Revised Common Lectionary (Complementary)
Paulo na Sila Wakiwa Gerezani
16 Siku moja tulipokuwa tunakwenda pale mahali pa kufanyia kuomba, mtumishi mmoja msichana alikutana nasi. Msichana huyu alikuwa na roho ya ubashiri[a] ndani yake iliyompa uwezo wa kutabiri mambo yatakayotokea baadaye. Kwa kufanya hivi alipata fedha nyingi kwa ajili ya waliokuwa wanammiliki. 17 Akaanza kumfuata Paulo na sisi sote kila mahali akipaza sauti na kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu! Wanawaambia mnavyoweza kuokolewa!” 18 Aliendelea kufanya hivi kwa siku kadhaa na ikamuudhi Paulo, akageuka na kumkemea yule roho akisema, “Kwa uwezo wa Yesu Kristo, ninakuamuru utoke ndani yake!” Mara ile roho chafu ikamtoka.
19 Wamiliki wa mtumishi yule msichana walipoona hili, wakatambua kuwa hawataweza kumtumia tena ili kupata pesa. Hivyo wakawakamata Paulo na Sila na kuwaburuta mpaka kwa watawala. 20 Wakawaleta Paulo na Sila mbele ya maofisa wa Kirumi na kusema, “Watu hawa ni Wayahudi, wanafanya vurugu katika mji wetu. 21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi haturuhusiwi kuzifuata wala kutenda.”
22 Umati wote wa watu ukawa kinyume na Paulo na Sila. Maofisa wakawachania nguo Paulo na Sila na wakaamuru wapigwe bakora. 23 Walichapwa sana kisha wakawekwa gerezani. Maofisa wakamwambia mkuu wa gereza, “Walinde watu hawa kwa umakini!” 24 Mkuu wa gereza aliposikia amri hii maalumu, aliwaweka Paulo na Sila ndani zaidi gerezani na kuwafunga miguu yao kwenye nguzo kubwa za miti.
25 Usiku wa manane Paulo na Sila walipokuwa wakiomba na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa, wafungwa wengine wakiwa wanawasikiliza. 26 Ghafla kulitokea tetemeko kubwa lililotikisa msingi wa gereza. Milango yote ya gereza ilifunguka, na minyororo waliyofungwa wafungwa wote ikadondoka. 27 Mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza imefunguliwa. Alidhani wafungwa wametoroka, hivyo alichukua upanga wake ili ajiue.[b] 28 Lakini Paulo alipaza sauti akamwambia, “Usijidhuru! Sote tuko hapa!”
29 Mkuu wa gereza akaagiza aletewe taa. Kisha akakimbia kuingia ndani, akitetemeka kwa woga, akaanguka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawatoa nje na kusema, “Nifanye nini ili niokoke?”
31 Wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokolewa pamoja na watu wote waishio katika nyumba yako.” 32 Hivyo Paulo na Sila wakamhubiri ujumbe wa Bwana mkuu wa gereza na watu wote walioishi katika nyumba yake. 33 Ilikuwa usiku sana, lakini mkuu wa gereza aliwachukua Paulo na Sila na akawaosha majeraha yao. Kisha mkuu wa gereza na watu wote katika nyumba yake wakabatizwa. 34 Baada ya hili mkuu wa gereza akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake akawapa chakula. Watu wote walifurahi kwa sababu sasa walikuwa wanamwamini Mungu.
12 “Sikiliza, nakuja upesi! Nakuja na ujira ili kumlipa kila mtu sawa sawa na matendo yake. 13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 Heri walioosha kanzu zao.[a] Watakuwa na haki ya kula chakula kutoka kwenye mti wa uzima. Wanaweza kuingia katika mji kwa kupitia katika malango yake.
16 Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kukuambia mambo hayo kwa ajili ya makanisa. Mimi ni mzao wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi.”
17 Roho Mtakatifu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Kila asikiaye hili aseme pia, “Njoo!” Wote wenye kiu waje wanywe maji ya uzima bure ikiwa wanataka.
20 Yesu ndiye anayesema kwamba haya yote ni kweli. Sasa anasema, “Ndiyo, naja upesi.”
Amina! Njoo, Bwana Yesu!
21 Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja na watu wote.
20 Siwaombei tu hao wafuasi wangu lakini nawaombea pia wale watakaoniamini kutokana na mafundisho yao. 21 Baba, naomba kwamba wote wanaoniamini waungane pamoja na kuwa na umoja. Wawe na umoja kama vile wewe na mimi tulivyoungana; wewe umo ndani yangu nami nimo ndani yako. Nami naomba nao pia waungane na kuwa na umoja ndani yetu. Ndipo ulimwengu nao utaamini kuwa ndiwe uliyenituma. 22 Mimi nimewapa utukufu ule ulionipa. Nimewapa utukufu huo ili wawe na umoja, kama mimi na wewe tulivyo na umoja. 23 Nitakuwa ndani yao, nawe utakuwa ndani yangu. Hivyo watakuwa na umoja kamili. Kisha ulimwengu utajua kwamba wewe ndiwe uliyenituma na ya kuwa uliwapenda jinsi ulivyonipenda mimi.
24 Baba, ninataka hawa watu ulionipa wawe nami mahali pale nitakapokuwa. Nataka wauone utukufu wangu, utukufu ule ulionipa kwa sababu ulinipenda kabla ulimwengu haujaumbwa. 25 Baba wewe ndiye unayetenda yaliyo haki. Ulimwengu haukujui, bali mimi nakujua, na hawa wafuasi wangu wanajua kuwa wewe ndiye uliyenituma. 26 Nimewaonesha jinsi ulivyo, na nitawaonesha tena. Kisha watakuwa na upendo ule ule ulio nao wewe kwangu, nami nitaishi ndani yao.”
© 2017 Bible League International