M’Cheyne Bible Reading Plan
Luka Aandika Kuhusu Maisha ya Yesu
1 Mheshimiwa Theofilo:[a]
Watu wengine wengi wamejaribu kuandika juu ya mambo yaliyotokea katikati yetu ili kuukamilisha mpango wa Mungu. 2 Mambo hayo waliyoyaandika yanalingana na yale tuliyosikia kutoka kwa watu walioyaona tangu mwanzo. Na walimtumikia Mungu kwa kuwaambia wengine ujumbe wake. 3 Nimechunguza kila kitu kwa makini tangu mwanzo. Na nimeona kuwa ni vyema nikuandikie kwa mpangilio mzuri. 4 Nimefanya hivi ili uwe na uhakika kuwa yale uliyofundishwa ni ya kweli.
Malaika Amjulisha Zakaria Kuhusu Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
5 Herode alipokuwa mfalme wa Uyahudi, alikuwepo kuhani mmoja aliyeitwa Zakaria, aliyekuwa mmoja wa makuhani wa kikundi[b] cha Abiya. Mkewe alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Haruni, na jina lake alikuwa Elizabeti. 6 Wote wawili Zakaria na Elizabeti walikuwa wema waliompendeza Mungu na daima walifanya yote yaliyoamriwa na Bwana na kila mara walifuata maagizo yake kwa ukamilifu. 7 Lakini hawakuwa na watoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana.
8 Ilipofika zamu ya kundi la Zakaria kuhudumu Hekaluni, yeye mwenyewe alikuwepo ili kuhudumu kama kuhani mbele za Mungu kwa ajili kundi. 9 Makuhani walikuwa wanapiga kura kumchagua mmoja wao atakayeingia katika Hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na Zakaria alichaguliwa wakati huu. 10 Wakati wa kufukiza uvumba ulipofika watu wote walikusanyika nje ya Hekalu wakiomba.
11 Zakaria akiwa ndani ya Hekalu alitokewa na malaika wa Bwana akiwa amesimama mbele yake upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba. 12 Zakaria alipomwona malaika aliogopa, na akaingiwa na hofu. 13 Lakini Malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria. Mungu amelisikia ombi lako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Utafurahi sana, na watu wengine wengi watamfurahia pamoja nawe. 15 Atakuwa mkuu kwa ajili ya Bwana. Kamwe asinywe mvinyo wala kitu chochote kile kitakachomlewesha. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa mama yake.
16 Naye atawafanya Waisraeli wengi wamrudie Bwana Mungu wao. 17 Atamtangulia Bwana ili kuwaandaa watu kuupokea ujio wake. Atakuwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha wazazi na watoto wao na kuwafanya wale wasiomtii Mungu kubadilika na kuanza kumtii Mungu.”
18 Zakaria akamwambia malaika, “Nitajuaje kuwa haya unayosema ni ya kweli? Maana mimi ni mzee na mke wangu ana umri mkubwa pia.”
19 Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, ambaye daima husimama mbele za Mungu nikiwa tayari. Amenituma kuzungumza nawe na kukujulisha habari hizi njema. 20 Sasa sikiliza! Hautaweza kuzungumza mpaka siku ambayo mambo haya yatatokea kwa sababu hukuyaamini yale niliyokwambia. Lakini nilichosema hakika kitatokea.”
21 Watu waliokuwa nje ya Hekalu wakimngojea Zakaria walishangaa kwa sababu alikaa kwa muda mrefu ndani ya Hekalu. 22 Zakaria alipotoka nje hakuweza kuzungumza nao. Aliwafanyia watu ishara kwa mikono yake. Hivyo watu walitambua kuwa alikuwa ameona maono alipokuwa Hekaluni. 23 Zamu ya utumishi wake ilipokwisha alirudi nyumbani.
24 Wakati fulani baadaye, Elizabeti, mke wa Zakaria akawa mjamzito. Alikaa katika nyumba yake na hakutoka nje kwa miezi mitano. Alisema, 25 “Na sasa, hatimaye Bwana amenisaidia kwa kuniondolea aibu yangu.”
Malaika Atangaza Kuzaliwa kwa Yesu
26-27 Mwezi wa sita wa ujauzito wa Elizabeti, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa msichana mmoja bikira aliyeishi Nazareti, mji wa Galilaya. Msichana huyo alikuwa amechumbiwa na Yusufu mzaliwa katika ukoo wa Daudi. Jina la bikira huyo lilikuwa Mariamu. 28 Malaika alimwendea na kusema “Salamu! Bwana yu pamoja nawe; Kwa kuwa neema yake iko juu yako.”
29 Lakini, Mariamu alichanganyikiwa kutokana na yale aliyosema malaika. Akajiuliza, “Salamu hii ina maana gani?”
30 Malaika akamwambia, “Usiogope Mariamu, kwa kuwa neema ya Mungu iko juu yako. 31 Sikiliza! Utapata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. 32 Mtoto huyo atakuwa Mkuu na watu watamwita Mwana wa Mungu Aliye Mkuu Sana na Bwana Mungu atamfanya kuwa mfalme kama Daudi baba yake. 33 Naye ataitawala nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34 Mariamu akamwambia malaika, “Jambo hili litatokeaje? Kwa maana mimi bado ni bikira.”
35 Malaika akamwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujia, na nguvu zake Mungu Mkuu zitakufunika. Na hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Pia sikiliza hili: Jamaa yako Elizabeti ni mjamzito. Ijapokuwa ni mzee sana, atazaa mtoto wa kiume. Kila mtu alidhani hataweza kuzaa, lakini sasa huu ni mwezi wa sita wa ujauzito wake. 37 Mungu anaweza kufanya jambo lolote!”
38 Mariamu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, basi jambo hili litokee kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka.
1 Salamu kutoka kwa Paulo. Mimi ni mtume kwa sababu Kristo Yesu[a] alinichagua. Alinichagua kwa sababu hivyo ndivyo Mungu alitaka. Naandika barua hii kwa msaada wa Sosthenesi[b] aliye kaka yetu katika Kristo.
2 Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, ninyi ambao mmefanywa watakatifu kwa sababu mmeunganishwa kwa Kristo Yesu. Mlichaguliwa kuwa watakatifu wa Mungu pamoja na watu wote kila mahali wanaomwamini Bwana[c] Yesu Kristo, Bwana wao na Bwana wetu.
3 Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.
Paulo Amshukuru Mungu
4 Ninamshukuru Mungu daima kwa sababu ya neema aliyowapa katika Kristo Yesu. 5 Ambaye kwa njia yake Mungu amewabariki sana kwa namna mbalimbali hata miongoni mwenu wapo watu wenye vipawa vya kuzungumza na wengine wana vipawa vya maarifa! 6 Hii ni kwa sababu yale tuliyowaambia kuhusu Kristo yamedhihirika kuwa kweli katikati yenu. 7 Na sasa mna karama zote mnapomsubiri Mungu audhihirishie ulimwengu jinsi Bwana wetu Yesu Kristo alivyo wa ajabu. 8 Ataendelea kuwatia nguvu na hakuna atakayeweza kuwashtaki mpaka siku ya mwisho Bwana wetu Yesu atakaporudi. 9 Mungu ni mwaminifu. Na ndiye aliyewachagua ninyi ili mshiriki uzima pamoja na Mwanaye, Yesu Kristo Bwana wetu.
Acheni Mabishano Miongoni Mwenu
10 Ndugu zangu, kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, ninawasihi mpatane ninyi kwa ninyi. Msigawanyike katika makundi. Lakini iweni pamoja tena katika kuwaza kwenu na katika nia zenu.
11 Kaka na dada zangu, baadhi ya jamaa wa Kloe wamenitaarifu kuwa kuna mabishano miongoni mwenu. 12 Baadhi yenu husema, “Mimi ninamfuata Paulo,”[d] na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Apolo.” Mwingine husema, “Mimi ninamfuata Petro,”[e] na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Kristo.” 13 Kristo hawezi kugawanywa katika makundi. Je, Paulo ndiye alikufa msalabani kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa katika jina la Paulo? 14 Ninashukuru kwa kuwa sikumbatiza mtu yeyote kwenu isipokuwa Krispo na Gayo. 15 Ninashukuru kwa sababu hakuna anayeweza kusema kuwa mlibatizwa katika jina langu. 16 (Niliwabatiza pia watu wote wa nyumbani mwa Stefana, lakini sikumbuki kuwa niliwabatiza watu wengine) 17 Kristo hakunipa kazi ya kubatiza watu. Alinipa kazi ya kuhubiri Habari Njema pasipo kutumia hekima ya maneno, inayoweza kubatilisha nguvu iliyo katika msalaba[f] wa Kristo.
Nguvu ya Mungu na Hekima Katika Kristo Yesu
18 Mafundisho kuhusu msalaba yanaonekana ni ya kipuuzi kwao wao wanaoelekea kwenye uharibifu. Lakini ni nguvu ya Mungu kwetu sisi tunaookolewa. 19 Kama Maandiko yanavyosema,
“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima.
Nitaukanganya uelewa wa wenye akili.”(A)
20 Je, hii inasema nini kuhusu mwenye hekima, mtaalamu wa sheria au yeyote katika ulimwengu huu mwenye ujuzi wa kutengeneza hoja zenye nguvu? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upuuzi. 21 Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu katika hekima yake aliamua kuwa hawezi kupatikana kwa kutumia hekima ya ulimwengu. Hivyo Mungu aliutumia ujumbe unaoonekana kuwa upuuzi kuwaokoa wale wanaouamini.
22 Na hii ndiyo sababu Wayahudi wanataka ishara za miujiza na Wayunani wanataka hekima. 23 Lakini ujumbe tunaomwambia kila mtu unahusu Masihi aliyekufa msalabani. Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi na kwa Wayunani ni upuuzi. 24 Lakini kwa Wayahudi na Wayunani walioteuliwa na Mungu, Masihi huyu aliyesulibiwa ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. 25 Maana upumbavu wa Mungu ni hekima zaidi ya hekima ya kibinadamu, na udhaifu wa Mungu ni nguvu zaidi ya nguvu ya kibinadamu.
26 Kaka na dada zangu, fikirini kuhusu hili kwamba Mungu aliwachagua ili muwe milki yake. Wachache wenu mlikuwa na hekima kwa namna dunia inavyoichukulia hekima. Wachache wenu mlikuwa mashuhuri na wachache wenu mnatoka katika familia maarufu. 27 Lakini Mungu aliyachagua mambo ambayo wanadamu huyachukulia kuwa ya kipumbavu ili ayaaibishe yenye hekima. Aliyachagua mambo yanayoonekana kuwa manyonge ili ayaaibishe yenye nguvu. 28 Aliwachagua wasio kitu ili ayaangamize yale ambayo ulimwengu unadhani ni muhimu. 29 Mungu alifanya hivi ili mtu yeyote asisimame mbele zake na akajisifu kuwa yeye ni bora kuliko mwingine. 30 Lakini Mungu ameyafungamanisha maisha yenu na Kristo Yesu. Yeye alifanywa kuwa hekima yetu kutoka kwa Mungu. Na kupitia kwake tumehesabiwa haki na Mungu na tumefanywa kuwa watakatifu. Kristo ndiye aliyetuokoa, akatufanya watakatifu na akatuweka huru mbali na dhambi. 31 Hivyo, kama Maandiko yanavyosema, “Kila anayejisifu, ajisifu juu ya Bwana tu.”(B)
© 2017 Bible League International