Revised Common Lectionary (Complementary)
Sauli Awa Mfuasi wa Yesu
9 Huko Yerusalemu Sauli aliendelea kuwatisha wafuasi wa Bwana, na hata kuwaambia kuwa angewaua. Alikwenda kwa kuhani mkuu, 2 na kumwomba aandike barua kwenda kwenye masinagogi yaliyokuwa katika mji wa Dameski. Sauli alitaka kuhani mkuu ampe mamlaka ya kuwatafuta watu katika mji wa Dameski waliokuwa wafuasi wa Njia ya Bwana.[a] Ikiwa angewapata waamini huko, wanaume au wanawake, angewakamata na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hivyo Sauli alikwenda Dameski. Alipoukaribia mji, ghafla mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza kumzunguka. 4 Akadondoka chini na akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa?”
5 Sauli akasema, “Wewe ni nani, Bwana?”
Sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu, unayemtesa. 6 Simama sasa na uingie mjini. Mtu mmoja huko atakueleza unachopaswa kufanya.”
7 Wanaume waliokuwa wanasafiri pamoja na Sauli walisimama pale kimya. Waliisikia sauti, lakini hawakumwona yeyote. 8 Sauli alisimama kutoka chini na kufumbua macho yake, lakini hakuweza kuona. Hivyo wale aliokuwa nao wakamshika mkono na kumwongoza kuingia Dameski. 9 Kwa siku tatu Sauli hakuweza kuona; hakula wala kunywa.
10 Alikuwepo mfuasi wa Yesu katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Katika maono Bwana alimwita, “Anania!”
Anania alijibu, “Niko hapa, Bwana.”
11 Bwana akamwambia, “Amka na uende katika mtaa unaoitwa Mtaa Ulionyooka. Tafuta nyumba ya Yuda[a] na uliza kuhusu mtu anayeitwa Sauli anayetoka katika mji wa Tarso. Yuko katika nyumba hiyo sasa, anaomba. 12 Ameoneshwa katika maono kuwa mtu anayeitwa Anania anamwendea na kuweka mikono juu yake ili aweze kuona tena.”
13 Lakini Anania akajibu, “Bwana, watu wengi wameniambia kuhusu mtu huyu. Wameniambia kuhusu mambo mengi mabaya aliyowatendea watu wako watakatifu katika mji wa Yerusalemu. 14 Na sasa amekuja hapa Dameski. Viongozi wa makuhani wamempa mamlaka ya kuwakamata watu wote wanaokuamini wewe.”[b]
15 Lakini Bwana Yesu akamwambia Anania, “Nenda, nimemchagua Sauli kwa kazi maalumu. Ninataka ayahubiri mataifa mengine, watawala na watu wa Israeli kuhusu mimi. 16 Nitamwonyesha yote ambayo lazima atateseka kwa ajili yangu.”
17 Hivyo Anania aliondoka na kwenda nyumbani kwa Yuda. Akaweka mikono yake juu ya Sauli na kusema, “Sauli, ndugu yangu, Bwana Yesu amenituma. Ndiye uliyemwona barabarani wakati ukija hapa. Amenituma ili uweze kuona tena, pia ujazwe Roho Mtakatifu.” 18 Ghafla, vitu kama magamba ya samaki vikaanguka kutoka kwenye macho ya Sauli. Akaanza kuona tena! Kisha akasimama na kwenda kubatizwa. 19 Baada ya kula chakula, akaanza kujisikia kuwa na nguvu tena.
Sauli Aanza Kuhubiri Juu ya Yesu Kristo
Sauli alikaa pamoja na wafuasi wa Yesu katika mji wa Dameski kwa siku chache. 20 Baadaye alianza kwenda katika masinagogi na kuwahubiri watu kuhusu Yesu. Aliwaambia watu, “Yesu ni Mwana wa Mungu!”
11 Kisha, nilipotazama, nikasikia sauti ya malaika wengi waliozunguka kiti cha enzi pamoja na viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne. Walikuwa maelfu kwa maelfu ya malaika, elfu kumi mara elfu kumi. 12 Kwa sauti kuu malaika walisema:
“Mamlaka yote, utajiri, hekima na nguvu ni kwa Mwanakondoo aliyeuawa.
Anastahili kupokea heshima, utukufu na sifa!”
13 Ndipo nikasikia kila kiumbe kilichoumbwa kilichoko mbinguni na duniani na chini ya dunia na baharini, viumbe vyote sehemu hizo vikisema:
“Sifa zote na heshima
na utukufu na nguvu kuu ni kwa ajili yake Yeye aketiye
kwenye kiti cha enzi na kwa Mwanakondoo milele na milele!”
14 Viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amina!” Na wazee wakainama chini wakasujudu.
Yesu Awatokea wafuasi Wake Saba
21 Baadaye, Yesu akawatokea tena wafuasi wake karibu na Ziwa Galilaya. Hivi ndivyo ilivyotokea: 2 Baadhi ya wafuasi wake walikuwa pamoja; Simoni Petro, Tomaso (aliyeitwa Pacha), Nathanaeli kutoka Kana kule Galilaya, wana wawili wa Zebedayo, na wafuasi wengine wawili. 3 Simoni Petro akasema, “Ninaenda kuvua samaki.”
Wafuasi wengine wakasema, “Sisi sote tutaenda pamoja nawe.” Hivyo wote wakatoka na kwenda kwenye mashua. Usiku ule walivua lakini hawakupata kitu.
4 Asubuhi na mapema siku iliyofuata Yesu akasimama ufukweni mwa bahari. Hata hivyo wafuasi wake hawakujua kuwa alikuwa ni yeye Yesu. 5 Kisha akawauliza, “Rafiki zangu, mmepata samaki wo wote?”
Wao wakajibu, “Hapana.”
6 Yesu akasema, “Tupeni nyavu zenu kwenye maji upande wa kulia wa mashua yenu. Nanyi mtapata samaki huko.” Nao wakafanya hivyo. Wakapata samaki wengi kiasi cha kushindwa kuzivuta nyavu na kuziingiza katika mashua.
7 Mfuasi aliyependwa sana na Yesu akamwambia Petro, “Mtu huyo ni Bwana!” Petro aliposikia akisema kuwa alikuwa Bwana, akajifunga joho lake kiunoni. (Alikuwa amezivua nguo zake kwa vile alitaka kufanya kazi.) Ndipo akaruka majini. 8 Wafuasi wengine wakaenda ufukweni katika mashua. Wakazivuta nyavu zilizojaa samaki. Nao hawakuwa mbali sana na ufukwe, walikuwa kadiri ya mita 100[a] tu. 9 Walipotoka kwenye mashua na kuingia kwenye maji, wakaona moto wenye makaa yaliokolea sana. Ndani ya moto huo walikuwemo samaki na mikate pia. 10 Kisha Yesu akasema leteni baadhi ya samaki mliowavua.
11 Simoni Petro akaenda kwenye mashua na kuvuta wavu kuelekea ufukweni. Wavu huo ulikuwa umejaa samaki wakubwa, wapatao 153 kwa ujumla! Lakini pamoja na wingi wa samaki hao, nyavu hazikukatika. 12 Yesu akawaambia, “Njooni mle.” Hakuna hata mfuasi mmoja aliyemwuliza, “Wewe ni nani?” Walijua yeye alikuwa ni Bwana. 13 Yesu akatembea ili kuchukua mikate na kuwapa. Akawapa samaki pia.
14 Hii sasa ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
Yesu Azungumza na Petro
15 Walipomaliza kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohana, je, unanipenda kuliko watu wote hawa wanavyonipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akamwambia, “Wachunge wanakondoo[b] wangu.”
16 Kwa mara nyingine Yesu akamwambia, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, wewe unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akasema, “Watunze kondoo wangu.”
17 Mara ya tatu Yesu akasema, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika kwa sababu Yesu alimuuliza mara tatu, “Unanipenda?” Akasema, “Bwana, unafahamu kila kitu. Unajua kuwa nakupenda!”
Yesu akamwambia, “Walinde kondoo wangu. 18 Ukweli ni huu, wakati ulipokuwa mdogo, ulijifunga mwenyewe mkanda wako kiunoni na kwenda ulikotaka. Lakini utakapozeeka, utainyoosha mikono yako,[c] na mtu mwingine atakufunga mkanda wako. Watakuongoza kwenda mahali usikotaka kwenda.” 19 (Yesu alisema hivi kumwonyesha jinsi Petro atakavyokufa ili kumpa utukufu Mungu.) Kisha akamwambia Petro, “Nifuate!”
© 2017 Bible League International