Revised Common Lectionary (Complementary)
Mwanakondoo Afungua Kitabu
6 Kisha nilitazama Mwanakondoo alipokuwa anaufungua muhuri[a] wa kwanza kati ya mihuri saba. Kisha nikasikia sauti ya mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akisema kwa sauti kama ngurumo ya radi ikisema, “Njoo!” 2 Nilipotazama nilimwona farasi mweupe mbele yangu. Mwendesha farasi aliyekuwa amempanda farasi huyo alikuwa na upinde na alipewa taji. Alimwendesha farasi akatoka kwenda kumshinda adui na ili kupata ushindi.
3 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa pili, nilimsikia kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” 4 Nilipotazama nilimwona farasi mwekundu akitokea. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alipewa mamlaka ya kuondoa amani duniani ili watu wauane. Alipewa upanga mkubwa.
5 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tatu. Nilisikia kiumbe mwenye uhai wa tatu akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mweusi mbele yangu. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alikuwa na mizani mkononi mwake. 6 Kisha nilisikia kitu kilichosikika kama sauti ikitokea pale walipokuwa viumbe wenye uhai wanne. Kikisema, “Kilo moja[b] ya ngano au kilo tatu ya shayiri itagharimu mshahara wote wa siku moja. Lakini usiharibu upatikanaji wa mafuta ya mzeituni na divai!”
7 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa nne nilisikia sauti ya kiumbe wa nne mwenye uhai akisema, “Njoo!” 8 Nilipotazama nilimwona farasi mwenye rangi ya kijivu. Aliyempanda alikuwa mauti na kuzimu ilikuwa inamfuata nyuma yake kwa karibu. Alipewa mamlaka juu ya robo ya dunia kuwaua watu kwa upanga, njaa, magonjwa na kwa wanyama wa porini waliomo duniani.
9 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tano, niliziona baadhi ya roho za wale waliokuwa waaminifu kwa neno la Mungu na kweli waliyopokea zikiwa chini ya madhabahu. 10 Roho hizi zilipiga kelele kwa sauti kuu zikisema, “Mtakatifu na Bwana wa kweli, ni lini utakapowahukumu watu wa dunia na kuwaadhibu kwa kutuua sisi?” 11 Kisha kila mmoja wao alipewa kanzu ndefu nyeupe. Wakaambiwa wasubiri kwa muda mfupi kwani bado walikuwepo ndugu zao katika utumishi wa Kristo ambao ni lazima wauawe kama wao. Roho hizi ziliambiwa zisubiri mpaka mauaji yote yatakapokwisha.
12 Kisha nilitazama wakati Mwanakondoo anaufungua muhuri wa sita. Kulitokea tetemeko kubwa la ardhi na jua likawa jeusi kama gunia jeusi[c] na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zikaanguka chini duniani kama mtini uangushavyo tini zake upepo unapovuma. 14 Anga iligawanyika katikati na pande zote zikajiviringa kama kitabu.[d] Na kila mlima na kisiwa kiliondolewa mahali pake.
15 Kisha watu wote wa ulimwengu, wafalme, watawala, makamanda wa majeshi, matajiri, wenye mamlaka na nguvu, kila mtumwa na asiye mtumwa, walijificha katika mapango na nyuma ya miamba milimani. 16 Waliiambia milima na miamba, “Tuangukieni. Tuficheni mbali na uso wa yule aketiye kwenye kiti cha enzi. Tuficheni dhidi ya hasira ya Mwanakondoo! 17 Siku kubwa ya hasira yao imefika. Hakuna anayeweza kupingana nayo.”
Watu 144,000 wa Israeli
7 Baada ya hili kutokea, niliwaona malaika wanne wamesimama kwenye pembe nne za dunia wakiwa wamezishikilia pepo nne za dunia. Walikuwa wanazuia upepo kupuliza katika nchi au katika bahari au kwenye mti wowote. 2 Kisha nikaona malaika mwingine akija akitokea upande wa mashariki. Malaika huyu alikuwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Malaika akawaita kwa sauti kuu malaika wale wanne. Malaika hawa wanne walikuwa malaika ambao Mungu amewapa mamlaka ya kuidhuru dunia na bahari. Malaika akawaambia, 3 “Msiidhuru nchi au bahari au miti kabla hatujawawekea alama kwenye vipaji vya nyuso zao wale wanaomtumikia Mungu wetu.”
4 Kisha nikasikia idadi ya watu wenye alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. Walikuwa watu 144,000. Walitoka katika kila kabila la Israeli:
© 2017 Bible League International