Book of Common Prayer
Tito na Wale Watakaosafiri Pamoja Naye
16 Namshukuru Mungu kwa sababu alimpa Tito upendo ule ule nilionao mimi kwenu. 17 Tito alikubali kufanya vile tulivyomwomba. Yeye mwenyewe alitamani sana kuja kwenu. 18 Tunamtuma Tito pamoja ndugu anayekubalika katika makanisa yote. Anasifiwa kwa sababu ya huduma yake ya Habari Njema. 19 Pia, alichaguliwa na makanisa kuambatana nasi tunapoleta sadaka hii. Tunafanya huduma hii kumpa Bwana heshima[a] na kuonesha kuwa tunapenda kusaidia.
20 Tunajitahidi kuwa waangalifu ili asiwepo mtu wa kutukosoa kwa namna ambavyo tunashugulika na sadaka hii kubwa. 21 Tunajaribu kutenda lililo jema. Tunataka kufanya kile ambacho Bwana anakubali kuwa sahihi na kile ambacho watu wanafikiri kuwa ni sahihi.
22 Pia, tunawatuma pamoja nao kaka yetu ambaye yuko tayari siku zote kutoa msaada. Amethibitisha hili kwetu mara nyingi na kwa njia nyingi. Na anataka kusaidia zaidi sasa kwa sababu ana imani zaidi nanyi.
23 Na sasa kuhusu Tito, yeye ni mshirika mwenzangu. Anafanya kazi pamoja nami kuwasaidia ninyi. Na kuhusu hawa kaka wawili wengine: wao wametumwa kutoka katika makanisa mengine, na wanaleta heshima kwa Kristo. 24 Hivyo waonesheni watu hawa kuwa mna upendo. Waonesheni kwa nini tunajisifia ninyi. Ndipo makanisa yote yatakapo tambua hili.
Farisayo na Mtoza Ushuru
9 Walikuwepo baadhi ya watu waliojiona kuwa wenye haki na waliwadharau wengine. Yesu alitumia simulizi hii kuwafundisha: 10 “Siku moja Farisayo na mtoza ushuru walikwenda Hekaluni kuomba. 11 Farisayo alisimama peke yake mbali na mtoza ushuru. Farisayo aliomba akisema, ‘Ee Mungu, ninakushukuru kwa kuwa mimi si mwovu kama watu wengine. Mimi siyo kama wezi, waongo au wazinzi. Ninakushukuru kwa kuwa mimi ni bora kuliko huyu mtoza ushuru. 12 Ninafunga mara mbili kwa wiki na kutoa sehemu ya kumi ya vyote ninavyopata!’
13 Mtoza ushuru alisimama peke yake pia. Lakini alipoanza kuomba, hakuthubutu hata kutazama juu mbinguni. Alijipigapiga kifua chake akijinyenyekeza mbele za Mungu. Akasema, ‘Ee Mungu, unihurumie, mimi ni mwenye dhambi.’ 14 Ninawaambia, mtu huyu alipomaliza kuomba na kwenda nyumbani, alikuwa amepatana na Mungu. Lakini Farisayo, aliyejisikia kuwa bora kuliko wengine, hakuwa amepatana na Mungu. Watu wanaojikweza watashushwa. Lakini wale wanaojishusha watakwezwa.”
© 2017 Bible League International