M’Cheyne Bible Reading Plan
Furaha Mbinguni
(Mt 18:12-14)
15 Watoza ushuru na wenye dhambi wengi waliendelea kuja kumsikiliza Yesu. 2 Hivyo Mafarisayo na walimu wa sheria wakaanza kulalamika wakisema, “Mtazameni mtu huyu[a] huwakaribisha wenye dhambi na hata kula pamoja nao!”
3 Hivyo Yesu akawaambia mfano huu, 4 “Chukulia mmoja wenu ana kondoo mia, lakini mmoja akapotea. Utafanya nini? Utawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea mpaka umpate. 5 Na ukishampata, utafurahi sana. Utambeba mabegani mwako 6 mpaka nyumbani. Kisha utakwenda kwa majirani na rafiki zako na utawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea!’ 7 Katika namna hiyo hiyo ninawaambia, kunakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mtu anayeacha dhambi zake. Kuna furaha zaidi kwa ajili ya mtu mmoja anayeacha dhambi kuliko watu wema tisini na tisa ambao hudhani hawahitaji kubadilika.
8 Fikiria kuhusu mwanamke mwenye sarafu kumi za fedha,[b] lakini akapoteza sarafu moja kati ya hizo. Atawasha taa na kuifagia nyumba. Ataitafuta sarafu kwa bidii mpaka aione. 9 Na akiiona, atawaita rafiki na jirani zake na kuwaaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu niliyoipoteza!’ 10 Katika namna hiyo hiyo, ni furaha kwa malaika wa Mungu, mwenye dhambi mmoja anapotubu.”
Simulizi Kuhusu Mwana Mpotevu
11 Kisha Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12 Mwana mdogo alimwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali ninayotarajia kurithi baadaye.’ Hivyo baba yake akagawa utajiri wake kwa wanawe wawili.
13 Baada ya siku chache yule mdogo akauza mali zake, akachukua pesa zake na akaondoka. Akasafiri mbali katika nchi nyingine. Huko alipoteza pesa zake zote katika starehe na anasa. 14 Baada ya kutumia vyote alivyokuwa navyo, kukatokea njaa kali katika nchi ile yote. Akawa na njaa na mhitaji wa pesa. 15 Hivyo alikwenda kutafuta kazi kwa mwenyeji mmoja wa nchi ile, naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 Alikuwa anasikia njaa kiasi kwamba alikuwa anatamani kula chakula walichokula nguruwe. Lakini hakuna mtu aliyempa chakula.
17 Alipotambua namna alivyokuwa mjinga, akafikiri moyoni mwake na kusema, ‘Wafanyakazi wote wa baba yangu wana chakula kingi. Lakini niko hapa kama niliyekufa kwa sababu sina chakula. 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu. Nitamwambia hivi: Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe. 19 Sistahili kuitwa mwanao tena. Lakini niruhusu niwe kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ 20 Hivyo akaondoka na kurudi kwa baba yake.
Alipokuwa mbali na nyumbani kwao, baba yake alimwona, akamwonea huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia na kumbusu sana. 21 Mwanaye akasema, ‘Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe; sistahili kuitwa mwanao tena.’
22 Lakini baba akawaambia watumishi wake, ‘Fanyeni haraka, leteni vazi maalumu, mvikeni. Pia, mvisheni viatu vizuri na pete kwenye kidole chake. 23 Na leteni ndama aliyenona, mchinjeni ili tule na kusherehekea. 24 Kwa sababu mwanangu alikuwa amekufa, lakini sasa yuko hai tena! Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kusherehekea.
25 Mwanaye mkubwa alikuwa shambani. Alipoikaribia nyumba, alisikia sauti za muziki na kucheza. 26 Akaita mmoja wa watumishi na akamwuliza, ‘Kuna nini?’ 27 Mtumishi akasema, ‘Mdogo wako amerudi, na baba yako amechinja ndama aliyenona. Anafurahi kwa sababu amempata mwanaye akiwa salama na mzima.’
28 Mwana mkubwa alikasirika na hakutaka kwenda kwenye sherehe. Hivyo baba yake akatoka nje kumsihi. 29 Lakini alimwambia baba yake, ‘Tazama, miaka yote hii nimekutumikia kama mtumishi, kamwe sijaacha kukutii! Lakini hujawahi kunipa hata mbuzi mdogo ili nisherehekee pamoja na rafiki zangu. 30 Lakini alipokuja huyu mwanao aliyepoteza mali zako kwa makahaba, umemchinjia ndama aliyenona!’
31 Baba yake akamwambia, ‘Mwanangu, daima umekuwa pamoja nami, na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32 Lakini tulipaswa kusherehekea. Mdogo wako alikuwa amekufa, lakini sasa ni hai tena. Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”
Makusanyo kwa Ajili ya Waamini Katika Uyahudi
16 Sasa, kuhusu mchango wa pesa kwa ajili ya watu wa Mungu: Fanyeni kama nilivyoyaambia makanisa ya Galatia kufanya. 2 Siku ya kwanza ya kila wiki, kila mmoja wenu achukue kiasi cha pesa kutoka kwenye pesa zake na azitenge. Akusanye kiasi anachoweza kutokana na anavyobarikiwa. Na hivyo hamtahitaji kukusanya nitakapokuja. 3 Nitakapofika, nitatuma baadhi ya watu wapeleke sadaka yenu Yerusalemu. Hawa watakuwa wale ambao ninyi mtakubali kuwa waende. Nitawatuma na barua ya utambulisho. 4 Ikiwa itakuwa vizuri kwangu kwenda pia, basi tutasafiri pamoja.
Mipango ya Paulo
5 Nimepanga kupitia Makedonia, hivyo nitakuja kwenu baada ya hapo. 6 Pengine nitakaa kwenu kwa muda. Pengine nitakaa kwenu majira yote ya baridi. Hivyo mtaweza kunisaidia katika safari yangu, kila ninapokwenda. 7 Sitaki kuja kuwaona sasa, kwa sababu nitaweza tu kukaa nanyi kwa muda mfupi, kabla haijanilazimu kwenda mahali pengine. Ninategemea kukaa pamoja nanyi kwa muda mrefu, ikiwa Bwana ataruhusu. 8 Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste. 9 Nitakaa hapa, kwa sababu sasa nimepewa fursa nzuri kwa kazi kubwa na inayokua. Na kuna watu wengi wanaopinga.
10 Timotheo atakapokuja kwenu, mjitahidi akae kwa raha na amani akiwa kwenu. Anafanya kazi kwa ajili ya Bwana kama mimi. 11 Hivyo yeyote miongoni mwenu asikatae kumpokea Timotheo. Msaidieni aendelee katika safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu. Ninategemea atakuja kwangu pamoja na ndugu wengine.
12 Na sasa kuhusu Apolo: Ninamsihi sana aje na ndugu wengine kuwatembelea ninyi huko Korintho. Hajataka kuja sasa, lakini atakuja kwenu atakapopata nafasi.
Paulo Amalizia Barua Yake
13 Iweni waangalifu. Simameni imara katika imani yenu. Mwe jasiri na wenye nguvu. 14 Fanyeni kila kitu katika upendo.
15 Mnajua kuwa Stefana na familia yake walikuwa waamini wa kwanza katika Akaya. Wamejitia katika kazi ya kuwahudumia watu wa Mungu. Ndugu zangu, ninawaomba, 16 mjiweke chini ya uongozi wa watu kama hawa na wengine wanaofanya kazi kwa bidii na kutumika pamoja nao.
17 Ninafurahi kwa sababu Stefana, Fortunato na Akaiko wamekuja. Hamko hapa pamoja nami lakini wamejaza nafasi yenu. 18 Wamekuwa faraja kuu kwangu na kwenu pia. Basi, mnapaswa kuitambua thamani ya watu kama hawa.
19 Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Priska wanawasalimu katika Bwana. Na kanisa linalokutana nyumbani mwao linawasalimu pia. 20 Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kila mmoja wenu kwa salamu maalum ya watu wa Mungu.[a]
21 Hii ni salamu yangu kwa mkono wangu mwenyewe: Paulo.
22 Ikiwa mtu yeyote hampendi Bwana, mwacheni mtu huyo abaki chini ya laana ya Mungu.
Njoo, Ewe Bwana![b]
23 Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja nanyi.
24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu.
© 2017 Bible League International