Book of Common Prayer
Joka na Mwanamke Anayezaa
12 Jambo la ajabu lilionekana mbinguni: Mwanamke aliyevalishwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake alionekana. Alikuwa na taji yenye nyota kumi na mbili kichwani pake. 2 Alikuwa na mimba na alilia kwa uchungu kwa sababu alikuwa karibu ya kuzaa.
3 Kisha ajabu nyingine ikaonekana mbinguni: Alikuweko huko joka mkubwa mwekundu. Joka huyo alikuwa na vichwa saba na alikuwa na taji juu ya kila kichwa. Na alikuwa na pembe kumi. 4 Mkia wake ulizoa theluthi ya nyota na kuziangusha duniani. Joka hili lilisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa karibu ya kuzaa mtoto. Lilitaka kumla mtoto mara atakapozaliwa.
5 Mwanamke alimzaa mtoto wa kiume, atakayewatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya chuma. Na mwana wa mwanamke huyu alichukuliwa juu mbinguni kwa Mungu, kwenye kiti chake cha enzii. 6 Mwanamke alikimbilia jangwani mpaka mahali ambako Mungu amemwandalia. Huko angetunzwa kwa siku 1,260.
7 Kisha kulikuwa vita mbinguni. Mikaeli[a] na malaika zake walipigana na joka. Nalo joka na malaika zake wakapigana na Mikaeli pamoja na malaika zake, 8 lakini joka na malaika zake hawakuwa na nguvu za kutosha kushinda, na hivyo wakapoteza nafasi zao mbinguni. 9 Likatupwa chini kutoka mbinguni. (Joka hili kubwa ni nyoka yule wa zamani, aitwaye Ibilisi au Shetani, anayeudanganya ulimwengu wote.) Joka na malaika zake walitupwa duniani.
10 Kisha nilisikia sauti kubwa mbinguni ikisema:
“Ushindi na uweza na ufalme wa Mungu wetu
na mamlaka ya Masihi wake umekuja sasa,
kwa sababu mshitaki wa kaka na dada zetu
ametupwa chini.
Ndiye aliyewashitaki kwa Mungu,
mchana na usiku.
11 Walimshinda kwa sadaka ya damu ya Mwanakondoo
na kwa ujumbe wa Mungu waliowaambia watu.
Hawakuyapenda maisha yao sana.
Hawakuogopa kifo.
12 Hivyo furahi, ewe mbingu
na wote waishio humo!
Lakini ole kwa nchi na bahari,
kwa sababu Ibilisi ameshuka kwako.
Amejaa ghadhabu.
Anajua ana muda mchache.”
Yesu Awaponya Watu Wengi
29 Kisha Yesu akatoka pale na kwenda pwani ya Ziwa Galilaya. Alipanda vilima na akaketi chini.
30 Kundi kubwa la watu likamwendea. Walileta watu wengine wengi waliokuwa wagonjwa na kuwaweka mbele yake. Walikuwepo watu wasioweza kutembea, wasiyeona, walemavu wa miguu, wasiyesikia na wengine wengi. 31 Watu walishangaa walipoona kuwa waliokuwa wasiyesema walianza kusema, walemavu wa miguu waliponywa, waliokuwa hawawezi kutembea waliweza kutembea, wasiyeona waliweza kuona. Kila mtu alimshukuru Mungu wa Israeli kwa hili.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000
(Mk 8:1-10)
32 Kisha Yesu akawaita wafuasi wake na kuwaambia, “Ninawaonea huruma watu hawa. Wamekuwa pamoja nami kwa siku tatu, na sasa hawana chakula. Sitaki niwaache waende wakiwa na njaa. Wanaweza kuzimia njiani wanaporudi nyumbani.”
33 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha watu wote hawa? Tuko nyikani mbali ni miji.”
34 Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tuna mikate saba na samaki wadogo wachache.”
35 Yesu akawaambia watu waketi chini. 36 Akaichukua mikate saba na samaki. Akamshukuru Mungu kwa sababu ya chakula. Akaigawa vipande vipande, akawapa wafuasi wake na wafuasi wakawapa watu chakula. 37 Watu wote walikula mpaka wakashiba. Baada ya hili, wafuasi walijaza vikapu saba kwa vipande vya chakula vilivyosalia ambavyo havikuliwa. 38 Walikuwepo wanaume 4,000 pale waliokula. Walikuwepo pia wanawake na watoto. 39 Baada ya wote kula, Yesu akawaambia watu wanaweza kwenda nyumbani. Alipanda mashua na kwenda eneo la Magadani.
© 2017 Bible League International