Mathayo 6
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa
6 Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.
2 Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.[a] Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. 3 Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.[b] 4 Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Lk 11:2-4)
5 Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. 6 Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.
7 Na unapoomba usiwe kama watu wasiomjua Mungu. Wao kila wanapoomba wanarudia maneno yale yale, tena na tena, wakidhani kuwa wanapoyarudia maneno hayo mara nyingi watasikiwa na Mungu na kujibiwa maombi yao. 8 Msiwe kama wao. Baba yenu anajua yale mnayohitaji kabla hamjamwomba. 9 Hivyo, hivi ndivyo mnapaswa kuomba:
‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako lipewe utukufu.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike hapa dunia,
kama yanavyofanyika huko mbinguni.
11 Utupe leo chakula tunachohitaji.
12 Utusamehe dhambi zetu,
kama tunavyowasamehe wale wanaotukosea.
13 Usiruhusu tukajaribiwa,
lakini utuokoe na Yule Mwovu.’[c]
14 Mkiwasemehe wengine makosa waliyowatendea, Baba yenu wa mbinguni naye atawasamehe makosa yenu pia. 15 Lakini msipowasamehe wengine, Baba Yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi.
Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga
16 Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. 17 Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, 18 ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Huwezi Kuwatumikia Mabwana Wawili
(Lk 12:33-34; 11:34-36; 16:13)
19 Msijiwekee hazina hapa duniani, mahali nondo na kutu[d] huiharibu. Na wezi wanaweza kuvunja nyumba yako na kuziiba. 20 Badala yake jiwekeeni hazina mbinguni ambako haziwezi kuharibiwa na nondo wala kutu na ambako wezi hawawezi kuvunja na kuziiba. 21 Kwa kuwa roho yako itakuwa mahali ilipo hazina yako.
22 Jinsi unavyowaangalia watu wengine ndivyo inavyoonyesha jinsi wewe mwenyewe ulivyo ndani yako. Ukiwaangalia watu kwa nia njema utajawa na nuru ndani yako. 23 Lakini ukiwaangalia watu kwa nia mbaya, utajawa na giza ndani yako. Na ikiwa yote yanayoonekana ndani yako ni giza peke yake, basi unalo giza baya zaidi![e]
24 Hamwezi kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Mtamchukia mmoja na kumpenda yule mwingine au mtakuwa waaminifu kwa mmoja na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na pesa.[f]
Utangulizeni Kwanza Ufalme wa Mungu
(Lk 12:22-34)
25 Kwa hiyo ninawaambia, msiyahangaikie mahitaji ya mwili; mtakula nini, mtakunywa nini au mtavaa nini. Uhai ni zaidi ya chakula na mavazi. 26 Waangalieni ndege wa angani. Hawapandi, hawavuni wala kutunza chakula ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, hamjui kuwa ninyi mna thamani zaidi ya ndege? 27 Hamwezi kujiongezea muda wa kuishi kwa kujisumbua.
28 Na kwa nini mna wasiwasi kuhusu mavazi? Yaangalieni maua ya kondeni. Yatazameni namna yanavyomea. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. 29 Lakini ninawaambia kuwa hata Suleimani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya maua haya. 30 Ikiwa Mungu anayafanya majani yanayoota mashambani kuwa mazuri mnafikiri atawafanyia ninyi kitu gani? Hayo ni majani tu, siku moja yako hai na siku inayofuata hutupwa katika moto. Lakini Mungu anajali kiasi cha kuyafanya kuwa mazuri ya kupendeza. Muwe na hakika basi atawapa ninyi mavazi mnayohitaji. Imani yenu ni ndogo sana!
31 Msijisumbue na kusema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Haya ndiyo mambo ambayo watu wasiomjua Mungu huyawazia daima. Msiwe na wasiwasi, kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnayahitaji haya yote. 33 Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na mambo yote ambayo Mungu anahesabu kuwa ni mema na yenye haki. Ndipo Mungu atakapowapa yote mnayohitaji. 34 Msiisumbukie kesho. Kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Kila siku ina mahangaiko yake ya kutosha.
Footnotes
- 6:2 makusanyiko Au “masinagogi”.
- 6:3 asijue unachofanya Kwa maana ya kawaida, “Mkono wako wa kushoto usijue kile ambacho mkono wako wa kushoto unafanya.”
- 6:13 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza: “Kwa kuwa ufalme na nguvu na utukufu ni vyako milele na milele. Amina.”
- 6:19 nondo na kutu Pia katika mstari wa 20.
- 6:22-23 Kwa maana ya kawaida, 22 Taa ya mwili ni jicho. Hivyo, jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru tele. 23 Lakini jicho lako likiwa na uovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Hivyo ikiwa nuru ndani yako ni giza, giza hilo ni linatisha.
- 6:24 pesa Au “mamona”, neno la Kiaramu linalomaanisha “utajiri”.
Mathayo 7-13
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Iweni Waangalifu Mnapokosoa Wengine
(Lk 6:37-38,41-42)
7 Msiwahukumu wengine, ili Mungu asiwahukumu ninyi pia. 2 Mtahukumiwa jinsi ile ile mnavyowahukumu wengine. Mungu atawatendea kama mnavyowatendea wengine.
3 Kwa nini unaona vumbi iliyo katika jicho la rafiki yako, na hujali kipande cha mti kilicho katika jicho lako? 4 Kwa nini unamwambia rafiki yako, ‘Ngoja nitoe vumbi lililo katika jicho lako wakati wewe mwenyewe bado una kipande cha mti katika jicho lako?’ 5 Ewe mnafiki! Ondoa kwanza kipande cha mti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utaweza kuona vizuri na kutoa vumbi katika jicho la rafiki yako.
6 Msiwape mbwa kitu kitakatifu, watawageuka na kuwadhuru. Na msiwatupie nguruwe lulu zenu kwa kuwa watazikanyaga tu.
Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji
(Lk 11:9-13)
7 Endeleeni kumwomba Mungu, naye atawapa, endeleeni kutafuta nanyi mtapata, endeleeni kubisha nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Ndiyo, yeyote anayeendelea kuomba atapokea. Yeyote anayeendelea kutafuta atapata. Na yeyote anayeendelea kubisha atafunguliwa mlango.
9 Ni nani kati yenu aliye na mwana ambaye akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au akimwomba samaki, atampa nyoka? Bila shaka hakuna! 11 Ijapokuwa ninyi watu ni waovu, lakini bado mnajua kuwapa vitu vyema watoto wenu. Hakika Baba yenu wa mbinguni atawapa vitu vyema wale wamwombao.
Kanuni ya Muhimu Sana
12 Watendee wengine kama ambavyo wewe ungetaka wao wakutendee. Hii ndiyo tafsiri ya torati[a] na mafundisho ya manabii.
Wachache tu Ndiyo Huiona Njia ya Uzima
(Lk 13:24)
13 Unapaswa kuingia katika uzima wa kweli kupitia lango lililo jembamba. Kwa kuwa lango ni pana na njia inayoelekea katika uharibifu nayo ni pana na watu wengi wanaifuata njia hiyo. 14 Lakini lango la kuelekea katika uzima wa kweli ni jembamba. Na njia iendayo huko ni ngumu kuifuata. Na ni watu wachache wanaoiona.
Kile Wanachokifanya watu Kinadhihirisha jinsi gani Walivyo
(Lk 6:43-44; 13:25-27)
15 Mjihadhari na manabii wa uongo wanaokuja kwenu wakijifanya kondoo wasio na madhara ingawa ni watu hatari kama mbwa mwitu. 16 Mtawatambua watu hawa kwa matendo yao. Mambo mazuri hayatoki kwa watu wabaya, kama ambavyo zabibu haitokani na miiba, na tini hazitokani na mbigiri. 17 Vile vile, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, na wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto. 20 Mtawatambua manabii hawa wa uongo kwa matendo yao.
21 Si kila aniitaye Bwana ataingia katika ufalme wa Mungu. Watakaoingia ni wale tu wafanyao yale ambayo Baba yangu wa mbinguni anataka. 22 Siku ya mwisho wengi wataniiita Bwana. Watasema, ‘Bwana, kwa nguvu za jina lako tulihubiri. Na kwa nguvu za jina lako tulitoa mashetani na kufanya miujiza mingi.’ 23 Ndipo nitawaambia waziwazi, ‘Ondokeni kwangu, ninyi waovu. Sikuwahi kuwajua.’
Aina Mbili za Watu
(Lk 6:47-49)
24 Kila anayeyasikia mafundisho yangu na kuyatii ni kama mwenye hekima aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko yakaja, na upepo ukavuma sana, na kuipiga sana nyumba yake. Lakini, nyumba yake haikuanguka kwa sababu ilijengwa kwenye mwamba.
26 Lakini kila anayeyasikia mafundisho yangu na asiyatii ni kama mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko kuja, na upepo ukavuma sana, nyumba yake ilianguka kwa kishindo kikuu.”
28 Yesu alipomaliza kufundisha, watu walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. 29 Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[b]
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mk 1:40-45; Lk 5:12-16)
8 Yesu alipotelemka kutoka kwenye kilima, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 2 Mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea, akainama mbele yake mpaka chini na akasema, “Bwana ukitaka una uwezo wa kuniponya.”
3 Yesu aliunyoosha mkono wake akamshika mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Akasema, “Hakika, ninataka kukuponya. Upone!” Mtu huyo akapona ugonjwa mbaya sana wa ngozi saa hiyo hiyo. 4 Kisha Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea, lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.[c] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”
Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi
(Lk 7:1-10; Yh 4:43-54)
5 Yesu alikwenda Kapernaumu. Alipoingia mjini, afisa wa jeshi alimjia na kumwomba msaada. 6 Akasema, “Bwana, mtumishi wangu ni mgonjwa sana nyumbani na amelala kitandani. Hawezi hata kutingishika na ana maumivu makali sana.”
7 Yesu akamwambia yule afisa, “Nitakwenda nimponye.”
8 Yule afisa akajibu, “Bwana, mimi si mwema kiasi cha wewe kuingia katika nyumba yangu. Toa amri tu, na mtumishi wangu atapona. 9 Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”
10 Yesu aliposikia maneno hayo alishangaa. Akawaambia wale waliokuwa wakifuatana naye, “Ukweli ni kuwa, mtu huyu ana imani kuliko mtu yeyote niliyewahi kumwona katika Israeli. 11 Watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi na kula pamoja na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo katika ufalme wa Mungu. 12 Na wale wanaopaswa kuwa katika ufalme watatupwa nje gizani. Na huko watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”
13 Kisha Yesu akamwambia yule afisa, “Rudi nyumbani kwako. Mtumishi wako atapona kama unavyoamini.” Mtumishi wa afisa huyo akapona wakati ule ule.
Yesu Awaponya Watu Wengi
(Mk 1:29-34; Lk 4:38-41)
14 Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa na homa. 15 Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, kisha akasimama na kuanza kumhudumia.
16 Ilipofika jioni, watu wengi waliokaliwa na mashetani waliletwa kwa Yesu. Naye aliyaamuru mashetani hayo kuwaacha watu. Na aliowaponya wagonjwa wote. 17 Hii ilitokea ili kutimiza maneno yaliyosemwa na nabii Isaya aliposema:
“Aliyaondoa magonjwa yetu
na kuyabeba madhaifu yetu.”(A)
Kumfuata Yesu
(Lk 9:57-62)
18 Yesu alipoona kundi la watu waliomzunguka, aliawaambia wafuasi waende upande mwingine wa ziwa. 19 Kisha, mwalimu wa sheria ya Musa akamwendea na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kila mahali utakapokwenda.”
20 Yesu akamwambia, “Mbweha wana mashimo wanamoishi, ndege wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kupumzika.”
21 Mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana mimi pia nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate mimi, na uwaache wale waliokufa wawazike wafu wao.”
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mk 4:35-41; Lk 8:22-25)
23 Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake. 24 Baada ya mashua kutoka pwani, upepo wenye nguvu sana ukaanza kuvuma ziwani. Mawimbi yakaifunika mashua. Lakini Yesu alikuwa amelala. 25 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha. Wakamwambia, “Bwana tuokoe! Tutazama majini!”
26 Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Hamna imani ya kutosha.” Yesu akasimama akaukemea upepo na mawimbi, na ziwa likatulia.
27 Wanafunzi wake wakashangaa sana, wakasema, “Huyu ni mtu wa namna gani? Hata upepo na maji vinamtii!”
Yesu Afukuza Mashetani Kutoka Kwa Watu Wawili
(Mk 5:1-20; Lk 8:26-39)
28 Yesu alifika ng'ambo ya ziwa katika nchi walimoishi Wagadarini.[d] Hapo wanaume wawili waliokuwa na mashetani ndani yao na kuishi makaburini walimwijia Yesu. Watu hao walikuwa hatari sana na watu hawakuitumia njia iliyopita karibu na makaburi yale. 29 Wakapaza sauti na akasema, “Unataka nini kwetu, Mwana wa Mungu? Umekuja kutuadhibu kabla ya wakati uliopangwa?”
30 Mbali kidogo na mahali hapo lilikuwepo kundi la nguruwe waliokuwa wanapata malisho yao. 31 Mashetani yakamsihi Yesu yakasema, “Ikiwa utatufukuza kutoka ndani ya watu hawa, tafadhali tuache tuwaingie wale nguruwe.”
32 Ndipo akawaamuru na akasema, “Nendeni!” Wale mashetani wakatoka ndani ya wale watu na kuwaingia nguruwe. Kisha kundi lote la nguruwe likaporomoka ziwani na nguruwe wote wakazama na kufa. 33 Wachungaji waliokuwa wakiwachunga wale nguruwe wakakimbia. Wakaenda mjini na kuwaambia watu kila kitu kilichotukia, hasa juu ya wanaume wale wawili waliokuwa na mashetani. 34 Kisha watu wote mjini walikwenda kumwona Yesu. Walipomwona, walimsihi aondoke katika eneo lao.
Yesu Amponya Aliyepooza
(Mk 2:1-12; Lk 5:17-26)
9 Yesu akapanda katika mashua na akasafiri kwa kukatisha ziwa kurudi kwenye mji wake. 2 Baadhi ya watu wakamletea mtu aliyepooza akiwa amelala kwenye machela. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Changamka mtoto wangu! Dhambi zako zimesamehewa.”
3 Baadhi ya walimu wa sheria walisikia alichosema Yesu. Wakaambizana wao kwa wao, “Si anamtukana Mungu mtu huyu akasema hivyo!”
4 Yesu alipotambua walichokuwa wanafikiri, akasema, “Kwa nini mna mawazo maovu kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? 5 Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kitanda chako na utembee’? 6 Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kitanda chako uende nyumbani!’”
7 Mtu yule akasimama na kwenda nyumbani. 8 Watu walipoliona tukio hili wakashangaa. Wakamsifu Mungu kwa kuwapa watu mamlaka hii.
Mathayo Amfuata Yesu
(Mk 2:13-17; Lk 5:27-32)
9 Yesu alipokuwa anaondoka, alimwona mtu aliyeitwa Mathayo amekaa mahali pa kukusanyia ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Hivyo Mathayo akasimama na kumfuata Yesu.
10 Baadaye Yesu alikula chakula nyumbani kwa Mathayo. Watoza ushuru wengi na watu wenye sifa mbaya walikuja na kula chakula pamoja na Yesu pamoja na wafuasi wake. 11 Mafarisayo walipoona kuwa Yesu anakula pamoja na watu hao, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”
12 Yesu alipowasikia wakisema hili, akawaambia, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari si wenye afya. 13 Nendeni mkajifunze andiko hili linamaanisha nini: ‘Sihitaji dhabihu ya mnyama; Ninataka ninyi mwoneshe wema kwa watu.’(B) Sikuja kuwaalika wema kujiunga nami, bali wenye dhambi.”
Swali Kuhusu Kufunga
(Mk 2:18-22; Lk 5:33-39)
14 Kisha wafuasi wa Yohana wakamjia Yesu na kusema, “Sisi na Mafarisayo tunafunga mara kwa mara, lakini wafuasi wako hawafungi. Kwa nini?”
15 Yesu akajibu, “Kwenye harusi marafiki wa bwana harusi hawana huzuni anapokuwa pamoja nao, hivyo hawawezi kufunga. Lakini wakati unakuja ambao bwana harusi ataondolewa kwao. Ndipo watakuwa na huzuni kisha watafunga.
16 Mtu anaposhona kiraka kwenye vazi la zamani, atatumia kiraka chakavu. Akitumia kiraka kipya vazi lake litachanika kwa sababu ya kusinyaa kwa kiraka hicho kipya. Kisha tundu litakuwa baya zaidi. 17 Pia, watu hawawaweki divai mpya kwenye viriba[e] vya zamani. Wakifanya hivyo viriba vitapasuka, na divai itamwagika na viriba vitaharibika. Daima watu huweka divai mpya katika viriba vipya, ambavyo haviwezi kupasuka, na divai huwa salama.”
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mk 5:21-43; Lk 8:40-56)
18 Yesu alipokuwa bado anaongea, kiongozi wa sinagogi akamwendea. Kiongozi akainama chini mbele yake na akasema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini ikiwa utakuja na kumgusa kwa mkono wako, atafufuka.”
19 Hivyo Yesu na wafuasi wake wakaenda na mtu huyo.
20 Wakiwa njiani, alikuwepo mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili. Alimwendea Yesu kwa nyuma na akagusa sehemu ya chini ya vazi lake. 21 Aliwaza, “Ikiwa nitagusa tu joho lake, nitapona.”
22 Yesu aligeuka na kumwona mwanamke. Akasema, “Uwe na furaha, mwanamke. Imani yako imekuponya.” Kisha yule mwanamke akapona saa ile ile.
23 Yesu aliendelea kwenda na kiongozi wa Kiyahudi na kuingia nyumbani kwake. Aliwaona watu wapigao muziki kwa ajili ya mazishi pale. Na aliliona kundi la watu waliohuzunika sana. 24 Yesu akasema, “Ondokeni. Msichana hajafa. Amelala tu.” Lakini watu wakamcheka. 25 Baada ya watu kutolewa nje ya nyumba, Yesu aliingia kwenye chumba cha msichana. Aliushika mkono wa msichana na msichana akasimama. 26 Habari kuhusu jambo hili ilienea kila mahali katika eneo lile.
Yesu Awaponya Watu Watatu
27 Yesu alipokuwa anaondoka kutoka pale, wasiyeona wawili walimfuata. Walisema kwa sauti, “Mwana wa Daudi, uwe mwema kwetu.”
28 Baada ya Yesu kuingia ndani, wasiyeona wakamwendea. Akawauliza, “Mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone?” Wakajibu, “Ndiyo, Bwana, tunaamini.”
29 Kisha Yesu akayagusa macho yao na akasema, “Kwa kuwa mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone, hivyo itatokea.” 30 Ndipo wakaweza kuona. Yesu akawaonya kwa nguvu. Akasema, “Msimwambie yeyote kuhusu hili.” 31 Lakini waliondoka na kutawanya habari kuhusu Yesu kila mahali katika eneo lile.
32 Watu hawa wawili walipokuwa wanaondoka, baadhi ya watu walimleta mtu mwingine kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa haongei kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. 33 Yesu akamtoa nje pepo na mtu yule aliweza kuongea. Watu walishangaa na akasema, “Hakuna mtu yeyote aliyewahi kuona kitu kama hiki katika Israeli.”
34 Lakini Mafarisayo walisema, “Mtawala wa mashetani ndiye anayempa nguvu ya kuyatoa mashetani.”
Mwombeni Mungu Atume Watenda Kazi Zaidi
35 Yesu alisafiri akipita katika miji yote na vijiji. Alifundisha katika masinagogi yao na kuwaeleza watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Aliponya kila aina ya magonjwa na udhaifu. 36 Yesu aliona watu wengi na kuwahurumia kwa sababu walikuwa wanakandamizwa na hawakuwa na tumaini; kama kondoo bila mchungaji wa kuwaongoza. 37 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kuna mavuno mengi ya watu ya kuleta. Lakini kuna wafanyakazi wachache wa kusaidia kuwavuna. 38 Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni atume wafanyakazi wengi zaidi wa kusaidia kukusanya mavuno yake.”
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mk 3:13-19; 6:7-13; Lk 6:12-16; 9:1-6)
10 Yesu aliwaita pamoja wafuasi wake kumi na mbili. Akawapa uwezo juu ya pepo wabaya ili waweze kuwafukuza na pia kuponya kila aina ya magonjwa na maradhi. 2 Haya ni majina ya mitume kumi na wawili:
Simoni (ambaye pia aliitwa Petro),
Andrea, kaka yake Petro,
Yakobo, mwana wa Zebedayo,
Yohana, kaka yake Yakobo,
3 Filipo,
Bartholomayo,
Thomaso,
Mathayo, mtoza ushuru,
Yakobo, mwana wa Alfayo,
Thadayo,
4 Simoni Mzelote,
Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu).
5 Yesu aliwatuma mitume hawa kumi na wawili pamoja na maelekezo haya: “Msiende kwa watu wasio Wayahudi. Na msiingie katika miji ambako Wasamaria wanaishi. 6 Lakini nendeni kwa watu wa Israeli. Wako kama kondoo waliopotea. 7 Mtakapokwenda, waambieni hivi: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’ 8 Waponyeni wagonjwa. Fufueni waliokufa. Waponyeni watu wenye magonjwa mabaya sana ya ngozi. Na toeni mashetani kwa watu. Ninawapa nguvu hii bure, hivyo wasaidieni wengine bure. 9 Msibebe pesa pamoja nanyi; dhahabu au fedha au shaba nyekundu. 10 Msibebe mikoba. Chukueni nguo na viatu mlivyovaa tu. Na msichukue fimbo ya kutembelea. Mfanyakazi anastahili kupewa anachohitaji.
11 Mnapoingia katika mji, tafuteni kwa makini hadi mumpate mtu anayefaa na mkae katika nyumba yake mpaka mtakapoondoka mjini. 12 Mtakapoingia katika nyumba hiyo, semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ 13 Ikiwa watu katika nyumba hiyo watawakaribisha, wanastahili amani yenu. Wapate amani mliyowatakia. Lakini ikiwa hawatawakaribisha, hawastahili amani yenu. Ichukueni amani mliyowatakia. 14 Na ikiwa watu katika nyumba au mji watakataa kuwapokea au kuwasikiliza, basi ondokeni mahali hapo na mkung'ute mavumbi kutoka katika miguu yenu. 15 Ninaweza kuwathibitishia kuwa siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa mji huo kuliko watu wa Sodoma na Gomora.[f]
Yesu Aonya Kuhusu Matatizo
(Mk 13:9-13; Lk 21:12-17)
16 Sikilizeni! Ninawatuma, nanyi mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Hivyo muwe na akili kama nyoka. Lakini pia muwe kama njiwa na msimdhuru yeyote. 17 Muwe waangalifu! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka ili kuwashitaki mbele ya mabaraza ya mijini. Watawachapa ndani ya masinagogi yao. 18 Mtasimamishwa mbele ya magavana na wafalme. Watu watawafanyia ninyi hivi kwa sababu mnanifuata. Mtakuwa mashahidi wangu mbele za wafalme na magavana hao na kwa watu wa mataifa mengine. 19 Mtakapokamatwa, msisumbuke kuhusu nini mtakachosema au namna gani mtakavyosema. Katika wakati huo mtapewa maneno ya kusema. 20 Si ninyi mtakaoongea; Roho wa Baba Mungu wenu atakuwa anaongea kupitia ninyi.
21 Ndugu watakuwa kinyume cha ndugu zao wenyewe na kuwapeleka kwenda kuuawa. Baba watawapeleka watoto wao wenyewe kuuawa. Watoto watapigana kinyume na wazazi wao na watawapeleka kuuawa. 22 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 23 Mnapotendewa vibaya katika mji mmoja, nendeni katika mji mwingine. Ninawaahidi kuwa hamtamaliza kwenda katika miji ya Israeli kabla Mwana wa Adamu hajarudi.
24 Wanafunzi si wazuri kuliko mwalimu wao. Watumwa si wazuri kuliko bwana wao. 25 Inatosha kwa wanafunzi kuwa kama walimu wao na watumwa kuwa kama bwana wao. Iwapo watu hao wananiita ‘mtawala wa pepo’, na mimi ni kiongozi wa familia, basi ni dhahiri kwa kiasi gani watawatukana ninyi, mlio familia yangu!
Mwogopeni Mungu, Siyo Watu
(Lk 12:2-7)
26 Hivyo msiwagope watu hao. Kila kitu kilichofichwa kitaoneshwa. Kila kilicho siri kitajulikana. 27 Ninayowaambia ninyi faraghani myaseme hadharani. Kila ninachowanong'oneza nawataka mkiseme kwa sauti kila mtu asikie.
28 Msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Mnapaswa kumwogopa Mungu, anayeweza kuuharibu mwili na roho jehanamu. 29 Ndege wanapouzwa, ndege wawili wadogo hugharimu senti moja tu. Lakini hakuna hata mmoja wa ndege hao wadogo anaweza kufa bila Baba yenu kufahamu. 30 Mungu anafahamu idadi ya nywele katika vichwa vyenu. 31 Hivyo msiogope. Mna thamani kuliko kundi kubwa la ndege.
Msiionee Haya Imani Yenu
(Lk 12:8-9)
32 Iwapo mtawaambia watu wengine kuwa mnaniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi ni wangu. 33 Lakini ikiwa mtasimama mbele ya wengine na kusema kuwa hamniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi si wangu.
Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo
(Lk 12:51-53; 14:26-27)
34 Msidhani kuwa nilikuja duniani kuleta amani. Sikuja kuleta amani. Nilikuja kuleta vita. 35 Nimekuja ili hili litokee:
‘Mwana atamgeuka baba yake.
Binti atamgeuka mama yake.
Binti mkwe atamgeuka mama mkwe wake.
36 Hata watu wa familia zenu watakuwa adui zenu.’(C)
37 Wale wanaowapenda baba zao au mama zao kuliko wanavyonipenda mimi hawana thamani kwangu. Na wale wanaowapenda wana wao au binti zao kuliko wanavyonipenda mimi hawastahili kuwa wafuasi wangu. 38 Wale ambao hawataupokea msalaba waliopewa wanaponifuata hawastahili kuwa wanafunzi wangu na kunifuata. 39 Wale wanaojaribu kuyatunza maisha waliyonayo, watayapoteza. Lakini wale wanaoyaacha maisha yao kwa ajili yangu watapata uzima halisi.
Mungu Atawabariki Wanaowakaribisha Ninyi
(Mk 9:41)
40 Yeyote anayewakubali ninyi ananikubali mimi. Na yeyote anayenikubali anamkubali yule aliyenituma. 41 Yeyote anayemkubali nabii kwa sababu ni nabii atapata ujira wa nabii. Na yeyote anayemkubali mwenye haki kwa sababu ni mwenye haki atapata ujira anaoupata mwenye haki. 42 Yeyote anayemsaidia mmoja wa wafuasi wangu hawa wanyenyekevu kwa sababu ni wafuasi wangu hakika atapata ujira, hata ikiwa wanawapa tu kikombe cha maji baridi.”
Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali
(Lk 7:18-35)
11 Yesu alipomaliza maelekezo haya kwa wafuasi wake kumi na wawili wa karibu, aliondoka mahali pale. Akaenda katika miji ya Galilaya kuwafundisha watu na kuwaeleza ujumbe wa Mungu.
2 Yohana alipokuwa gerezani, alisikia kuhusu mambo yaliyokuwa yanatokea; mambo ambayo Masihi angefanya. Hivyo akawatuma baadhi ya wafuasi wake kwa Yesu. 3 Wakamuuliza, “Wewe ni yule tuliyekuwa tunamngojea, au tumsubiri mwingine?”
4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mliyosikia na kuona: 5 Vipofu wanaona. Viwete wanatembea. Watu wenye magonjwa ya ngozi wanaponywa. Wasiyesikia wanasikia. Wafu wanafufuliwa. Na habari njema inahubiriwa kwa maskini. 6 Heri ni kwa wale wasio na shida kunikubali.”
7 Wafuasi wa Yohana walipoondoka, Yesu alianza kuongea na watu kuhusu Yohana. Alisema, “Ninyi watu mlikwenda jangwani kuona nini? Mtu aliye dhaifu, kama unyasi unaoyumbishwa na upepo? 8 Hakika, ni nini mlichotarajia kuona? Aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hivyo. Watu wote wanaovaa mavazi mazuri wanapatikana katika ikulu za wafalme. 9 Hivyo mlitoka kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yeye ni zaidi ya hilo. 10 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:
‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(D)
11 Ukweli ni kuwa Yohana Mbatizaji ni mkuu kuliko yeyote aliyewahi kuja katika ulimwengu huu. Lakini hata mtu asiye wa muhimu katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana. 12 Tangu wakati wa Yohana Mbatizaji ulipokuja mpaka sasa, Ufalme wa Mungu umekabiliwa na mashambulizi. Watu wenye nguvu wamejaribu kuudhibiti ufalme huu.[g] 13 Kabla ya Yohana kuja, Sheria ya Musa na manabii wote wamesema kuhusu mambo ambayo yangetokea. 14 Na ikiwa mnaamini waliyosema, basi Yohana ni Eliya. Ndiye waliyesema angekuja. 15 Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!
16 Ninaweza kusema nini kuhusu watu wanaoishi leo? Watu siku ya leo ni kama watoto wanaokaa katika masoko. Kundi moja la watoto linaliambia kundi lingine,
17 ‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliimba wimbo wa maziko,
lakini hamkuhuzunika.’
18 Kwa nini ninasema watu wako hivyo? Kwa sababu Yohana alikuja na hakula vyakula vya kawaida na kunywa divai, na watu walisema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 19 Mwana wa Adamu amekuja akila na kunywa, na watu husema, ‘Mwangalie! Hula sana na kunywa divai nyingi. Ni rafiki wa wakusanya kodi na wenye dhambi wengine.’ Lakini hekima inaonesha kuwa sahihi kutokana na yale inayotenda.”
Maonyo Kwa Wanaomkataa Yesu
(Lk 10:13-15)
20 Kisha Yesu akaanza kuikosoa miji ambako alifanya miujiza yake mingi. Aliikosoa miji hii kwa sababu watu katika miji hii hawakubadili maisha yao na kuacha kutenda dhambi. 21 Yesu alisema, “Itakuwa vibaya kwako Korazini! Itakuwa vibaya kwako Bethsaida![h] Ikiwa miujiza hii hii ingetokea Tiro na Sidoni,[i] watu huko wangeshabadili maisha yao kitambo. Wangekwishavaa magunia na kujimwagia majivu kuonesha kuwa wanasikitikia dhambi zao. 22 Lakini ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya zaidi kwako kuliko Tiro na Sidoni.
23 Nawe Kapernaumu, utakwezwa mpaka mbinguni? Hapana! Utatupwa chini mpaka Kuzimu. Nimetenda miujiza mingi ndani yako. Iwapo miujiza hii ingetokea Sodoma,[j] watu huko wangeacha kutenda dhambi na ungekuwa bado ni mji hata leo. 24 Lakini ninakuambia, itakuwa vibaya kwako siku ya hukumu kuliko Sodoma.”
Yesu Awapa Pumziko Watu Wake
(Lk 10:21-22)
25 Kisha Yesu akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, Bwana wa mbinguni na duniani. Ninashukuru kwa sababu umeyaficha mambo haya kwa wale wanaofikiri kuwa ni wenye hekima na werevu sana. Lakini umeyaonesha haya kwa watu walio kama watoto wadogo.[k] 26 Ndiyo, Baba, ulifanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulivyotaka kufanya.
27 Baba yangu amenipa kila kitu. Hakuna amjuaye Mwana isipokuwa Baba peke yake. Na hakuna amjuaye Baba isipokuwa Mwana ndiye anayemjua Baba. Na watu pekee watakaomjua Baba ni wale ambao Mwana atachagua kuwaonesha.
28 Njooni kwangu ninyi nyote mliochoka kutokana na mizigo mizito mnayolazimishwa kubeba. Nitawapa pumziko. 29 Chukueni nira yangu,[l] jifunzeni kutoka kwangu. Mimi ni mwema na mnyenyekevu katika roho. Nanyi mtaweza kupumzika. 30 Ndiyo, nira yangu ni rahisi. Mzigo ninaowapa muubebe ni mwepesi.”
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mk 2:23-28; Lk 6:1-5)
12 Katika wakati huo huo, Yesu alikuwa anasafiri akipita katika mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wafuasi wake walikuwa pamoja naye, na walikuwa na njaa. Hivyo walianza kuchuma nafaka na kula. 2 Mafarisayo walioliona hili, wakamwambia Yesu, “Tazama! Wafuasi wako wanafanya kitu ambacho ni kinyume na sheria yetu kufanya katika siku ya Sabato.”
3 Yesu akawaambia, “Mmekwisha soma alichofanya Daudi wakati yeye na wale waliokuwa pamoja naye walipokuwa na njaa. 4 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu. Yeye na wale waliokuwa pamoja naye walikula mkate uliotolewa kwa Mungu. Ilikuwa kinyume cha sheria kwa Daudi au wale waliokuwa pamoja naye kula mkate huo. Makuhani pekee ndio walioruhusiwa kuula. 5 Na mmekwisha soma katika Sheria ya Musa kuwa katika kila Sabato makuhani kwenye Hekalu wanavunja Sheria kwa kufanya kazi Siku ya Sabato. Lakini hawakosei kwa kufanya hivyo. 6 Ninawaambia kuwa kuna kitu hapa ambacho ni kikuu kuliko Hekalu. 7 Maandiko yanasema, ‘Sihitaji dhabihu ya wanyama; Ninataka ninyi muoneshe wema kwa watu.’(E) Hakika hamjui hilo linamaanisha nini. Iwapo mngelielewa, msingewahukumu wale ambao hawajafanya chochote kibaya.
8 Mwana wa Adamu ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mk 3:1-6; Lk 6:6-11)
9 Kutoka hapo Yesu alikwenda katika sinagogi lao. 10 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepooza mkono. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pale walikuwa wanatafuta sababu ya kumshitaki Yesu kwa kutenda kitu kibaya, hivyo walimuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
11 Yesu akajibu, “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo na akatumbukia shimoni siku ya Sabato, utamsaidia kumtoa yule kondoo katika shimo. 12 Hakika mtu ni bora kuliko kondoo. Hivyo ni sawa kutenda wema siku ya Sabato.”
13 Kisha Yesu akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Unyooshe mkono wako.” Mtu yule akaunyoosha mkono wake, na ukawa mzima tena, kama mkono mwingine. 14 Lakini Mafarisayo waliondoka na wakaweka mipango ya kumuua Yesu.
Yesu ni Mtumishi Aliyechaguliwa na Mungu
15 Yesu alitambua kuwa Mafarisayo walikuwa wanapanga kumuua. Hivyo aliondoka mahali pale na watu wengi walimfuata. Akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, 16 lakini aliwaonya wasiwaambie wengine yeye alikuwa nani. 17 Hii ilikuwa ni kuthibitisha kile ambacho nabii Isaya alisema alipozungumza kwa niaba ya Mungu:
18 “Hapa ni mtumishi wangu,
niliyemchagua.
Ndiye ninayempenda,
na ninapendezwa naye.
Nitamjaza Roho yangu,
naye ataleta haki kwa mataifa.
19 Hatabishana au kupiga kelele;
hakuna atakayesikia sauti yake mitaani.
20 Hatavunja wala kupindisha unyasi.
Hatazimisha hata mwanga hafifu.
Hatashindwa mpaka ameifanya haki kuwa mshindi.
21 Watu wote watatumaini katika yeye.”(F)
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mk 3:20-30; Lk 11:14-23; 12:10)
22 Kisha baadhi ya watu wakamleta mtu kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa asiyeona na hakuweza kuzungumza, kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. Yesu akamponya na akaweza kuzungumza na kuona. 23 Watu wote walikishangaa kile Yesu alichotenda. Walisema, “Pengine ni Mwana wa ahadi wa Daudi!”
24 Mafarisayo waliposikia hili, walisema, “Mtu huyu anatumia nguvu za Shetani[m] kufukuza mashetani kutoka kwa watu. Beelzebuli ni mtawala wa mashetani.”
25 Yesu alijua kile Mafarisayo walikuwa wanafikiri. Hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe utateketezwa. Na kila mji au familia iliyogawanyika haiwezi kuishi. 26 Hivyo ikiwa Shetani anayafukuza mashetani[n] yake mwenyewe, anapigana kinyume chake yeye mwenyewe, na ufalme wake hautaishi. 27 Mnasema kuwa ninatumia nguvu za Shetani kuyatoa mashetani. Ikiwa hiyo ni kweli, sasa ni nguvu gani watu wenu hutumia wanapoyafukuza mashetani? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa mmekosea. 28 Lakini ninatumia nguvu ya Roho wa Mungu kuyafukuza mashetani, na hili linaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu. 29 Watu wowote wanaotaka kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuiba vitu vyake lazima wamfunge kwanza. Kisha wanaweza kuiba vitu kutoka katika nyumba yake. 30 Yeyote ambaye hayuko pamoja nami yu kinyume nami. Na yeyote ambaye hakusanyi pamoja nami hutawanya.
31 Hivyo ninawaambia, Mungu atawasamehe watu kila dhambi wanayotenda au kila jambo baya wanalosema kinyume naye. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32 Unaweza kusema kinyume na Mwana wa Adamu na ukasamehewa. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa; si sasa au baadaye.
Yale Unayofanya Yanaonesha Jinsi Ulivyo
(Lk 6:43-45)
33 Ikiwa unataka matunda mazuri, ni lazima uutunze mti vizuri. Ikiwa mti wako siyo mzuri, utakuwa na matunda mabaya. Mti unajulikana kutokana na aina ya matunda inaozalisha. 34 Ninyi nyoka! Ni waovu sana. Mnawezaje mkasema chochote kilicho chema? Kile ambacho watu husema kwa midomo yao kinatoka katika yale yaliyojaa katika mioyo yao. 35 Walio wema wana vitu vizuri vilivyotunzwa katika mioyo yao. Ndiyo maana husema mambo mazuri. Lakini wale walio waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu husema mambo maovu. 36 Ninawaambia kuwa kila mmoja atajibu kwa ajili ya mambo yasiyo ya maana waliyosema. Hili litatokea siku ya hukumu. 37 Maneno yenu yatatumika kuwahukumu ninyi. Uliyosema yataamua ikiwa una haki mbele za Mungu au unahukumiwa na Mungu.”
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-12; Lk 11:29-32)
38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjibu Yesu. Wakasema, “Mwalimu, tunataka kukuona ukifanya miujiza kama ishara kuwa unatoka kwa Mungu.”
39 Yesu akajibu, “Watu wenye dhambi na wasio na imani hutafuta kuona muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika kudhibitisha chochote kwao. Yona[o] ni ishara pekee itakayotolewa kwenu ninyi mlio wa kizazi kiovu cha leo. 40 Yona alikuwa ndani ya tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu, mchana na usiku. Vivyo hivyo, Mwana wa Adamu atakuwa kaburini kwa siku tatu, mchana na usiku. 41 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi leo mtalinganishwa na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha namna mlivyokosea. Kwa nini ninasema hivi? Kwa sababu Yona alipowahubiri watu hao, walibadili maisha yao. Na aliye mkuu kuliko Yona, yupo hapa lakini mnakataa kubadilika!
42 Pia, siku ya hukumu, Malkia wa Kusini[p] atasimama pamoja na wale wanaoishi sasa, atasababisha mhukumiwe kuwa na makosa. Ninasema hivi kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana kuja kusikiliza mafundisho yenye hekima ya Sulemani. Nami Ninawaambia aliye mkuu zaidi ya Sulemani yuko hapa, lakini hamnisikii!
Hatari ya Kuwa Mtupu
(Lk 11:24-26)
43 Roho chafu inapotoka kwa mtu, husafiri katika sehemu kavu ikitafuta mahali pa kupumzika, lakini haipati mahali pa kupumzika. 44 Inapokosa mahali pa kupumzika, husema, ‘Nitarudi katika nyumba niliyotoka.’ Inaporudi, ikakuta nyumba hiyo bado ni tupu, ikiwa safi na nadhifu, 45 hutoka nje na kuleta roho zingine saba zilizo chafu zaidi yake. Huingia na kuishi humo, na mtu huyo anakuwa na matatizo mengi kuliko mwanzo wakati roho chafu moja iliishi ndani yake. Ndivyo ilivyo kwa kizazi hiki cha watu wanaoishi leo.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mk 3:31-35; Lk 8:19-21)
46 Yesu alipokuwa akiongea na watu, mama yake na ndugu zake walikuwa nje. Walitaka kuongea naye. 47 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na wadogo zako wanakusubiri nje. Wanataka kuongea nawe.”
48 Yesu akajibu, “Mama yangu ni nani? Ndugu zangu ni nani?” 49 Kisha akanyoosha kidole kwa wafuasi wake na akasema, “Unaona! Watu hawa ni mama yangu na ndugu zangu. 50 Kaka yangu, dada yangu na mama yangu halisi ni yule afanyaye yale Baba yangu wa mbinguni anataka.”
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mk 4:1-9; Lk 8:4-8)
13 Siku hiyo hiyo Yesu alitoka nje ya nyumba na kukaa kando ya ziwa. 2 Kundi kubwa wakakusanyika kumzunguka. Hivyo akapanda mtumbwini na kuketi. Watu wote wakabaki ufukweni. 3 Kisha Yesu akatumia simulizi kuwafundisha mambo mengi. Akawaambia simulizi hii:
“Mkulima alitoka kwenda kupanda mbegu. 4 Alipokuwa anatawanya mbegu, baadhi ziliangukia njiani. Ndege wakaja na kuzila zote. 5 Mbegu zingine ziliangukia kwenye ardhi yenye mawe, ambako hakukuwa na udongo wa kutosha. Zikakua haraka pale, kwa sababu udongo haukuwa na kina. 6 Lakini jua lilipowaka, likaichoma mimea. Mimea ikafa kwa sababu haikuwa na mizizi mirefu. 7 Baadhi ya mbegu ziliangukia katikati ya miiba. Miiba ikakua na kusababisha mimea mizuri kuacha kukua. 8 Lakini baadhi ya mbegu ziliangukia kwenye udongo wenye rutuba. Hapo zikakua na kuzaa nafaka. Baadhi ya mimea ikazaa nafaka mara mia zaidi, baadhi mara sitini na baadhi mara thelathini zaidi. 9 Ninyi watu mnaoweza kunisikia, nisikilizeni!”
Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha
(Mk 4:10-12; Lk 8:9-10)
10 Wafuasi wake wakamwendea Yesu na kumuuliza, “Kwa nini unatumia simulizi hizi kuwafundisha watu?”
11 Yesu akawajibu, “Mungu amewapa ninyi ujuzi wa kuelewa siri za ufalme wa Mungu, lakini hajawapa watu hawa wengine ujuzi huu. 12 Kisha akawaambia, ‘Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.’ 13 Ndiyo sababu ninatumia simulizi hizi kuwafundisha watu: Wanaona, lakini hakika hawaoni. Wanasikia, lakini hakika hawasikii au kuelewa. 14 Hiyo inathibitisha alichosema nabii Isaya kuhusu wao kuwa kweli:
‘Ninyi watu mtasikia na kusikia,
lakini hamtaelewa.
Mtatazama na kutazama,
lakini hakika hamtaona.
15 Ndiyo, akili za watu hawa sasa zimefungwa.
Wana masikio, lakini hawasikii vizuri.
Wana macho, lakini wameyafumba.
Iwapo akili zao zisingekuwa zimefungwa,
wangeona kwa macho yao;
wangesikia kwa masikio yao;
Iwapo wangeelewa kwa akili zao.
Kisha wangenigeukia na kuponywa.’(G)
16 Bahati gani mliyonayo ninyi. Mnaelewa mnachokiona kwa macho yenu. Na mnaelewa mnachosikia kwa masikio yenu. 17 Ninaweza kuwathibitishia, manabii na watakatifu wengi walitaka kuona mnayoyaona. Lakini hawakuyaona. Walitaka kusikia mnayosikia sasa. Lakini hawakuyasikia.
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mk 4:13-20; Lk 8:11-15)
18 Hivyo sikilizeni maana ya simulizi hiyo kuhusu mkulima:
19 Vipi kuhusu mbegu zilizoangukia njiani? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho kuhusu ufalme wa Mungu lakini hawauelewi. Mwovu huja na kuyachukua yaliyopandwa katika mioyo yao.
20 Na vipi kuhusu mbegu zilizoangukia kwenye udongo wenye mawe? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho haraka na kwa furaha huyapokea. 21 Lakini hawaruhusu mafundisho kutawala maisha yao. Huyatunza kwa muda mfupi. Mara tatizo au mateso yanapokuja kwa sababu ya mafundisho waliyoyapokea, wanaacha kuyafuata.
22 Na vipi kuhusu mbegu zilizoanguka katikati ya miiba? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho lakini huyaruhusu mahangaiko ya maisha na kutaka utajiri, hufanya mafundisho yasikue. Hivyo mafundisho hayazai mazao mazuri katika maisha yao.
23 Lakini vipi kuhusu mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye rutuba? Hizo ni sawa na watu wanaosikia mafundisho na kuyaelewa. Hukua na kuzaa mazao mazuri, wakati mwingine mara mia, wakati mwingine mara sitini, na wakati mwingine mara thelathini zaidi.”
Simulizi Kuhusu Ngano na Magugu
24 Kisha Yesu akatumia simulizi nyingine kuwafundisha. Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25 Usiku ule, kila mtu alipokuwa amelala, adui wa yule mtu akaja na kupanda magugu katikati ya ngano kisha akaondoka. 26 Baadaye, ngano ikakua na vichwa vya nafaka vikaota juu ya mimea. Kisha mtumishi akayaona magugu. 27 Watumwa wa mwenye shamba wakaja na akasema, ‘Bwana ulipanda mimea mizuri kwenye shamba lako. Magugu yametoka wapi?’
28 Yule mtu akajibu, ‘Adui alipanda magugu.’
Wale watumwa wakauliza, ‘Je, unataka twende na kung'oa magugu?’
29 Akajibu, ‘Hapana, kwa sababu mtakapokuwa mnang'oa magugu, mtaweza pia kung'oa ngano. 30 Yaacheni magugu na ngano vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati wa mavuno nitawaambia wafanyakazi hivi: Kwanza, yakusanyeni magugu na kuyafunga pamoja ili myachome. Kisha kusanyeni ngano na kuileta ghalani mwangu.’”
Simulizi Nyingine ya Ufalme
(Mk 4:30-34; Lk 13:18-21)
31 Kisha Yesu akawaambia watu simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na mbegu ya mharadali ambayo mtu alipanda katika shamba lake. 32 Ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote. Lakini unapokua, ni kubwa kuliko mimea yote ya bustanini. Unakuwa mti mkubwa unaotosha ndege kuja na kutengeneza viota kwenye matawi yake.”
33 Kisha Yesu akawaambia simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na chachu ambayo mwanamke huichanganya katika bakuli kubwa la unga ili atengeneze mkate. Chachu hufanya kinyunya chote kiumuke.”
34 Yesu alitumia simulizi akasema mambo yote haya kwa watu. Daima alitumia simulizi kuwafundisha. 35 Hii ilikuwa kuweka wazi maana halisi kama manabii walivyosema:
“Nitazungumza kwa kutumia simulizi;
Nitayasema mambo ambayo yamekuwa siri
tangu ulimwengu ulipoumbwa.”(H)
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Magugu
36 Kisha Yesu akawaacha watu na kuingia katika nyumba. Wafuasi wake wakamwendea na akasema, “Tufafanulie maana ya simulizi kuhusu magugu ndani ya shamba.”
37 Akajibu, “Mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba ni Mwana wa Adamu. 38 Shamba ni ulimwengu. Mbegu nzuri ni watoto katika ufalme wa Mungu. Magugu ni watu wa Yule Mwovu. 39 Na adui aliyepanda mbegu mbaya ni ibilisi. Mwisho wa nyakati ndiyo wakati wa mavuno. Wafanyakazi wanaokusanya ni malaika wa Mungu.
40 Magugu hung'olewa na kuchomwa motoni. Itakuwa vivyo hivyo nyakati za mwisho. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watawatafuta watu wanaosababisha dhambi na wale wote watendao maovu. Malaika watawatoa watu hao katika ufalme wa Mungu. 42 Watawatupia katika tanuru la moto. Huko watu watakuwa wakilia na kusaga meno kwa maumivu. 43 Kisha wenye haki watang'aa kama jua. Watakuwa katika ufalme wa baba yao. Ninyi watu, mlio na masikio, sikilizeni!
Simulizi Kuhusu Hazina na Lulu
44 Ufalme wa Mungu unafanana na hazina iliyofichwa shambani. Siku moja mtu alipoiona aliificha tena; na kwa sababu alikuwa na furaha sana alikwenda kuuza kila kitu alichonacho na kulinunua shamba.
45 Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mchuuzi anayetafuta lulu safi. 46 Siku moja alipoipata, alikwenda na akauza kila kitu alichokuwa nacho ili kuinunua.
Simulizi Kuhusu Wavu wa Kuvulia Samaki
47 Pia, ufalme wa Mungu unafanana na nyavu kubwa iliyowekwa katika ziwa. Nyavu ile ikavua aina nyingi tofauti ya samaki. 48 Ikajaa, hivyo wavuvi wakaivuta mpaka pwani. Wakakaa chini na kutoa samaki wote wazuri na kuwaweka kwenye kikapu. Kisha wakawatupa samaki wabaya. 49 Itakuwa hivyo wakati wa mwisho. Malaika watakuja na kuwatenganisha waovu na watakatifu. 50 Watawatupa waovu katika tanuru la moto. Huko watu watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”
51 Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Mnaelewa mambo yote haya?”
Wakasema, “Ndiyo, tunaelewa.”
52 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivyo kila mwalimu wa sheria aliyejifunza kuhusu ufalme wa Mungu ana baadhi ya vitu vizuri vya kufundisha. Ni kama mmiliki wa nyumba, aliye na vitu vipya na vya zamani nyumbani mwake. Na huvitoa nje vipya na vya zamani.”
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mk 6:1-6; Lk 4:16-30)
53 Yesu alipomaliza kufundisha kwa simulizi hizi, aliondoka pale. 54 Alikwenda katika mji wa kwao. Aliwafundisha watu katika sinagogi lao, nao walishangaa. Walisema, “Mtu huyu alipata wapi hekima na nguvu hii ya kutenda miujiza? 55 Je, yeye si mwana wa seremala tunayemfahamu? Je, jina la mamaye si Mariamu na wadogo zake ni Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake bado wanaishi hapa katika mji huu? Anawezaje kutenda mambo haya?” 57 Hivyo wakawa na mashaka kumpokea.
Lakini Yesu akawaambia, “Watu kila mahali huwaheshimu manabii, lakini katika mji wake au katika nyumba yake nabii hapati heshima yoyote.” 58 Yesu hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu watu hawakumwamini.
Footnotes
- 7:12 torati Au “Sheria ya Musa”.
- 7:29 mamlaka Hakuhitaji mamlaka yoyote zaidi ya kwake. Kinyume chake waandishi daima waliwanukuu walimu wa kale wa Kiyahudi kama mamlaka ya mafundisho yao.
- 8:4 kuhani akakuchunguze Sheria ya Musa (torati) ilisema kuhani ni lazima aamue ikiwa mtu amepona ukoma.
- 8:28 Wagadarini Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagerasi” na zingine zina “Wagergesini”.
- 9:17 viriba Kibuyu au chombo cha kuhifadhia divai au maji kilichotengenezwa kwa ngozi.
- 10:15 Sodoma na Gomora Miji ambayo Mungu aliiangamiza kwa sababu watu waliokuwa wakiishi pale walikuwa waovu sana. Tazama Mwa 19.
- 11:12 Herode Antipa alimkamata na kisha kumwua Yohana Mbatizaji na pia alijaribu kumzuia Yesu na wanafunzi wake kwa nguvu. Tazama Herode katika Orodha ya Maneno.
- 11:21 Korazini, Bethsaida Miji ya Kiyahudi iliyokuwa kando kando mwa Ziwa Galilaya ambapo Yesu alifanya miujiza mingi kudhihirisha mamlaka yake yanayotoka kwa Mungu. Pamoja na hili, watu walikataa kubadili maisha waliyoishi yasiyokuwa na Mungu.
- 11:21 Tiro na Sidoni Miji iliyojaa ibada ya sanamu ambayo ilijulikana sana kwa uovu uliokuwemo humo.
- 11:23 Sodoma Mji ambao Mungu aliuangamiza, pamoja na Jiji la Gomora, kwa sababu watu walioishi walikuwa waovu sana. Tazama Mwa 19.
- 11:25 kama watoto wadogo Maana wale ambao hawajaenda shule bado.
- 11:29 nira yangu Nira iliwekwa shingoni mwa mnyama anayefanya kazi ili kuvuta mzigo. Ilikuwa pia ni alama ya Kiyahudi kwa sheria. Tazama Mdo 15:10; Gal 5:1. Ilikuwa pia alama ya kutawaliwa na taifa katili la kigeni, kama vile Ufalme wa Rumi.
- 12:24 Shetani Jina la Mwovu lenye maana “Adui”. Kwa maana ya kawaida, “Beelzebuli” kwa Kiyunani (mwovu). Pia katika mstari wa 27.
- 12:26 ikiwa Shetani … mashetani Kwa maana ya kawaida, “ikiwa Shetani atamfukuza Shetani.”
- 12:39 Yona Au “Nabii Yona”, nabii katika Agano la Kale. Baada ya kukaa katika tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu alitoka akiwa mzima, kisha akaenda kwenye mji uliojaa uovu wa Ninawi kuwaonya watu huko kama alivyotumwa na Mungu. Kwa njia hiyo hiyo, Yesu angetoka kaburini siku ya tatu, ishara ya kuthibitisha ukweli wa ujumbe wake kutoka kwa Mungu.
- 12:42 Malkia wa Kusini Au “Malkia wa Sheba.” Alisafiri kama maili 1,000 (kilomita 1,600) ili kujifunza hekima ya Mungu kutoka kwa Sulemani. Tazama 1 Fal 10:1-13.
© 2017 Bible League International