M’Cheyne Bible Reading Plan
Je, ni Sahihi Kuponya Siku ya Sabato?
14 Siku moja ya Sabato Yesu alikwenda nyumbani kwa miongoni mwa viongozi wa Mafarisayo kula chakula pamoja naye. Watu wote mahali pale walikuwa wanamwangalia kwa makini kuona atafanya nini. 2 Mbele yake kulikuwa na mtu aliyekuwa na ugonjwa mbaya.[a] 3 Yesu akawauliza wanasheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au kosa kuponya siku ya Sabato?” 4 Lakini walishindwa kujibu swali lake. Hivyo akamshika yule mgonjwa, na kumponya, akamruhusu aende zake. 5 Kisha akawaambia Mafarisayo na wanasheria, “Ikiwa mwanao au mnyama wako atatumbukia kisimani siku ya Sabato, mnatambua kuwa mtamtoa haraka.” 6 Mafarisayo na wanasheria hawakuweza kujibu kinyume na alivyosema.
Usijifanye Mtu wa Muhimu
7 Ndipo Yesu akagundua kuwa baadhi ya wageni walikuwa wanachagua sehemu za heshima za kukaa mezani. Ndipo akawaambia, 8 “Ukialikwa na mtu katika sherehe ya harusi, usikae katika sehemu za heshima. Wanaweza kuwa wamemwalika mtu muhimu kuliko wewe. 9 Na kama umekaa katika kiti muhimu zaidi, watakuja kwako na kukuambia ‘toka ulipokaa umpishe huyu!’ Ndipo itakulazimu kuhamia sehemu zisizo za heshima na utaaibika.
10 Hivyo ukialikwa, nenda ukae mahali pasipo pa heshima, ili yule aliyekualika akija, akuambie, ‘Rafiki, njoo huku mbele zaidi mahali pazuri.’ Ndipo utaheshimiwa mbele ya wageni wote walio mezani pamoja nawe. 11 Kila ajikwezaye atashushwa. Lakini ajishushaye atakwezwa.”
Utazawadiwa
12 Kisha Yesu akamwambia Farisayo aliyemwalika, “Unapoandaa chakula, usiwaalike rafiki zako tu, au ndugu zako, au jamaa zako, wala jirani zako matajiri. Kwa sababu wao pia watakualika, na kwa kufanya hivyo watakuwa wanakulipa. 13 Lakini ufanyapo sherehe waalike maskini, waliolemaa, walemavu wa miguu, na wasiyeona. 14 Utabarikiwa, kwa sababu watu hawa hawana kitu cha kukulipa. Lakini Mungu atakupa thawabu wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
Mfano Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Chakula
(Mt 22:1-10)
15 Basi mmoja wa watu waliokuwa mezani pamoja naye aliposikia hayo akamwambia Yesu, “Wamebarikiwa watakaokula karamu katika ufalme wa Mungu.”
16 Yesu akamwambia, “Mtu mmoja aliandaa sherehe kubwa, na kuwaalika watu wengi. 17 Wakati wa kuanza sherehe ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie wale walioalikwa, ‘Tafadhalini njooni sasa. Kila kitu kiko tayari.’ 18 Lakini wageni waalikwa wote walisema kuwa hawawezi kuja. Kila mmoja alitoa udhuru. Wa kwanza alisema, ‘Nimenunua shamba, hivyo ni lazima niende nikalitazame. Tafadhali unisamehe.’ 19 Mwingine alisema, ‘Nimenunua ng'ombe wa kulimia jozi tano; ni lazima niende kuwajaribu. Tafadhali unisamehe.’ 20 Na mtu wa tatu alisema, ‘Nimeoa mke, kwa sababu hiyo siwezi kuja.’
21 Hivyo mtumishi alirudi na kumjulisha bwana kilichotokea. Bwana wake akakasirika, akamwambia mtumishi wake, ‘Fanya haraka! Nenda mitaani na katika vichochoro vya mji. Niletee maskini, vilema, wasiyeona na walemavu wa miguu!’
22 Baadaye mtumishi akamwambia, ‘Mkuu nimefanya kama ulivyoniagiza, lakini bado tuna nafasi kwa ajili ya watu wengine zaidi.’ 23 Hivyo bwana wake akamwambia mtumishi, ‘Toka nje uende kwenye barabara zinazoelekea vijijini na kando kando ya mashamba. Waambie watu huko waje, ninataka nyumba yangu ijae! 24 Ninakwambia, sitaki mtu hata mmoja kati ya wale niliowaalika kwanza atakayekula chakula hiki nilichoandaa.’”
Amua Ikiwa Unaweza Kunifuata
(Mt 10:37-38)
25 Watu wengi walikuwa wanasafiri pamoja na Yesu. Akawaambia, 26 “Ikiwa unakuja kwangu na hauko tayari kuiacha familia yako, huwezi kuwa mfuasi wangu. Ukimpenda zaidi baba yako, mama yako, mke wako, watoto wako, kaka na dada zako na hata maisha yako zaidi yangu huwezi kuwa mwanafunzi wangu. 27 Yeyote ambaye hatauchukua msalaba atakaopewa na akanifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu.
28 Ikiwa unataka kujenga nyumba, kwanza utakaa na kuamua ili kujua itakugharimu kiasi gani. Ni lazima uone ikiwa una pesa za kutosha kumaliza kazi ya ujenzi. 29 Usipofanya hivyo, unaweza ukaanza kazi, lakini ukashindwa kumaliza kujenga nyumba. Na usipoweza kuimaliza, kila mtu atakucheka, 30 Watasema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini alishindwa kumalizia.’
31 Ikiwa mfalme anakwenda kupigana vita na mfalme mwingine, atakaa chini kwanza na kupanga. Ikiwa ana askari elfu kumi, ataamua ikiwa ana uwezo wa kumshinda mfalme mwenye askari elfu ishirini. 32 Akiona hawezi kumshinda mfalme mwingine, atatuma baadhi ya watu kwa mfalme mwingine ili wapatane akiwa bado yuko mbali.
33 Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Lazima uache kila kitu ulichonacho. La sivyo, huwezi kuwa mfuasi wangu.
Msipoteze Umuhimu Wenu
(Mt 5:13; Mk 9:50)
34 Chumvi ni kitu kizuri; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, huwezi kuitengenezea ladha tena. 35 Haifai. Huwezi hata kuitumia kama uchafu au mbolea. Watu huitupa tu.
Mnaonisikiliza, sikilizeni!”
Habari Njema Kuhusu Yesu Kristo
15 Sasa ndugu zangu, ninataka mkumbuke Habari Njema niliyowahubiri. Mliupokea ujumbe huo na endeleeni kuishi kwa kuufuata. 2 Habari Njema hiyo, ujumbe mliousikia kutoka kwangu, ni njia ya Mungu kuwaokoa. Ni lazima mwendelee kuuamini. Ikiwa mtaacha, kuamini kwenu ni bure.
3 Niliwapa ujumbe nilioupokea. Niliwaambia ukweli muhimu zaidi ya kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema; 4 kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema 5 na kwamba alimtokea Petro kisha mitume kumi na wawili. 6 Baada ya hilo, aliwatokea waamini wengine zaidi ya mia tano kwa wakati mmoja. Wengi wao bado wanaishi sasa, lakini wengine wamekwisha kufa. 7 Kisha alimtokea Yakobo na baadaye aliwatokea mitume wote. 8 Mwisho wa yote kabisa alinitokea mimi. Nilikuwa tofauti, kama mtoto anayezaliwa wakati usiostahili.
9 Mitume wengine wote ni wakuu kuliko mimi. Ninasema hivi kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. Ndiyo sababu sistahili hata kuitwa mtume. 10 Lakini, kwa sababu ya neema ya Mungu, ndivyo hivi nilivyo. Na neema aliyonipa haikupotea bure bila manufaa. Nilifanya kazi kwa bidii kuliko mitume wengine wote. (Lakini, kwa hakika si mimi niliyekuwa nafanya kazi. Ni neema ya Mungu iliyo ndani yangu.) 11 Hivyo basi, si muhimu ikiwa ni mimi au mitume wengine ndiyo waliowahubiri, sisi sote tunawahubiri watu ujumbe huo huo, na hiki ndicho mlichoamini.
Tutafufuliwa Kutoka kwa Wafu
12 Tunamwambia kila mtu kuwa Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Hivyo kwa nini baadhi yenu mnasema watu hawatafufuliwa kutoka kwa wafu? 13 Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu. 14 Na ikiwa Kristo hakufufuliwa, ujumbe tunaowahubiri ni bure. Na imani yenu ni bure. 15 Nasi tutakuwa na hatia ya kutoa ushuhuda wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumewahubiri watu kuhusu Yeye, kwa kusema kuwa alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Na ikiwa hakuna anayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Mungu hakumfufua Kristo. 16 Ikiwa wale waliokufa hawatafufuliwa, basi Kristo hakufufuliwa pia. 17 Na ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, basi imani yenu ni bure; bado mngali watumwa wa dhambi zenu. 18 Na watu wa Kristo waliokwisha kufa wamepotea. 19 Ikiwa tumaini letu katika Kristo ni kwa ajili tu ya maisha haya hapa duniani, basi watu watuhurumie sisi kuliko mtu mwingine yeyote.
20 Lakini hakika Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu; ndiye wa kwanza miongoni mwa wafu wote watakaofufuliwa. 21 Kifo huja kwa watu kwa sababu ya tendo la mtu mmoja. Lakini sasa kuna ufufuo kutoka kwa wafu kwa sababu ya mtu mwingine. 22 Ndiyo, kwa sababu sisi sote ni wa Adamu, sisi sote tunakufa. Kwa njia hiyo hiyo, sisi sote tulio wa Kristo, tutakuwa hai tena. 23 Lakini kila mmoja atafufuliwa kwa mpango sahihi. Kristo alikuwa wa kwanza kufufuliwa. Kisha atakaporudi, wale walio wake watafufuliwa. 24 Ndipo mwisho utakuja. Kristo atamwangamiza kila mtawala na kila mamlaka na nguvu. Kisha atampa Mungu Baba ufalme.
25 Kristo lazima atawale mpaka Mungu atakapowaweka adui zake wote chini ya udhibiti wake.[a] 26 Adui wa mwisho kuangamizwa ni kifo. 27 Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu ameweka kila kitu chini ya udhibiti wake.”(A) Inaposema “kila kitu” kimewekwa chini yake, hii ni wazi Mungu peke yake ndiye ambaye hayuko chini yake. Mungu ndiye anayeweka kila kitu chini ya udhibiti wa Kristo. 28 Baada ya kuweka kila kitu chini ya Kristo, ndipo yeye mwenyewe, kama Mwana, atawekwa chini ya Mungu. Katika namna hii Mungu atakuwa mtawala mkuu juu ya kila kitu.
29 Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, sasa watu wanafikiri wanafanya nini kwa kubatizwa kwa ajili ya wale waliokufa? Ikiwa wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini watu wanabatizwa kwa ajili yao?
30 Na vipi kuhusu sisi? Kwa nini tunajiweka katika hatari wakati wote? 31 Ninakumbana na kifo kila siku. Ni kweli, ndugu zangu kwamba ninajivuna kwa sababu ninyi ni wa Kristo Yesu Bwana wetu. 32 Niliwapiga wanyama wa porini kule Efeso. Ikiwa nilifanya hivyo kwa sababu za kibinadamu tu, sijapata kitu. Ikiwa hatufufuliwi kutoka kwa wafu, “basi tule na tunywe, kwa sababu tutakufa kesho.”(B)
33 Msidanganywe: “Marafiki wabaya huharibu tabia njema.” 34 Rudieni kuwaza kwenu kwa usahihi na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hamumjui Mungu. Ninasema hivi ili niwafedheheshe.
Tutakuwa na Mwili wa Namna Gani?
35 Lakini mtu mmoja anaweza kuuliza, “Waliokufa wanafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Haya ni maswali ya kijinga. Unapopanda kitu fulani, ni lazima kife udongoni kabla hakijawa hai na kuota. 37 Na unapopanda kitu fulani, unachopanda hakina “mwili” sawa na ule kitakachokuwa nao baadaye. Unapanda mbegu, pengine ngano au kitu kingine. 38 Na yeye Mungu hutoa mwili kwa kila aina ya mbegu. 39 Vitu vyote vilivyoumbwa kwa mwili haviko sawa: Wanadamu wana aina moja ya mwili, wanyama wana aina nyingine, ndege wana nyingine na samaki nao wana aina yao. 40 Pia kuna miili ya kimbingu na miili ya kidunia. Lakini uzuri wa miili ya kimbingu ni wa aina yake na uzuri wa miili ya kidunia ni kitu kingine. 41 Jua lina uzuri wa aina yake, mwezi una aina yake na nyota zina aina nyingine ya uzuri. Na kila nyota iko tofauti kwa uzuri wake.
42 Ndivyo itakavyokuwa waliokufa watakapofufuliwa na kuwa hai. Mwili “uliopandwa” kaburini utaharibika na kuoza, lakini utafufuliwa katika uhai usioharibika. 43 Mwili hauna heshima “unapopandwa”. Lakini utakapofufuliwa, utakuwa na utukufu. Mwili unakuwa dhaifu “unapopandwa”. Lakini unapofufuliwa, unakuwa na nguvu nyingi. 44 Mwili unaopandwa ni mwili wa kawaida, wa asili. Utakapofufuliwa utakuwa mwili wa ajabu uliopewa uwezo na Roho.
Kuna mwili wa asili unaoonekana kwa macho. Na hivyo kuna mwili wa Kiroho wa ajabu. 45 Kama Maandiko yanavyosema, “Mtu[b] wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe asili kilichokuwa hai.”(C) Lakini Adamu[c] wa mwisho akafanyika roho. 46 Mtu wa kiroho hakuja kwanza. Mtu wa asili anayeonekana kwa macho ndiye alikuja kwanza; kisha akaja wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza alitokana na mavumbi ya dunia. Mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Watu wote ni wa dunia. Wako sawa na yule mtu wa kwanza wa dunia. Lakini wale walio wa mbinguni wako kama mtu wa mbinguni. 49 Tumeivaa sura ya mtu aliyetoka mavumbini, pia tutaivaa sura ya mtu aliyetoka mbinguni.
50 Ninawaambia hili ndugu zangu: Miili yetu na nyama na damu haiwezi kuwa na nafasi katika ufalme wa Mungu. Kitu kitakachoharibika hakiwezi kuwa na sehemu katika kitu kisichoharibika kamwe. 51 Lakini sikilizeni, ninawaambia siri hii: Sote hatutakufa, lakini sote tutabadilishwa. 52 Itachukuwa sekunde moja. Tutabadilishwa kufumba na kufumbua. Hili litatokea parapanda ya mwisho itakapopulizwa. Parapanda itakapolia wale waliokufa watafufuliwa ili waishi milele. Na tutabadilishwa sote. 53 Mungu ataibadilisha miili yetu ili isiharibike kamwe. Mwili huu unaokufa utabadilishwa na kuwa mwili usiokufa. 54 Hivyo mwili huu unaokufa utajivika kutokufa. Hili litakapotokea, ndipo Maandiko yatatimilizwa:
“Mauti imemezwa katika ushindi.(D)
55 Ewe kifo, ushindi wako uko wapi?
Nguvu yako ya kudhuru iko wapi?”(E)
56 Dhambi ni nguvu ya mauti inayodhuru, na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini tunamshukuru Mungu anayetupa ushindi kupitia Yesu Kristo Bwana wetu!
58 Hivyo, kaka na dada zangu, simameni imara. Msiruhusu kitu chohote kiwabadilishe. Jitoeni nafsi zenu kikamilifu kwa kazi yenu katika Bwana. Mnajua ya kuwa chochote mnachofanya kwa ajili ya Bwana hakitapotea bure bila manufaa.
© 2017 Bible League International