Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Exod for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Luka 13

Badilisheni Namna Mnavyoishi

13 Sehemu ya watu waliokuwa pamoja na Yesu pale, walimweleza kilichowapata baadhi ya waabuduo kutoka Galilaya. Pilato alikuwa ameamuru wauawe. Damu zao zilichanganywa na damu za wanyama waliowaleta kwa ajili ya kutoa dhabihu. Yesu alijibu akasema, “Mnadhani hili liliwapata watu hao kwa sababu walikuwa wenye dhambi kuliko watu wengine wote wa Galilaya? Hapana, hawakuwa hivyo. Lakini ikiwa hamtaamua kubadili maisha yenu sasa, ninyi nyote mtaangamizwa kama wao! Na vipi kuhusu wale watu kumi na wanane waliokufa pale mnara wa Siloamu ulipowaangukia? Mnadhani walikuwa na dhambi kuliko watu wengine katika mji wa Yerusalemu? Hawakuwa hivyo. Lakini ninawaambia, ikiwa hamtaamua kubadilika sasa, hata ninyi mtaangamizwa pia!”

Mti Usiozaa Matunda

Yesu akawasimulia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa amepanda mtini katika shamba lake. Alipokuja kutafuta matunda kwenye mtini huo hakupata tunda lolote. Alikuwa na mtumishi aliyekuwa akilitunza shamba. Hivyo alimwambia mtumishi wake, ‘Nimekuwa nikitafuta matunda kwenye mti huu kwa miaka mitatu, lakini sijawahi kupata tunda lolote. Ukate mti huu! Kwa maana unaiharibu ardhi.’ Lakini mtumishi alijibu, ‘Mkuu, tuuache mti huu mwaka mmoja zaidi ili tuone ikiwa utazaa matunda. Nitakusanya samadi kuuzunguka ili kuupa mbolea. Unaweza kuzaa matunda mwaka ujao. Ikiwa hautazaa, ndipo utaweza kuukata.’”

Yesu Amponya Mwanamke Siku ya Sabato

10 Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi moja siku ya Sabato. 11 Alikuwepo mwanamke mmoja ndani ya sinagogi aliyekuwa na pepo mchafu aliyemlemaza kwa muda wa miaka kumi na nane. Mgongo wake ulikuwa umepinda na hakuweza kusimama akiwa amenyooka. 12 Yesu alipomwona alimwita na kumwambia, “Mama, umefunguliwa kutoka katika ugonjwa wako!” 13 Akaweka mikono yake juu yake na saa hiyo hiyo akaweza kusimama akiwa amenyooka. Akaanza kumsifu Mungu.

14 Kiongozi wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu aliponya siku ya Sabato. Akawaambia watu, “Kuna siku sita za kufanya kazi. Hivyo njooni ili mponywe katika moja ya siku hizo, msije siku ya Sabato kutafuta uponyaji.”

15 Yesu akamjibu kwa kusema, “Ninyi watu ni wanafiki! Ninyi nyote huwafungulia punda au ng'ombe wenu wa kulimia kutoka zizini na kuwapeleka kunywa maji kila siku, hata siku ya Sabato. 16 Mwanamke huyu niliyemponya ni mzaliwa halisi wa Ibrahimu.[a] Lakini Shetani alikuwa amemfunga kwa miaka kumi na nane. Hakika si kosa yeye kuponywa ugonjwa wake siku ya Sabato!” 17 Yesu aliposema haya, watu wote waliokuwa wanampinga walidhalilika. Kundi lote likafurahi kwa sababu ya mambo makuu aliyatenda.

Simulizi Nyingine ya Ufalme

(Mt 13:31-33; Mk 4:30-32)

18 Kisha Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Niufananishe na nini? 19 Ufalme wa Mungu ni kama mbegu ya haradali. Mtu mmoja aliichukua na kuipanda katika bustani yake. Mbegu ikaota, ikakua na kuwa mti na ndege wakatengeneza viota kwenye matawi yake.”

20 Yesu akasema tena, “Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? 21 Ufalme wa Mungu unafanana na kiasi kidogo cha chachu ambacho mwanamke hutumia kuchanganya na kilo 20 za unga kutengeneza mkate. Hamira huumua kinyunya[b] chote.”

Mlango Mwembamba

(Mt 7:13-14,21-23)

22 Yesu alikuwa akifundisha katika kila mji na kijiji. Aliendelea kusafiri kuelekea Yerusalemu. 23 Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, watu wangapi wataokolewa? Ni wachache?”

Yesu akajibu, 24 “Mlango wa kuingia katika ufalme wa Mungu ni mwembamba. Jitahidini kuingia kupitia mlango huo. Watu wengi watataka kuingia huko, lakini hawataweza. 25 Mtu anapoufunga mlango wa nyumba yake, unaweza ukasimama nje na kubisha mlangoni, lakini hataufungua. Mnaweza kusema, ‘Mkuu tufungulie mlango!’ Lakini yeye akawajibu, ‘Siwajui ninyi na mnakotoka sikujui.’ 26 Ndipo mtaanza kusema, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe. Ulifundisha katika mitaa ya mji wetu.’ 27 Kisha atawaambia, ‘Siwajui na sijui mlikotoka! Ondokeni kwangu! Ninyi nyote ni watu mnaotenda maovu!’

28 Mtamwona Ibrahimu, Isaka, Yakobo na manabii wote wakiwa katika ufalme wa Mungu. Lakini ninyi wenyewe mtatupwa nje. Hapo mtalia na kusaga meno yenu kwa uchungu. 29 Watu watakuja kutoka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini. Watakaa kuizunguka meza ya chakula katika ufalme wa Mungu. 30 Zingatieni kwamba wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”

Yesu Atakufa Yerusalemu

(Mt 23:37-39)

31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakaja kwa Yesu, na wakamwambia, “Ondoka hapa, nenda ukajifiche. Kwa sababu Herode anataka kukuua!”

32 Lakini Yesu akawaambia, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha,[c] ‘Leo na kesho ninatoa pepo wachafu na kuponya watu, na kesho kazi itakwisha.’ 33 Baada ya hilo, ni lazima niende, kwa sababu manabii wote wanapaswa kufia Yerusalemu.

34 Yerusalemu! Yerusalemu! Uwauaye manabii. Unawapiga kwa mawe watu waliotumwa na Mungu kwako. Mara ngapi nimetaka kuwasaidia watu wako! Nilitaka kuwakusanya kama kuku anavyovikusanya vifaranga vyake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu. 35 Mungu atakuacha ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(A)

Error: Book name not found: Job for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
1 Wakorintho 14

Zitumieni Karama za Roho Kulisaidia Kanisa

14 Upendo uwe lengo la maisha yenu, lakini mnapaswa pia kuzitaka karama za Roho. Na itakeni sana karama ya unabii. Nitafafanua ni kwa nini. Wenye karama ya kusema kwa lugha zingine hawazungumzi na watu. Huzungumza na Mungu. Hakuna anayewaelewa kwa sababu huzungumza mambo ya siri kupitia Roho. Lakini wanaotabiri huzungumza na watu. Huwasaidia watu kuwa imara katika imani, na huwatia moyo na kuwafariji. Wanaosema kwa lugha hujiimarisha wao wenyewe. Lakini wanaotabiri huliimarisha kanisa lote.

Ningependa ninyi nyote muwe na karama ya kusema kwa lugha zingine. Lakini ninachotaka zaidi ni ninyi kutabiri. Yeyote anayetabiri ni wa muhimu zaidi kuliko wale wanaosema kwa lugha zingine. Hata hivyo, ikiwa wanaweza kufasiri lugha hizo, basi kanisa linasaidiwa kutokana na kile wanachosema.

Ndugu zangu, je, itawasaidia nikija kwenu na kusema kwa lugha zingine? Hapana, itawasaidia pale tu nitakapowaletea ufunuo mpya au maarifa fulani, unabii au mafundisho. Hii ni kweli hata kwa vitu visivyo na uhai vinavyotoa sauti kama filimbi na kinubi. Ikiwa muziki hauchezwi kwa ufasaha, hutaweza kujua ni wimbo gani unaopigwa. Na katika vita, ikiwa tarumbeta haitatoa ishara vizuri, askari hawawezi kujua kuwa ni wakati wa kujiandaa kwa mapigano.

Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Watu hawataweza kuelewa unachosema, ikiwa utazungumza katika lugha tofauti wasiyoitambua. Utakuwa unazungumza hewani tu! 10 Ni dhahiri kuwa kuna lugha nyingi ulimwenguni, na zote zina maana. 11 Lakini ikiwa sielewi maana ya maneno wanayosema wengine, kwangu itakuwa sauti ya ajabu tu, na nitasikika kama ninayetoa sauti za ajabu. 12 Kwa kuwa mna nia kuhusu karama za Kiroho, muwe na hamu ya kulisaidia kanisa kuwa imara.

13 Hivyo wenye karama ya kusema kwa lugha waombe ili waweze kufasiri yale wanayosema. 14 Ninapoomba kwa lugha zingine, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haifanyi chochote. 15 Hivyo nifanye nini? Nitaomba kwa roho yangu, lakini pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho yangu, lakini pia nitaimba kwa akili yangu. 16 Unaweza ukawa unamshukuru Mungu kwa roho yako. Lakini mtu mwingine ambaye haielewi lugha unayotumia hawezi kusema “Amina” kwa maombi yako ya shukrani. 17 Unaweza ukawa unamshukuru Mungu katika njia nzuri, lakini isiwasaidie wengine kuwa imara.

18 Ninamshukuru Mungu kwamba nimepewa karama ya kusema lugha aina nyingi mbalimbali kuliko yeyote kati yenu. 19 Lakini wakati wa mikutano ya kanisa napenda kuzungumza maneno matano ninayoyaelewa kuliko maelfu ya maneno katika lugha zingine. Ni afadhali nizungumze nikiwa katika uelewa wangu ili niwafundishe wengine.

20 Ndugu zangu, msiwaze kama watoto wadogo. Iweni kama watoto wachanga katika mambo maovu, lakini katika kuwaza kwenu muwe kama watu wazima, waliokua. 21 Kama Maandiko[a] yanavyosema,

“Kwa kutumia wanaozungumza lugha tofauti
    na kutumia midomo ya wageni,
nitazungumza na watu hawa,
    hata hivyo, hawatanitii.”(A)

Hivi ndivyo Bwana anasema.

22 Na kutokana na hili tunaona kwamba matumizi ya lugha zingine ni ishara kuonesha namna ambavyo Mungu anawashughulikia wasioamini, na si walioamini. Na unabii unaonesha namna ambavyo Mungu hutenda kazi kupitia wanaoamini, na si wasioamini. 23 Chukulieni kuwa kanisa lote limekusanyika nanyi nyote mkaanza kusema kwa lugha zingine. Ikiwa baadhi ya watu wasio sehemu ya kundi lenu au wasio waamini wataingia katika kusanyiko lenu, watasema ninyi ni wendawazimu. 24 Lakini chukulieni kuwa ninyi nyote mnatabiri na mtu asiyeamini ama asiyekuwa sehemu ya kundi lenu akaingia. Dhambi zao zitawekwa wazi kwao, na watahukumiwa kwa kila kitu mtakachosema. 25 Mambo ya siri katika mioyo yao yatajulikana. Na watapiga magoti na kumwabudu Mungu. Watakiri na kusema, “Pasipo shaka, Mungu yuko hapa pamoja nanyi.”[b]

Mikutano Yenu Inapaswa Kuwasaidia Wote

26 Basi ndugu, mnapaswa kufanya nini? Mnapokusanyika, mtu mmoja ana wimbo, mwingine ana mafundisho na mwingine ana kweli mpya kutoka kwa Mungu. Mmoja anasema kwa lugha nyingine na mwingine anafasiri lugha hiyo. Cho chote mnachofanya lazima kiwe na lengo la kumfanya kila mmoja wenu akue katika imani. 27 Mnapokusanyika, ikiwa kuna yeyote atasema na kanisa katika lugha, iwe watu wawili tu au isiwe zaidi ya watu watatu. Na wanapaswa wanene kwa zamu, mmoja baada ya mwingine. Na mwingine afasiri kile wanachosema. 28 Lakini ikiwa hakuna mfasiri, basi mtu yeyote anayesema kwa lugha nyingine anapaswa kunyamaza kimya. Wanapaswa kuzungumza katika nafsi zao wenyewe ama na Mungu.

29 Na manabii wawili au watatu tu ndiyo wanapaswa kuzungumza. Wengine watathmini kile wanachosema. 30 Na ujumbe kutoka kwa Mungu ukimjia mtu aliyekaa, mzungumzaji wa kwanza anapaswa kunyamaza. 31 Nyote mnaweza kutabiri mmoja baada ya mwingine. Kwa njia hii kila mmoja anaweza kufundishwa na kutiwa moyo. 32 Roho za manabii ziko chini ya udhibiti wa manabii[c] wenyewe. 33 Mungu si Mungu wa machafuko lakini ni Mungu wa amani. Hii ni kanuni kwa ajili ya mikutano yote ya watu wa Mungu.

34 Wanawake wanapaswa kunyamaza katika mikutano hii ya kanisa. Kama Sheria ya Musa inavyosema, hawaruhusiwi kuzungumza pasipo utaratibu bali wawe chini ya mamlaka. 35 Wakiwa na jambo wanalotaka kujua, wawaulize waume zao nyumbani. Ni aibu kwa mwanamke kuzungumza pasipo utaratibu katika mikutano ya kanisa.

36 Je, ni kutoka kwenu neno la Mungu lilikuja ama lilikuja kwa ajili yenu pekee? 37 Ikiwa yeyote kati yenu anafikiri kuwa yeye ni nabii au kwamba ana karama ya kiroho, anapaswa kuelewa kuwa ninachowaandikia ninyi nyote ni amri ya Bwana. 38 Ikiwa yeyote miongoni mwenu hatalikubali hili, basi hatakubaliwa.

39 Hivyo ndugu zangu, mzingatie sana kutabiri. Na msimzuie mtu yeyote kutumia karama ya kusema katika lugha zingine. 40 Lakini kila kitu kifanywe kwa usahihi na kwa utaratibu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International