M’Cheyne Bible Reading Plan
Kuzaliwa kwa Yesu
(Mt 1:18-25)
2 Ulikuwa wakati ambapo amri ilitolewa na Kaisari Augusto kwamba watu wote wanaoishi katika utawala wote wa Rumi[a] wahesabiwe na kuorodheshwa[b] katika kumbukumbu za serikali. 2 Orodha hii ilikuwa ya kwanza tangu Kirenio alipokuwa gavana wa Shamu. 3 Kila mtu alikwenda katika mji aliozaliwa ili akahesabiwe na kuingizwa katika orodha hiyo.
4 Hivyo Yusufu alitoka Nazareti, mji uliokuwa katika jimbo la Galilaya na kwenda katika mji wa Bethlehemu uliokuwa katika jimbo la Uyahudi. Pia, mji huu ulijulikana kama mji wa Daudi. Yusufu alikwenda Bethlehemu kwa sababu alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Daudi. 5 Yusufu alijiandikisha akiwa pamoja na Mariamu kwani alikuwa tayari amemchumbia ili amwoe. Na Mariamu alikuwa mjamzito. 6 Yusufu na Mariamu walipokuwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu kujifungua ulifika. 7 Akamzaa mwanawe wa kwanza. Akamvingirishia nguo vizuri, kisha akamlaza katika hori la kulishia mifugo.[c] Walimweka humo kwa sababu chumba cha wageni kilikuwa kimejaa.
Wachungaji wa Mifugo Wajulishwa Kuhusu Yesu
8 Usiku ule, baadhi ya wachungaji walikuwa mashambani nje ya mji wa Bethlehemu wakilinda kondoo zao. 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukaangaza kuwazunguka, wakaogopa sana. 10 Malaika akawaambia, “Msiogope, kwa kuwa nimewaletea habari njema zitakazowafurahisha watu wa Mungu wote. 11 Kwa sababu leo katika mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo,[d] Bwana. 12 Na hivi ndivyo mtakavyomtambua: Mtamkuta mtoto mchanga amevingirishiwa nguo na amelala katika hori la kulishia mifugo.”
13 Kisha malaika pamoja na jeshi kubwa la mbinguni wakaanza kumsifu Mungu, wakisema:
14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
na amani iwepo duniani
kwa watu wote wanaompendeza.”
15 Malaika walipoondoka kurudi mbinguni, wale wachungaji wakaambiana wakisema, “Twendeni Bethlehemu, tukalione jambo hili lililotokea, ambalo Bwana ametujulisha.”
16 Wakaenda haraka, wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala katika hori la kulishia mifugo. 17 Wachungaji walipomwona huyo mtoto, walisimulia kile walichoambiwa na malaika kuhusu mtoto. 18 Kila aliyesikia maelezo ya wachungaji, alishangaa. 19 Mariamu aliendelea kuyatafakari mambo haya, na kuyaweka moyoni. 20 Wachungaji waliirudia mifugo yao, wakawa wanamsifu na kumshukuru Mungu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona. Ilikuwa kama walivyoambiwa na malaika.
21 Ilipofika siku ya nane mtoto alitahiriwa, akaitwa Yesu. Hili ndilo jina alilopewa na malaika kabla mama yake hajaibeba mimba yake.
Yesu Atambulishwa Hekaluni
22 Muda wa kutakaswa ulimalizika, kama ilivyotakiwa na Sheria ya Musa baada ya mtoto kuzaliwa.[e] Baada ya hapo walimpeleka Yesu Yerusalemu na kumweka mbele za Bwana. 23 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana: Mzaliwa wa kwanza akiwa mtoto wa kiume, atolewe wakfu kwa ajili ya Bwana.[f] 24 Pia Mariamu na Yusufu walikwenda Yerusalemu kutoa dhabihu kama Sheria ya Bwana inavyosema kuwa, “Ni lazima utoe dhabihu ya jozi moja ya hua[g] au makinda mawili wa njiwa.”
Simeoni Amwona Yesu
25 Alikuwepo mtu mmoja aliyeishi katika mji wa Yerusalemu, mtu huyu aliitwa Simeoni. Alikuwa mtu mwema na mcha Mungu na Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Alikuwa akiusubiri wakati ambao Mungu angeisaidia Israeli. 26 Roho Mtakatifu alimwambia kwamba asingekufa kabla ya kumwona Masihi kutoka kwa Bwana. 27 Roho Mtakatifu alimwongoza mpaka Hekaluni. Hivyo, alikuwemo Hekaluni wakati Mariamu na Yusufu walipomleta mtoto Yesu ili wamfanyie kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Kiyahudi. 28 Simeoni alimbeba mtoto Yesu mikononi mwake, akamshukuru Mungu na kusema,
29 “Sasa, Bwana, niruhusu mimi mtumishi wako nife kwa amani
kwa kuwa umeitimiza ahadi yako kwangu.
30 Nimeona kwa macho yangu namna utakavyowaokoa watu wako.
31 Sasa watu wote wanaweza kuuona mpango wako.
32 Yeye ni mwanga wa kuionesha njia yako kwa mataifa mengine,
na atawaletea heshima watu wako Israeli.”
33 Mariamu na Yusufu walishangazwa sana na maneno aliyosema Simeoni kuhusu Yesu. 34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu; “Wayahudi wengi wataanguka na wengi watainuka kwa sababu ya mtoto huyu. Atakuwa ishara kutoka kwa Mungu, lakini baadhi ya watu watamkataa. 35 Mawazo ya siri ya watu wengi yatajulikana. Na mambo yatakayotokea yatakuumiza, kama upanga unaokuchoma moyoni.”
Ana Amwona Yesu
36 Alikuwapo nabii aliyeitwa Ana binti Fanueli, kutoka katika kabila la Asheri. Alikuwa mwanamke mzee sana. Aliishi na mume wake kwa miaka saba, 37 kabla ya mume wake kufa na kumwacha peke yake. Na sasa alikuwa na umri wa miaka themanini na nne. Ana alikuwa Hekaluni daima, hakutoka. Alimwabudu Mungu kwa kufunga na kuomba usiku na mchana.
38 Simeoni alipokuwa anazungumza na Yusufu na Mariamu, Ana alikwenda walipokuwa na akaanza kumsifu Mungu na kuwaambia kuhusu Yesu watu wote waliokuwa wanasubiri Mungu kuikomboa Yerusalemu.
Yusufu, Mariamu na Yesu Warudi Nyumbani
39 Yusufu na Mariamu walipotimiza mambo yote yanayotakiwa katika sheria ya Bwana, walirudi Galilaya, katika mji wao wa Nazareti. 40 Mtoto Yesu aliendelea kukua na kuwa kijana mwenye nguvu na aliyejaa hekima nyingi. Na Mungu alikuwa anambariki.
Yesu Akiwa Mvulana
41 Kila mwaka wazazi wa Yesu walikwenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. 42 Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walikwenda kwenye sikukuu kama ilivyokuwa desturi ya Kiyahudi. 43 Sikukuu ilipokwisha, walirudi nyumbani, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kutambua. 44 Walianza kumtafuta kwa jamaa na rafiki zao baada ya kusafiri kutwa nzima, wakidhani kuwa alikuwa pamoja nao katika msafara. 45 Walipomkosa, walirudi Yerusalemu kumtafuta.
46 Ikawa baada ya siku tatu wakamkuta Hekaluni, amekaa katikati ya walimu wa dini, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Na wote waliomsikiliza walishangazwa sana kwa ufahamu wake na majibu yake ya busara. 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa pia, ndipo mama yake akamwambia, “Mwanangu, kwa nini umefanya hivi? Mimi na baba yako tulikuwa na wasiwasi sana, na tumekuwa tukikutafuta.”
49 Yesu akawaambia, “Kwa nini mlikuwa mnanitafuta? Mnapaswa kujua kuwa inanilazimu kuwemo nyumbani mwa Baba yangu?” 50 Lakini wao hawakuelewa alichowaambia.
51 Yesu alirudi pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii. Mama yake aliendelea kuyaweka mambo haya yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Walimu ni Watumishi tu wa Mungu
3 Ndugu zangu, nilipokuwa kwenu, sikuzungumza nanyi kama ninavyozungumza na watu wanaoongozwa na Roho. Nilizungumza nanyi kama watu wa kawaida wa duniani. Mlikuwa kama watoto katika Kristo. 2 Mafundisho niliyowafundisha yalikuwa kama maziwa, siyo chakula kigumu. Nilifanya hivi kwa kuwa hamkuwa tayari kwa chakula kigumu. Na hata sasa hamjawa tayari. 3 Bado hamwenendi katika Roho, mnaoneana wivu na mnabishana ninyi kwa ninyi kila wakati. Hii inaonesha kuwa bado mnazifuata tamaa zenu wenyewe. Mnaenenda kama watu wa kawaida wa ulimwengu huu. 4 Mmoja wenu anasema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine anasema, “Ninamfuata Apolo.” Mnaposema mambo kama haya, mnaenenda kama watu wa ulimwengu.
5 Je, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Apolo na mimi si watumishi tu ambao Mungu alitutumia ili mmwamini Yesu Kristo. Kila mmoja wetu alifanya kazi aliyopewa na Bwana. 6 Nilipanda mbegu na Apolo akamwagilia maji. Lakini Mungu ndiye aliyeiotesha na kuikuza. 7 Hivyo aliyepanda na kuimwagilia si wa muhimu. Mungu ndiye wa muhimu, kwa sababu ndiye anayevifanya vitu viote vikue. 8 Anayepanda na anayemwagilia maji wote wana nia moja. Na kila mmoja atalipwa kutokana na kazi yake yeye mwenyewe. 9 Ninyi ni shamba la Mungu, ambamo tulifanya kazi pamoja kwa ajili yake.
Nanyi pia ni jengo la Mungu. 10 Nami kama mjenzi stadi nilijenga msingi wa nyumba hiyo kwa kutumia karama alizonipa Mungu. Wengine wanajenga pia katika msingi huo. Lakini kila mtu lazima awe mwangalifu kwa namna anavyojenga. 11 Yesu Kristo ndiye msingi uliokwishajengwa, na hakuna yeyote anayeweza kujenga msingi mwingine. 12 Watu wanaweza kujenga juu ya msingi huo kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, mbao, nyasi au majani. 13 Kila kazi atakayoifanya kila mtu itaonekana siku ya hukumu itakapofika, na itaonekana ilivyo mbaya au nzuri. Siku hiyo kila kazi ya mtu itajaribiwa kwa moto. 14 Mungu atampa thawabu mtu anayejenga juu ya msingi huu ikiwa kazi yake haitateketea kwa moto. 15 Lakini ikiwa itateketea atapata hasara. Lakini yeye mwenyewe ataokolewa, lakini itakuwa kama mtu anayeokolewa kutoka kwenye moto.
16 Hakika mnajua kuwa ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. 17 Ndiyo, ninyi nyote kwa pamoja ni Hekalu la Mungu. Na yeyote atakayeliharibu Hekalu la Mungu ataadhibiwa na Mungu, kwa sababu Hekalu la Mungu ni mali yake yeye mwenyewe.
18 Msijidanganye. Yeyote anayejiona kuwa ana hekima kwa viwango vya ulimwengu huu, basi na awe mpumbavu. Hiyo ndiyo njia pekee itakayomfanya kuwa na hekima. 19 Ninasema hivi kwa sababu hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu huwanasa katika mitego yao wenyewe wale wanaojidhania kuwa na hekima.”(A) 20 Pia Maandiko yanasema, “Bwana anajua mawazo ya wenye hekima. Anajua kuwa mawazo yao hayana maana.”(B) 21 Hivyo hakuna mtu yeyote duniani ambaye ninyi mnapaswa kujivunia. Kila kitu ni chenu: 22 Paulo, Apolo, Petro, ulimwengu, uzima, mauti, wakati uliopo na ujao, vyote hivi ni vyenu. 23 Ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.
© 2017 Bible League International