Book of Common Prayer
3 Hatutaki watu waone makosa katika kazi yetu. Hivyo hatutendi jambo lolote litakalokuwa kikwazo kwa wengine. 4 Lakini kwa kila njia tunaonesha kuwa sisi ni watumishi wa Mungu. Hatukati tamaa, ingawa tunakutana na matatizo, mambo magumu na matatizo ya kila namna. 5 Tumepigwa na kutupwa gerezani. Watu wameanzisha fujo dhidi yetu. Tumefanya kazi kwa bidii, mara nyingi pasipo kula ama kulala. 6 Tunadhihirisha kuwa sisi tu watumishi wa Mungu kutokana na maisha yetu safi, kwa ufahamu wetu, kwa subira yetu na kwa upole wetu. Tunadhihirisha hilo kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo wetu wa kweli, 7 kwa kusema iliyo kweli, na kwa kuzitegemea nguvu za Mungu. Njia hii iliyo sahihi ya kuishi imetuandaa kujitetea wenyewe kinyume na kila aina ya shambulizi.
8 Baadhi ya watu wanatuheshimu, lakini wengine wanatudhihaki. Wengine wanasema mema juu yetu, lakini wengine wasema mabaya juu yetu. Wengine wanatusema kuwa tu waongo, lakini tunasema kweli. 9 Kwa wengine hatufahamiki, lakini twajulikana sana. Tunaonekana kama watu wanaostahili kufa, lakini angalia! Twadumu kuishi. Tunaadhibiwa, lakini hatuuawi. 10 Tuna huzuni nyingi, lakini tunafuraha kila siku. Tu maskini, lakini tunawafanya watu wengi kuwa matajiri katika imani. Hatuna kitu, lakini tunakila kitu.
11 Tumesema kwa uhuru kwenu ninyi watu wa Korintho. Tumefungua mioyo yetu kwenu. 12 Upendo wetu kwenu haujakoma. Ninyi ndiyo mliouzuia upendo wenu kwetu. 13 Ninawaambia kama watoto wangu. Fanyeni vivyo hivyo kama sisi tulivyotenda kwenu; fungueni mioyo yenu pia.
Sisi ni Hekalu la Mungu
14 Ninyi hamko sawa na wale wasioamini. Hivyo msifungwe nira pamoja nao. Wema na ubaya havikai pamoja. Nuru na giza haviwezi kukaa pamoja katika chumba kimoja. 15 Itawezekanaje kuwe na mapatano kati ya Kristo na beliali?[a] Je, mwamini anashirika gani na asiye amini? 16 Hekalu la Mungu halina mapatano yoyote na sanamu, na sisi tu hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu anavyosema,
“Nitakaa kati yao
na kutembea nao;
Nitakuwa Mungu wao,
na watakuwa watu wangu.”(A)
17 “Hivyo tokeni nje kati yao
na jitengeni nao, asema Bwana.
Msishike chochote kilicho kichafu,
nami nitawakaribisha.”(B)
18 “Nitakuwa baba yenu,
nanyi mtakuwa wana wangu na binti zangu,
asema Bwana Mwenyezi.”(C)
7 Rafiki wapendwa, tuna ahadi hizi toka kwa Mungu. Hivyo tujitakase maisha yetu na kuwa huru kutoka kwa kila kinachofanya miili yetu ama roho zetu kuwa najisi. Heshima yetu kwa Mungu itufanye tujaribu kuwa watakatifu kabisa kwa namna tunavyoishi.
Yesu Awaponya Baadhi ya Wayahudi na Msamaria
11 Yesu alikuwa anasafiri kwenda Yerusalemu. Alipotoka Galilaya alisafiri akipita kando ya mpaka wa Samaria. 12 Aliingia katika mji mdogo, na wanaume kumi walimwendea. Hawakumkaribia, kwa sababu wote walikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. 13 Lakini watu wale wakaita kwa kupaza sauti wakisema, “Yesu! Mkuu! Tafadhali utusaidie!”
14 Yesu alipowaona, akasema, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.”[a]
Wale watu kumi walipokuwa wanakwenda kujionesha kwa makuhani, waliponywa. 15 Mmoja wao alipoona kuwa amepona, alirudi kwa Yesu huku akimsifu Mungu kwa kupaza sauti. 16 Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu, akamshukuru. (Alikuwa Msamaria.) 17 Yesu akasema, “Watu kumi wameponywa, wengine tisa wako wapi? 18 Mtu huyu wala si mmoja wa watu wetu. Ni yeye peke yake aliyerudi kumsifu Mungu?” 19 Ndipo Yesu akamwambia, “Inuka! Unaweza kwenda. Umeponywa kwa sababu uliamini.”
© 2017 Bible League International