Revised Common Lectionary (Complementary)
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Laodikia
14 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia:
Huu ni ujumbe kutoka kwa yeye aliye Amina,[a] shahidi mwaminifu na wa kweli, aliye chanzo cha uumbaji wa Mungu.
15 Ninayajua matendo yako. Wewe si moto wala baridi. Ninatamani kama ungekuwa moto au baridi! 16 Lakini wewe ni vuguvugu tu, si moto, wala baridi. Hivyo niko tayari kukutema utoke mdomoni mwangu. 17 Unasema wewe ni tajiri. Unadhani ya kuwa umekuwa tajiri na huhitaji kitu chochote. Lakini hujui kuwa wewe ni mnyonge, mwenye masikitiko, maskini, asiyeona na uko uchi. 18 Ninakushauri ununue dhahabu kutoka kwangu, dhahabu iliyosafishwa katika moto. Kisha utakuwa tajiri. Nakuambia hili: Nunua kwangu mavazi meupe. Ndipo utaweza kuifunika aibu ya uchi wako. Ninakuagiza pia ununue kwangu dawa ya kuweka kwenye macho yako, nawe utaweza kuona.
19 Mimi huwasahihisha na kuwaadhibu wale niwapendao. Hivyo onesha kuwa kuishi kwa haki ni muhimu kwako kuliko kitu kingine. Geuzeni mioyo na maisha yenu. 20 Niko hapa! Nimesimama mlangoni nabisha hodi. Ikiwa utaisikia sauti yangu na ukaufungua mlango, nitaingia kwako na kula pamoja nawe. Nawe utakula pamoja nami.
21 Nitamruhusu kila atakayeshinda kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi. Ilikuwa vivyo hivyo hata kwangu. Nilishinda na kuketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.”
© 2017 Bible League International