazimu kuongea kwa jinsi hii?) Nimefanya kazi kwa juhudi kuliko wao. Nimekuwa gerezani mara nyingi. Nimepigwa vibaya sana. Nimekuwa katika hali za hatari ya kufa mara nyingi.
24 Mara tano Wayahudi wamenipa adhabu ya viboko 39. 25 Mara tatu katika nyakati tofauti nimepigwa kwa fimbo. Mara moja nilikuwa karibu kuuawa kwa kupigwa kwa mawe. Mara tatu nimevunjikiwa na merikebu, na mara moja katika hizo nilikesha usiku na kushinda kutwa nzima tukielea baharini. 26 Katika safari zangu za mara kwa mara nimekuwa katika hatari za kwenye mito, majambazi, watu wangu wenyewe, na toka kwa watu wasio Wayahudi. Nimekuwa katika hatari mijini, katika maeneo wasioishi watu, na katika bahari. Na nimekuwa katika hatari za watu wanaojifanya kuwa waamini lakini siyo waamini.
27 Nimefanya kazi ngumu na za kuchosha, na mara nyingi sikuweza kulala usingizi. Nimekuwa mwenye njaa na kiu. Mara nyingi nimekosa kula chakula. Nimekuwa katika hali ya baridi na kutokuwa na nguo za kujifunika. 28 Na kuna matatizo mengine mengi zaidi. Mojawapo ya hayo ni mzigo nilio nao kila siku wa majukumu yangu: Ninawaza juu ya makanisa yote. 29 Ninajisikia kuwa mdhaifu kila mara mtu mwingine anapokuwa dhaifu. Ninapata hasira sana pale mtu yeyote anapoingizwa dhambini.
30 Ikiwa ni lazima nisifu, nitajisifu katika vitu vinavyonidhihirisha kuwa mimi ni dhaifu. 31 Mungu ajua kuwa sisemi uongo. Yeye ni Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na anapaswa kutukuzwa milele. 32 Nilipo kuwa Dameski, gavana wa mfalme Areta alitaka kunikamata, hivyo aliweka walinzi nje ya malango ya jiji. 33 Lakini baadhi ya marafiki wakaniweka ndani ya kikapu. Kisha wakaniteremsha chini kupitia dirisha lililokuwa kwenye katika ukuta wa mji. Hivyo nikamtoroka gavana.
Simulizi Kuhusu Watumishi Watatu
(Mt 25:14-30)
11 Kundi la watu walipokuwa bado wanamsikiliza Yesu akizungumza mambo haya. Akaongeza kwa kuwasimulia simulizi hii. Na sasa alikuwa karibu na mji wa Yerusalemu na watu walidhani kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa unakwenda kutokea haraka. 12 Akasema, “Mtu mmoja maarufu alikuwa anajiandaa kwenda katika nchi ya mbali kutawazwa kuwa mfalme. Kisha arudi nyumbani na kuwatawala watu wake. 13 Hivyo aliwaita watumishi wake kumi kwa pamoja. Akampa kila mtumishi fungu la pesa.[a] Akamwambia kila mtumishi, ‘Zifanyie biashara pesa hizi mpaka nitakaporudi.’ 14 Lakini watu katika ule ufalme walikuwa wanamchukia mtu huyu na hivyo walituma kundi la watu kwenda katika nchi nyingine. Walipofika huko wakasema, ‘Hatutaki mtu huyu awe mfalme wetu.’
15 Lakini mtu yule akatawazwa kuwa mfalme. Aliporudi nyumbani, akaagiza akasema, ‘Waiteni wale watumishi wenye pesa zangu. Ninataka kujua wamezalisha kiasi gani kutokana na pesa hizo.’ 16 Mtumishi wa kwanza alikuja na akasema, ‘Mkuu, nilizalisha mafungu kumi ya pesa kutokana na fungu moja ulilonipa.’ 17 Mfalme akamwambia, ‘Vizuri sana! Wewe ni mtumishi mwema. Nilikuamini kwa vitu vidogo, lakini sasa utakuwa mtawala wa miji yangu kumi.’
18 Mtumishi wa pili akasema, ‘Mkuu, kwa fungu moja la pesa zako, nilizalisha mafungu matano.’ 19 Mfalme akamwambia mtumishi huyu, ‘Utatawala miji yangu mitano.’
20 Kisha mtumishi mwingine akaingia na akasema, ‘Mkuu, fungu lako la pesa hili hapa. Nilizifunga katika kipande cha nguo na kulificha. 21 Niliogopa kwa sababu wewe ni mgumu. Unachukua hata pesa ambazo hukuzizalisha na kukusanya chakula ambacho hukupanda.’
22 Kisha mfalme akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya! Nitatumia maneno yako mwenyewe kukuhukumu. Unasema kuwa mimi ni mtu mgumu, ninachukua hata pesa ambazo sikuzizalisha na nakusanya chakula ambacho sikupanda? 23 Ikiwa hiyo ni kweli, ulipaswa kuweka pesa zangu kwa watoao riba. Ili nitakaporudi pesa hiyo iwe imezalisha faida.’ 24 Kisha mfalme akawaambia watu waliokuwa pale, ‘Mnyang'anyeni mtumishi huyu fungu la pesa na mpeni mtumishi aliyezalisha mafungu kumi ya pesa.’
25 Lakini watu wakamwambia mfalme, ‘Mkuu, yule mtumishi ana mafungu kumi tayari.’
26 Mfalme akasema, ‘Waliozalisha faida watapata zaidi. Lakini ambao hawakuzalisha faida watanyang'anywa kila kitu. 27 Sasa, adui zangu wako wapi? Wako wapi watu ambao hawakutaka niwe mfalme? Waleteni adui zangu hapa na waueni huku nikiangalia wanavyokufa.’”
© 2017 Bible League International